January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Simba, Chama wang’ara tuzo VPL

Na Penina Malundo, TimesMajira Online

KLABU ya Simba imefanikiwa kuzoa tuzo nyingi zaidi huku kiungo wake Mzambia Clatous Chama akishinda tuzo mbili katika sherehe za Tuzo za Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL) zilizofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.

Katika sherehe hizo za kukabidhi zawadi mbalimbali kwa wachezaji, viongozi na klabu zilizofanya vizuri msimu uliomalika Chama ametwaa tuzo ya Mchezaji Bora na kuondoka na kitita cha Sh. milioni akiwapiku Nicolas Wadada wa Azam FC na Bakari Mwamnyeto wa Coastal Union.

Pia amechukua tuzo ya Kiungo Bora akiwashinda Lucas Kikoti wa Namungo na Mapinduzi Balama wa Yanga na kuchukua Sh. Milioni 3 akiongoza kwa kutengeneza pasi 10 za mwisho za magoli pamoja na kufunga goli mbili.

Mbali na Chama, kocha mkuu wa timu hiyo, Sven Vandebroeck kutangazwa kuwa Kocha Bora wa msimu akiwapiku kocha wa Azam, Aristica Cioaba na Thiery Hitimana wa Namungo FC.

Kwa upande wa Simba tuzo nyingine waliyojinyakulia ni tuzo ya kipa bora aliyochukua Aishi Manula akiwashinda Daniel Mgore wa Biashara United na Nouridine Balora wa Namungo.

Kipa Aishi Manula kwa mara nyingine amechukua tuzo ya Kipa Bora akiwashinda Nourdine Balora wa Namungo FC na Daniel Mgore wa Biashara United.

Beki wa Azam FC, Nicolas Wadada amewagaragaza Bakari Mwamnyeto na David Kuhende katika kipengele cha Beki Bora, uzo ya Mchezaji Bora Chipukizi ikienda kwa Novatus Dissmas wa Biashara United akiwazidi Dickson Job wa Mtibwa Sugar na Kelvin Kijiri wa KMC na Wakati Tuzo ya Bao Bora ikaenda kwa Patson Shikala wa Mbeya City akiwashinda Luis Miquissone wa Simba na Sadallah Lipangile wa KMC.

Kwa upande wa Waamuzi, Ramadhan Kayoko wa Dar es Salaam ameshinda Tuzo ya Mwamuzi Bora iliyokuwa ikishindaniwa pia na Ahmed Arajiga wa Manyara na Abdallah Mwinyimkuu wa Singida wakati Frank Komba pia wa Dar es Salaam akiwashinda Abdulaziz Ally wa Arusha na Hamdani Said wa Mtwara katika tuzo ya Mwamuzi Msaidizi.

Hata hivyo katika tuzo mpya ya Seti Bora ya Waamuzi walioshinda ni Athumani Lazi wa Morogoro, Abdallah Mwinyimkuu wa Dar es Salaam, Ferdinand Chacha wa Mwanza na Mohamed Mkono wa Tanga.

Kagera Sugar ya Bukoba imeshinda Tuzo ya Timu yenye Nidhamu iliyokuwa pia inawaniwa na Coastal Union ya Tanga na Mwadui FC ya Shinyanga huku mchezaji wa zamani wa klabu ya Yanga, Sunday Ramadhan Manara akipewa Tuzo ya Heshima kutokana na mchango wake mkubwa katika soka.

Katika tuzo nyingine ambazo tayari washindi wake walikuwa wanajulikana, mabingwa klabu ya Simba wameondoka na Sh. Milioni 100, washindi wa pili, Yanga Sh. Milioni 45, Azam walionaliza nafasi ya tatu wamekabidhiwa Sh. Milioni 30 na washindi wa nne, Namungo FC S. Milioni 10 wakati kinara wa mabao aliyepachika magoli 22, Meddie Kagere wa Simba aliondoka na Sh. milioni 10.

Kwa upande wa Kikosi Bora cha msimu wa 2019/20, Simba wametoa wachezaji sita golini akikaa Aishi Manula (Simba), Nico Wadada (Azam), David Luhende (Kagera Sugar) Bakari Mwanyeto (Coastal Union), Sergie Wawa (Simba), Zawadi Mauya (Kagera Sugar), Lucas Kikoti (Namungo), Clatous Chama (Simba), Meddie Kagere (Simba), John Bocco (Simba), Luis Miquissone (Simba).