November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Safari ya Dkt.Angeline kwenye siasa, baada ya kuacha kazi-sehemu ya kwanza

Na Judith Ferdinand

ZIPO nyakati unahitaji kujitoa ili kupigania kile unachokipenda au kukitamani ili uache alama kwenye jamii yako, hiki ndicho kilichomtokea Mbunge wa Jimbo la Ilemela (CCM), Dk. Angeline Mabula ambaye aliacha kazi yenye mshahara mnono na kuingia kwenye nafasi ya siasa isiyo na mshahara.

Ili kupata nafasi ya Ubunge alionayo sasa ilimlazimu kuanzia kwenye Udiwani Vitimaalum, aligombea jimboni mara tatu na kuanguka mara mbili lakini hakukata tamaa kwa kuwa kila hatua ilikuwa ni kujifunza.

Ukimuona Dkt.Angeline wa leo ambaye amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya za  Muleba,Butiama-Musoma na Iringa, pia Naibu Waziri na Waziri wa Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, unaweza kuona moja kwa moja aliibuka kwenye nafasi hiyo kumbe alipita njia ngumu yenye milima na mabonde ili kupigania kile alichoamini ndicho Mungu alichomtuma kukifanya duniani.

Dkt.Angeline alitamani kuwa karibu na jamii ili kuyajua na kuyaishi matatizo yao hasa kwa makundi ya wanawake, watoto na wenye mahitaji maalum na kutokana na hayo alianzisha Taasisi ya Angeline (The Angeline Foundation).

Kutokana na dhamira hiyo, Dk. Angeline amekuwa mwanamke wa kwanza kuongoza Jimbo la Ilemela tangu mwaka 2015, kisha akapewa jina la Nshimba Nkema.

Aliyekuwa Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Meneja kampeni wa Jimbo la Ilemela mwaka 2020, Kazungu Safari,anaeleza kuwa Oktoba 13,2019,uwanja wa kanisa la AICT Kabangaja,ndipo alipo mpa jina la Nshimba Nkema Dkt.Angeline Mabula.

“NShimba Nkema ni lugha ya kisukuma ikimanisha Simba Jike. Simba Jike ana sifa ya umahiri katika mawindo awapo nyikani, atapambana kwa kila hali kuhakikisha watoto wake wanapata chakula,”anaeleza Kazungu.

Katika mahojiano maalum na majira, Dkt. Angeline anasema kupitia  taasisi yake amefanya mambo mengi jimboni Ilemela ikiwemo kuwarejesha watoto wa kike zaidi ya 50, waliokatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali kuendelea na masomo.

Ni Oktoba 10, mwaka huu nabisha hodi nyumbani kwake,ananikaribisha na tabasamu pana ndipo mazungumzo yetu yanaanza kwa kunieleza safari yake kwenye siasa ambayo ni yenye milima, mabonde na mafanikio lukuki.

“Nimezaliwa Mei 6, 1962,Tafara ya Ngudu, wilayani Kwimba, mkoani Mwanza,ni mtoto wa saba kati ya 11,wa familia ya Sylivester Lubala na Cecilia Fidelix, ni mama wa watoto wa nne,na jina la Mabula ni la mume wangu,”anaeleza Dkt.Angeline.

Elimu ya msingi  ameipata  katika shule ya Kirumba Kata ya Kirumba wilayani Ilemela.1981 alihitimu elimu ya sekondari katika shule ya  Lake,iliopo Kata ya Mirongo wilayani Nyamagana mkoani Mwanza.Mwaka 1982, alijiunga na Chuo cha Uhasibu kilichopo Dar-es-Salaam na baadaye akajiriwa na Shirika la Ukaguzi Tanzania(Tanzania Audit Cooparation).

Anasema akiendelea na kazi aliendelea na masomo kwa kujiunga na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ambapo alipata Diploma ya Juu katika Uhasibu.Wakati akitumikia  nafasi ya Ukuu wa Wilaya  ya Butiama ,alikuchukua Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii na Uchumi katika Chuo Kikuu Huria Tanzania(Open University).

KUACHA KAZI

Anasema alianza kazi mwaka 1984 katika Shirika la Ukaguzi Tanzania (Tanzania Audit Corporation), alitumika kwa miaka 16, na aliamua kuacha kazi katika shirika hilo mwaka 2000, kwa kupenda mwenyewe kwa sababu aliwiwa kufanya kazi na wanawake, watoto, wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu kama mwakilishi wao.

“Mwaka huo,niliamua kuingia kwenye siasa na kuchaguliwa kuwa Diwani wa Viti maalumu (CCM),Jiji la Mwanza kabla alijatenganishwa na kuzaa halmashauri mbili za Ilemela na Jiji la Mwanza, nafasi nilioitumikia kwa kipindi kimoja cha 2000-2005.Watu walinishangaa kuacha kazi niliosomea na kukimbilia siasa,kipindi hicho Udiwani tulikuwa tunalipwa posho ya sh. 30,000,”anasimulia Dkt.Angeline na kuongeza:

“Ilikuwa ngumu kuacha kazi,nilipata upinzani kwa mume wangu,pia mwajiri wangu wa Tanzania Audit Corporation akutaka niache kazi,maana alinitegemea mimi nishike nafasi yake kwa sababu alikuwa anakaribia kustaafu,mara tatu walinikatalia,mwisho wa siku walikubali”. 

Anaendelea kusimulia kuwa,baada ya kuingia kwenye siasa mwaka 2000-2009,alitumikia Jimbo Kuu Katoliki la  Mwanza kama Mhasibu na Mratibu wa masuala ya kijinsia.

Akiwa kwenye nafasi ya Udiwani wa Vitimaalum Mwaka 2003, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Ilemela baada ya kuanzishwa  Wilaya  mpya ya Ilemela kisiasa nafasi alioitumikia kwa miaka 10.

ANGUKO KWENYE UBUNGE

“Nikiwa Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Ilemela,mwaka 2005 niligombea Ubunge wa Jimbo,wagombea tulikuwa 19, nilishika nafasi ya pili, mwanamke  pekee yangu.

“Kabla ya kugombea mara ya pili mwaka 2009,niliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba kwa mara ya kwanza, mwaka 2010, nikagombea tena Ubunge wa Viti Maalum  nikawa mshindi wa tatu.Nikaendelea na majukumu yangu ya Ukuu wa Wilaya,Mwaka 2012-2015,nikatumika kama mkuu wa Wilaya ya Butiama-Musoma,baada ya kuhamishiWa eneo hilo mwaka 2012,”anasimulia na kuongeza kuwa:

“Februari 2015 niliamishiwa kuwa Mkuu wa Wilaya Iringa, ambapo nilidumu mpaka Julai 2015,ambapo nilikuja na wazo la kugombea Ubunge kwa mara ya tatu,licha ya kuwa mara mbili nilithubutu lakini nilishindwa,sikukata tamaa wakati mwingine wanasema subira yavuta heri,”.

SAFARI KUSAKA UBUNGE 2015

Anasema baada ya kupata uzoefu kwa kuanguka mara mbili na kufanya kazi kwa karibu na jamii, alijitosa tena mwaka 2015 akapenya kwenye mchakato ndani ya chama na baadaye kuibuka kidedea kuperusha bendera ya CCM.

Anasema ugumu ulianza ndani ya chama chake kwenye kura za maoni kwa kuwa walikuwawagombea wanne naye ni mwanamke pekee lakini kwa uzoefu aliokuwa nao na kujipanga vyema aliibuka mshindi kwa kupata kura 7,000 na aliyemfuatia alipata kura 3,000

“Nikilinganisha wakati ule na sasa ule ulikuwa uchaguzi wa kistarabu, tofauti na sasa tunaona pilikapilika nyingi sana,”anasema.

Anasema baada ya kukamilisha mchakato huo kazi ngumu ikawa kushindana na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Highness Kiwia, ambaye baada ya mchuano mkali yeye (Dkt.Angeline) aliibuka mshindi kwa kura 85,424 dhidi ya mpinzani wake huyo aliyepata kura  takribani 61,000.

Kwa mujibu wa Dkt. Angeline, kwenye kugombea jimboni upinzani ulikuwa mkali sana kwa kuwa mchuano ulikuwa kwa wagombea 19 na haikuwa rahisi kumng’oa Mbunge aliyekuwepo wakati huo Highness Kiwia(CHADEMA).

“Mwaka 2020 niligombea tena ndani ya chama,tulijitokeza wagombea 72,wanawake tulikuwa 6,zilipigwa kura 685 nikapata kura 504,aliyenifuatia alipata  kura takribani 100.Na katika uchaguzi mkuu Wananchi walinipa kura baada ya kuona maendeleo nilioleta kwa kushirikiana nao,”.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Demokrasia (NDI), katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 wanawake waliochaguliwa kwa nafasi za ubunge ni asilimia 9.5,Wabunge wa Viti maalum ni asilimia 29, hivyo kufanya jumla ya wabunge 142 kati ya 393.

Vilevile, Ripoti ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ya mwaka 2020 inaonesha wanawake waliochaguzliwa kwa nafasi za udiwani walikuwa asilimia 6.58, viti maalum walikuwa 1,374 katika halmashauri 184 sawa na asilimia 24.59.Kwa ujumla wanawake walikuwa asilimia 29.24 ya madiwani wote nchi nzima.

Aidha, Ripoti ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka 2019 pia inaonesha kuwa kati ya nafasi 11,915za wenyeviti wa vijiji, wanawake walishinda nafasi 246 sawa na asilimia 2.1 huku wanaume wakishika asilimia 97.9 ya nafasi hizo. Kati ya nafasi 4,171 za wenyeviti wa mitaa, wanawake walishinda nafasi 528 sawa naasilimia 12.6.

 

Kwa mtazamo wa Dkt.Angeline, anasema hakuna sababu ya kumwekea kauzibe mgombea ambaye anazingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi zilizopo, kwa kuwa wananchi ndio huamua nani atawaongoza.

UKATILI KWENYE SIASA

“Wakati napanda jukwaani kuwania ubunge wa jimbo nilikutana na udhalilishaji wa kila aina, matusi ya kila aina kwasababu ni mwanamke,lakini niliyavumilia kwa kuwa nilijua nini nataka na sikutaka kuondoka kwenye kupigania ndoto yangu,”anasema.

“Changamoto zinazowakabili wanawake hata wanaume wanakutana nazo.Wanawake ni waoga kwa sababu mara nyingi wanapewa majina yasiyo ya kwao, hasa anapojitokeza kugombea,ataambiwa mhuni,malaya,anasema Dkt.Angeline na kuongeza:

“Wengi wanaogopa hayo na kuamua kurudi nyuma,mimi uwa nasema kama huyaishi,hauyafanyi,hauna sababu yakuyaogopa maana ndio siasa ilivyo.Unachotakiwa usiyazingatie yaingilie sikio hili yatoke sikio jingine. Afanye juhudi za kuonesha kinachosemwa siyo sawa,”anafafanua.

Utafiti uliofanywa na Umoja wa Mabunge ya Afrika (APU)mwaka 2021, ukihusisha Wabunge Wanawake 224 kutoka nchi 50 ikiwamo Tannzania, ulibaini kuwa asilimia 80 ya waliohojiwa walipitia ukatili wa kisaikolojia, huku asilimia 46 wakikumbana na ukatili wa kijinsia mtandaoni.

Pia Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ya mwaka 2023 inaonesha kuwapo ongezeko kubwa la udhalilishaji wa kidijitali na ukatili wa kijinsia mtandaoni nchini, wanawake wakiwa walengwa wakuu kwa asilimia 56.

“Natamani kuona wanawake wengi wanaingia kwenye siasa, kwani kila nafasi ilioshikwa na mwanamke imefanywa vizuri,ukimwangalia Jenista Mhagama (Waziri wa Afya), Doroth Gwajima (Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wenye Mahitaji Maalum) , Ukiangalia waliotutangulia kama Balozi Getruda Mongella, Balozi Dkt. Asha Rose Mingiro,aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah, Spika Mstaafu Anne Makinda, Mwanaharakati na siasa, Bibi Titi,wote wamefanya kazi nzuri,”anasisitiza Dkt.Angeline.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Buteja Kata ya Kahama, Elias Mabele, anasema kuwa Dkt.Angeline,amebadili mitazamo ya jamii,kuhusu uwezo wa wanawake katika uongozi.Na kuonesha matumaini kwamba wanawake wanaweza  kufanya mambo makubwa katika jamii.

“Kupitia Dkt.Angeline nimejifunza kwamba uwezo wa kufanya mambo makubwa,hautegemei jinsi,wanawake wameonesha ufanisi katika uongozi.Ni wakati wa kuunga mkono mchango wao katika jamii.”.

NAMNA ANAVYOGAWA SAA 24

“Katika kuweka sawa majukumu yangu,nikiwa kwenye kazi ni mtumishi wa umma,”Nikirudi nyumbani mimi ni mama, natimiza majukumu yangu kama mama kuhakikisha familia imekula na mambo mengine, hivyo napanga ratiba za kuhudumia familia na wananchi,”anaeleza Dkt,Angeline.

“Dkt.Angeline ni mlezi, akiwa nyumbani, chakula anachokula ndicho na wewe utakula.Mbunge pekee ambaye mlango wake ni wakila mtu,wakati mwingine anakaa nje ya nyumba yake na watoto wake na majirani,wakibadilishana mawazo,nakutaniana.Kijana mwenye ukaribu naye anakufanya kama mwanae, ukikosea atakuonya ukifanywa vizuri atakupongeza,”anaeleza Jumanne Ayubu, mwanachi jimboni Ilemela.

WAKATI MGUMU

“Sitasahau nilipopoteza familia yangu kwa kufiwa  na mume,baba na mama  kwa muda mfupi,nikiwa kiongozi hali ile iliniyumbisha.Kipindi nilichoona Dunia inakuwa chungu.Kwa maana mshauri mume hayupo, mshauri  baba,mama hayupo,baadaye nilikubaliana na hali ile, kwa sababu nasimamia imani,nikiamini sote ni wasafiri,”.

KITU GANI ANACHOKIPENDA

Anasema anapenda michezo tangu akiwa mtoto,alikuwa anacheza basketball, netball, lakini sasa anacheza mchezo wa kurusha mshale.

“Ukija bungeni,mimi ni moja wa magwiji wa kucheza mchezo wa kurusha mshale, natumia muda wa ziada  kwenye michezo kwani ninaipenda.Nashabikia timu ya Pamba Jiji “TP Lindanda”, Yanga SC,kwa timu za nje nashabikia  Arsenal,”.

Anaendelea kwa kusimulia kuwa anafurahia namna anavyowatumikia wananchi na wakaridhika na utendaji kazi wake,ambapo anapofanya vizuri wanampongeza na akiharibu wanamsema waziwazi.

“Mimi naipenda sana na inanipa furaha, sababu katika utumishi usitarajie kusifiwa kila kona,bali uweke kwenye mizani ujitafakari yanayosemwa ni kweli au siyo kweli,”.

Sehemu ya pili ya makala hii itaendelea tena kesho