November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano

Na Mwandishi Wetu,Morogoro

NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Mhandisi MaryPrisca Mahundi (Mb), amesema Serikali inayoongozwa na Dkt.Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuboresha mawasiliano hususani maeneo ya vijijini ili kuwaunganisha wananchi kwa lengo la kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kidijitali.

Mahundi ameyasema hayo Mkoani Morogoro alipofanya ziara ya kikazi, kukagua minara iliyojengwa katika Kata ya Mikese wilaya ya Morogoro na Kata ya Lubungo wilaya ya Mvomero, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 unatekelezwa na Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote (UCSAF) kwa usimamizi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP).

Awali, akitoa taarifa ya Utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Uendeshaji, Utafiti na Maendeleo  wa UCSAF, Mhandisi Albert Richard amesema, minara hiyo imejengwa kwa teknolojia ya 2G, 3G, na 4G na kuongeza kuwa katika kata ya Lubungo Serikali imetoa ruzuku ya shilingi milioni 360 ili kujenga minara miwili, mmoja umejengwa katika kijiji cha Lubungo na tayari umekamilika, na mnara mwingine unajengwa katika kijiji cha Vianzi, ambako utekelezaji unaendelea.

Baadhi ya wananchi waliofikiwa na huduma hiyo wameishukuru Serikali huku wakielezea changamoto walizokuwa wanakutana nazo awali ikiwa ni pamoja na kupanda kwenye miti ili kutafuta huduma ya mawasiliano

“Tunaishukuru sana Serikali kwa kutuletea mnara huu, hivi sasa tunapata mawasiliano vizuri na hatuna shida kama ilivyokuwa awali”

Mradi wa ujenzi wa minara 758 unatekelezwa kwa ruzuku ya shilingi bilioni 126, sehemu ya fedha hizo ni mkopo kutoka  Benki ya Dunia (WB) na sehemu nyingine ni fedha za ndani zinazotolewa na Serikali kupitia UCSAF. Hadi sasa jumla ya minara 302 imekamilika na inatoa huduma, ikiwa ni asilimia 40 ya utekelezaji wa mradi huo.