Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kuipa kipaumbele sekta ya kilimo ili kuleta tija kubwa kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa Tabora Neema Kapesa alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji shughuli za maendeleo katika Kikao cha Baraza la Madiwani.
Amesema kuwa katika kuhakikisha sekta ya kilimo inaendeshwa kisasa na kitaalamu wanafanya kazi kwa weledi mkubwa, serikali ya awamu ya 6 imewapatia vitendea kazi mbalimbali ikiwemo vishikwambi na usafiri.
Kapesa amebainisha kuwa jumla ya Vishikwambi 21 vimegawiwa kwa Maafisa Ugani wa Kata 21 kati ya 29 zilizopo katika manispaa hiyo ambazo zina Wataalamu wa Kilimo ili kuwarahishia utekelezaji majukumu yao kwa wakulima.
‘Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupatia vishikwambi kwa ajili ya Maafisa Ugani wote na hivi karibuni aliwapatia pikipiki zipatazo 20 kwa ajili ya ufuatiliaji shughuli za wakulima na juzi tumepokea gari jipya 1’, amesema.
Kapesa ametaja vifaa vingine vilivyoletwa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuchochea ufanisi wa sekta hiyo kuwa ni mavazi maalumu ya kazi kwa ajili ya maafisa ugani wote ikiwemo magari mapya 4 ya idara ya afya, elimu na ujenzi.
Akikakidhi vifaa hivyo kwa wahusika Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela amemshukuru sana Rais Samia kwa dhamira yake njema ya kuinua sekta ya kilimo nchini na kuwainua kiuchumi wakulima wote.
Amewataka kutumia vifaa hivyo kwa lengo lililokusudiwa ili kila mwananchi apate maendeleo na sio kuvitumia kwa matakwa binafsi huku wakulima wakiendelea kuhangaika pasipo msaada wowote.
Akiongea kwa niaba ya wenzake, Afisa Ugani wa Kata ya Malolo, Shaban Balangula ameishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kuwajali na kuwawezesha vitendea kazi huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii kubwa.
Amebainisha kuwa awali walikuwa wanashindwa kuwafikia wakulima wote katika maeneo yao kutokana na ukosefu wa usafiri lakini sasa hawana kisingizio chochote cha kushindwa kwenda vijijini kwa kuwa wana usafiri wa uhakika.
More Stories
TMDA:Toeni taarifa za ufuatiliaji usalama wa vifaa tiba ,vitendanishi
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo