November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online,Ileje

MKUU wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi, amekabidhi mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kwa vikundi vilivyokidhi vigezo, akivihimiza kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili viweze kuirejesha na wengine waweze kukopo.

DC Mgomi alitoa kauli hiyo,Novemba 20, mwaka huu kwenye hafla ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya hiyo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu iliyofanyika katika ukumbi wa Community Center uliopo wilayani hapa.

DC Mgomi alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kujali masilahi ya wananchi wa Wilaya ya Ileje kupitia mikopo hiyo inayolenga kuimarisha hali ya kiuchumi ya vikundi vya maendeleo.

Aidha, alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Nuru Waziri Kindamba kwa kusimamia na kuhakikisha zoezi la utoaji wa mikopo linakwenda vizuri.

Amesema kwa taarifa fupi ambayo aliipokea kutoka kwenye risala ambayo imetolewa mbele yao na neno la utangulizi ambalo limetolewa na Mkurugenzi (Kindamba) sh. milioni 626.7 ndizo zimetengwa kutoka Halmashauri ya Wilaya Ileje kwa ajili ya vikundi kuweza kupatiwa mikopo.

“Lakini kwa taarifa ambazo tumepewa leo zaidi ya sh. milioni 700 zipo kwa ajili ya kuendelea kupewa watu mikopo kwa maana ya ongezeko la zaidi ya sh. milioni 100 kutoka kwenye sh. milioni 626.7 ambazo tayari zimeishachakatwa, kwa maana hiyo kazi leo inaanza na inaendelea kwa kadri siku zinavyokwenda watu bado wana fursa ya kuendelea kuomba na kupatiwa mikopo kama ambavyo hapa mkurugenzi ameweza kutoa neno la utangulizi,”amesema DC Mgomi.

Aidha,amesema kwa taarifa alizopata ni kata 13 kati ya 18 ndizo ambazo zimeweza kuomba na kupatiwa mikopo, hiyo.

“Kwa hiyo niombe zile kata nyingine tano zilizobaki na wenyewe ni sehemu ya Wilaya ya Ileje, bado wana fursa ya kutumia kuweza na wao kujiunga kwenye vikundi kuomba mkopo na hatimaye na wao kuweza kupatiwa,” amesema DC Mgomi na kuongeza;

“Lakini vile vile naambiwa vikundi ambavyo vimechakatwa mpaka kwenye hatua ya mwisho na kukidhi vigezo ni 51 na mlemavu mmoja, kati ya vikundi 51, vikundi 33 vya wanawake na 18 vya vijana, kwa maana hiyo wale ambao hawakuwa na sifa na vile vigezo na masharti wakivingatia na wenyewe bado wana fursa ya kuweza kupewa mikopo.”

Kwa wale ambao wamekidhi vigezo, DC Mgomi amewapongeza akisema,”Hongereni sana, rai yangu kwenu, kama mnavyojua kwamba unapokopa unatakiwa kurejesha, ahadi ni deni, ile pesa inavyorudishwa ndivyo inazunguka na wengine wanaendelea kukopa, kwa sababu kila mtu anatakiwa apate fursa ya kukopa.

Wewe ambaye umepata fursa ya kupata mkopo kafanyie kazi kile unachoomba kwa makusudi ya ule mkopo, lakini pia ahakikisha unarudisha unatoa rejesho kwa wakati.”

Amesema kuna wengine unakuta anachukua mkopo wala hajui ule mkopo anaenda kuufanyia nini pamoja na kusema anaenda kufuga kuku, sijui anakwenda kununua mazao, lakini akishapata mkopo anaenda kufanya kitu tofauti na makusudio ya ule mkopo, anaweza kufanyia kitu ambacho fedha ile haizuguki ili kusaidia kuweza kuleta rejesho.

“Lakini wengi kwa sababu sisi huku tuko mpakani unakuta mtu anakopa mkopo ukifika muda anaruka upande wa pili, anakwenda zake Malawi kwa sababu kule kuna mjomba wake, shangazi wake kuna mama yake mkubwa, kwa hiyo mimi nisingependa tuanze kufuatanafuatana kwa sababu hatutaki kulipa mkopo,”ameonya DC Mgomi.

Hata hivyo, amesema sema anawafahamu sana wananchi wa Ileje ni waungwana mno, kwa hiyo anategemea na kuamini kwamba mikopo hiyo itatumika ipasavyo.

“Maana yake kama biashara yako ikiende vizuri kama (jana) leo umekopa sh. milioni 5, ukirudisha maana yake ukifanya vizuri biashara yako imetanuka unaweza ukaja ukaomba sh. milioni 10, 15, 20,”amesema.