November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimelitaka Jeshi la Polisi nchini kutokibeba chama chochote cha kisiasa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa,badala lishiriki ipasavyo kuwashughulikia wenye nia ovu ya kufanya udanganyifu kwenye uchaguzi huo na si kujiegemeza upande mmoja.

Kipenga cha kampeni za uchaguzi wa Serikali za mitaa kimepigwa Novemba,20,2024 na wagombea wakijinadi kila mahali.

Akizungumza wakati wa muendelezo wa ufunguzi wa kampeni za chama hicho,Novemba 21,2024, zilizofanyika eneo la Komesho jijini Tanga,Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar Ismail Jussa,amesema hawatamani kuona vyombo vya ulinzi vikijiegemeza kwenye upande mmoja.

“Niwaombe polisi wanaotulinda kila wakati,mara nyingi vituko huanza usiku wa kuamkia tarehe ya uchaguzi, hivyo nawaomba Novemba 27,2024,mfanye kazi yao kwa mujibu wa Katiba na Sheria,inavyowataka kulinda raia na mali zao.Muwalinde raia wafanye chaguo lao kwa uhuru na kwa haki,”amesisitiza Jussa.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT -Wazalendo, Taifa Rehema Ally Mohamed,amewatahadharisha mawakala kuwa makini na mamluki wanaoweza kutumiwa vibaya kwenye uchaguzi huo.

“Mkimuona mtu hajajiandikisha anakuja kupiga kura kwa jina la mtu,malizaneni naye,ng’ombe atakavyolala ndio atakavyochinjwa,uoga sasa basi kwani wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini msiogope kwenye Mkoa wa Tanga tumeweka wanasheria wane watakaodili na kesi za uchaguzi tu kwahiyo msiogope,”alibainisha Rehema.

Ili uchaguzi uwe huru na wa haki wananchi wanatakiwa kuachiwa uhuru wa kumchagua kiongozi wanayemtaka bila kushawishiwa kwa fedha na vitu vongine vinavyoweza kusababisha washindwe kufanya maamuzi sahihi kwa ajili ya maendeleo yao.