November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye.

Mwenyekiti wa CCM Mara ampongeza Rais Dkt.Magufuli kwa hotuba bora, asema ni mwendo wa maombi, Mungu atatenda

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Mara

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye (Namba Tatu) amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt.John Magufuli kwa kutoa hotuba fupi bora jana, yenye mwelekeo wa kuendelea kuipaisha Tanzania zaidi katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Kiboye ametoa pongezi hizo wakati akizungumza leo Agosti 7,2020 mkoani hapa kuelezea juu ya namna ambavyo hotuba ya Rais Dkt. Magufuli baada ya kupokea fomu ya kuwania urais kwa awamu ya pili kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jijini Dodoma jana ilivyokuwa imejaa mambo ya msingi kwa mustakabali wa Taifa letu.

Amesema, hotuba ya jana ilikuwa na mashiko na imegusa Watanzania wengi, hivyo wataendelea kumuombea ili Oktoba 28, mwaka huu akaandike historia kubwa kupitia ushindi wa kishindo.

“Kila ninapotafakati na tunapotafakari juu ya mambo mengi makubwa ambayo Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli amelifanyia Taifa letu ndani ya miaka mitano, tunakosa jibu la kuwapa wenye tabia ya kubeza kila kitu. Itoshe tu kusema, bado Watanzania tuna imani na Rais Magufuli na ingekuwa ni maamuzi yangu ningesema aendelee tu hata baada ya miaka mitano.

“Kila kona sasa tunashuhudia shughuli mbalimbali za maendeleo iwe barabara,elimu, afya, maji, nishati inang’arisha kila kona hata vile vijiji ambavyo hatukutarajia kuna siku vitapata nishati hiyo, na muda huu ninaoongeza watu wapo kazini wanaendelea kufanya mambo makubwa kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu, lazima tuendelee kumuombea na kumlinda Rais wetu ili wenye nia ovu wasipate nafasi ya kumkwamisha hata dakika moja,”amesema Kiboye.

Jana wakati Rais Dkt.Magufuli ambaye ni mgombea wa kiti cha urais na anayetetea kiti chake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu katika ofisi za NEC jijini Dodoma alisema,ameamua kuchukua fomu yeye na Mgombea Mwenza Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kipindi kingine cha miaka mitano ili wakamilishe miradi mingi ya maendeleo waliyoianza awali.

“Tumefanya mambo mengi katika kipindi hiki,tumejenga shule za msingi zaidi ya 908,shule za sekondari zaidi ya 228,vituo vya afya zaidi ya 500,mambo mengi mno yamefanyika. Mfano ukiangalia Dodoma tu tumefanya upanuzi wa uwanja wa ndege.

“Tumeweka taa za barabarani,majengo mengi yamejengwa,kuna program ya kujenga barabara ya njia nne yenye urefu wa kilomita 110 ambayo imetengewa zaidi ya shilingi bilioni 700,uwanja wa ndege wa Msalato umetengewa shilingi milioni 600,fedha hizi zipo. Kwa hiyo nikiangalia sioni mwingine wa kuja kuyafanya hayo,tunajenga reli ya mwendokasi ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 87 kwa kipande cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro na kipande cha Morogoro-Dodoma ujenzi wake umefikia asilimia 32 na tunahitaji tuendelee mpaka Mwanza,nikiacha,yataachiwa pale,ndio maana nimeona tugombee tena na Mama Samia,”alisema Dkt,Magufuli

Pia alisema,katika kipindi chake cha miaka mitano umeme umesambazwa katika vijiji 9,402 kutoka vijiji 3,000 wakati wanaingia madarakani na vimebaki vijiji 3,000 ambavyo alisema havitamshinda kuvifikia kwa miaka mitano.