November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela John Wanga akionyesha ufunguo wa bajaji mara baada ya kukabidhiwa na Meneja Mpango wa Usafi wa Shirika la Amref Health Africa Tanzania Mhandisi Mturi James(kulia mwenye tisheti nyeusi) kwa niaba ya Mkurungezi wa Shirika hilo, ambapo Halmashauri hiyo ilipewa bajaji mbili kwa ajili ya mradi wa kuboresha usafi wa mazingira kwa watu wenye kipato cha chini kibiashara Jijini Mwanza (PRO POOR WASH ENTREPRISE.

Walengwa 125,000 kunufaika na mradi wa mazingira

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online Mwanza

WALENGWA 125,000 wa Wilaya ya Ilemela na Nyamagana wanatarajia kufikiwa na mradi wa kuboresha usafi wa mazingira kwa watu wenye kipato cha chini kibiashara Jijini Mwanza(PRO POOR WASH ENTREPRISE).

Mradi huo ambao unatekelezwa na Shirika la Amref Health Africa Tanzania kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza kwa ufadhili wa Manispaa ya Jiji la Madrid nchini Hispania umelenga kusaidia juhudi za Serikali ya Tanzania kuongeza na kuboresha huduma za usafi wa mazingira kupitia kampeni ya kitaifa ya NSC-II(2016-2020).

Akizungumza wakati akikabidhi bajaji nne zenye thamani ya milioni 30 kwa Halmashauri ya Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela ambazo zitatumiwa na vikundi vya kukusanya taka taka kutoka Kata nne ambazo mradi huo ndio unafanya kazi, Meneja Mpango wa Usafi wa Shirika la Amref Health Africa nchini Tanzania, Mhandisi Mturi James kwa niaba ya Mkurungezi wa Shirika hilo nchini hapa amesema, mradi huo unatarajia kuongeza fursa kwa jamii nzima katika uelewa na mahitaji ya kusimamia na kuondoa taka katika maeneo ya makazi ambao unatekelezwa katika Kata za Kirumba na Nyamanoro Wilaya ya Ilemela huku kwa Nyamagana Kata ya Mkuyuni na Buhongwa.

Mhandisi James amesema, pia unalenga kuwawezesha na kuwanufaisha wakina mama na vijana katika maeneo ya wakazi wenye kipato cha chini kwa kuwezesha kupata fursa za kuongeza kipato na kuwakuza kiuchumi kwa kufanya ujasiriamali kwa kuzalisha bidhaa mbadala kutokana na taka ngumu na taka vinyesi.

Amesema, kwa kushirikiana na uongozi wa kata na mitaa husika, wamefanikiwa kutambua vikundi vinne vinavyojihusisha na ujasiriamali wa usafi wa mazingira ambavyo wamevipatia mafunzo ya ujasiriamali wa usafi wa mazingira na wamewapatia bajaji (kila kata bajaji moja moja) ili waweze kutoa huduma za kuzoa na kusafirisha taka hadi kwenye vituo vya kuchakata taka.

Kwa sasa mradi huo unaendelea na ujenzi wa vituo vya kuchakata taka katika Kata ya Nyamanoro ambao upo katika hatua za mwisho huku Kata ya Buhongwa kituo kipo hatua za awali za ujenzi ambapo vituo hivyo vitakapo kamilika wajasirimali hao watafanya shughuli za uchakataji wa taka kwa ajili ya kutengeneza bidhaa mbadala kama vile mkaa,mbolea na gesi.

“Tumefanya mafunzo kwa wahudumu wa afya 198 na viongozi wa kijamii 95 kutoka maeneo mbalimbali ya kata hizi kwa ajili ya kusaidia kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa njia bora za udhibiti wa taka ngumu na taka vinyesi kwa ngazi ya kaya ikiwemo utenganishaji wa taka ngumu ili kurahisisha zoezi la uchakataji wa taka hizo kwa ajili ya kutengeneza mkaa mbadala,mbolea na gesi,” amesema Mhandisi James.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Usafi na Mazingira wa Halmashauri hiyo, Danford Kamunya amesema, Jiji la Mwanza linazalisha kwa siku wastani wa tani 250 za taka ambapo kwa mazingira ya eneo hilo wanafikia asilimia 50 ya wakazi wetu kwani tukiangalia maeneo mengine yapo kwenye miinuko ambayo hayawezi kufikiwa na magari ya kuzolea taka.

“Tumepokea pikipiki za magurudumu matatu (bajaji) mbili kwa ajili ya kusaidia ukusanyaji wa taka kwenye maeneo ya Jiji la Mwanza zitasaidia kupanua wigo wa uzoaji taka katika Kata ya Mkuyuni na Buhongwa kwani mazingira ndio kila kitu na ukiyaharibu ni hatari kwa afya ya jamii, tunaamini mazingira yakiwa safi jamii itakuwa na afya njema ambayo itasaidia kufanya shughuli zao za kiuchumi na kuleta maendeleo ya taifa,” amesema kiongopzi huyo.

Pia amewataka watendaji wa kata husika kusimamia bajaji hizo na zifanye kazi iliyokusudiwa ya kuzoa taka tu na si vinginevyo pia watafute dereva mwenye leseni atakayeendesha bajaji hizo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela John Wanga, amelishukuru shirika hilo kwa kuguswa kushirikiana na Serikali kupitia Halmashauri hiyo ya Ilemela kwa suala la uondoaji taka katika maeneo ya Manispaa hiyo.

“Halmashauri ndio mhusika mkuu wa kuhakikisha wananchi wanaishi katika maeneo safi kwani wakiwa na afya njema itasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa, pia nawapongeza kwa kusema wameenda mbali kwa kuanzisha na kujenga kituo cha mafunzo ya kutengeneza mkaa kupitia taka taka jambo ambalo litasaidia kuokoa miti na kuweka mazingira safi na salama huku elimu watakayo ipata itasaidia wananchi kutumia majiko au mkaa bila ya kukata miti,” amesema Wanga.

Ofisa Usafishaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Daniel Paul,amesema Halmashauri hiyo kwa siku inazalisha tani 479 za taka na wanafikia asilimia 73 huku na tani zinazibaki zipo kwenye maeneo ya vijijini.