Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline, Korogwe
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga kimetaka Mradi wa Maji Same-Mwanga uwanufaishe wananchi wa Korogwe kama ilivyoahidiwa tangu mwanzo kwenye mipango ya kujengwa mradi huo.
Akizungumza kwenye mafunzo ya siku mbili yaliyowakutanisha viongozi wa CCM wilaya za Mkoa wa Tanga na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga, na kufanyika mjini Korogwe mwishoni mwa wiki,Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Ally Waziri alisema vijiji vitano vya Korogwe vinatakiwa kupata maji hayo.
“Kutokana na malengo ya kuanzishwa Mradi wa Maji wa Same-Mwanga ni kufikisha maji hata maeneo ya baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Korogwe. Sasa tunataka kujua maji hayo yatafika lini Korogwe ili wananchi hao wa vijijini waweze kunufaika na maji hayo,”amehoji Waziri.
Akijibu hoja hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Usambazaji Maji kutoka Wizara ya Maji Mhandisi Charles Mafie amesema mpango wa kupeleka maji kutoka Mradi wa Maji Same- Mwanga kwenda Wilaya ya Korogwe kwenye vijiji vya Buiko, Nanyogie, Manga- Mikocheni, Mkomazi na Manga- Mtindiro upo pale pale, kwani mradi huo unajengwa kwa awamu, na itakapofika kwenye kupeleka maji kwenye vijiji 29, ndipo na vijiji vitano vya Korogwe watapata maji hayo.
Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Korogwe Mhandisi Muharami Mohamed akiwasilisha taarifa yake, ameelezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kuwa wilaya hiyo ina vijiji 118, ambapo vijiji 71 vina huduma ya maji ya bomba, vijiji 24 vina maji ya visima, na vijiji 23 vina maji ya chemchemi na mto na vina vituo vya kuchotea maji. Lakini pia, wameweza kukamilisha miradi 14 yenye thamani ya sh. 5,201,008,770, ambayo itahudumia vijiji 34 vyenye watu 67,368.
“Huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama vijijini imeongezeka kutoka asilimia 63.6 hadi asilimia 71 ya sasa. RUWASA imeendelea kuwa na utekelezaji wa miradi 12 ya maji yenye thamani ya sh. 14,055,170,412, ambayo itahudumia vijiji 25 vyenye wananchi 57,972, ambapo miradi hii ikikamilika itaongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji hadi kufikia asilimia 89.9 ikiwa ni ziada ya asilimia 4.9 ya lengo la Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020- 2025.
“Pia RUWASA Korogwe, imeendelea kusanifu jumla ya miradi mipya 12 itakayohudumia wananchi wapatao 80,531 katika vijiji 36. Na imefanikiwa kufanya utafiti wa vyanzo vya maji chini ya ardhi na kuchimba visima virefu sita vya maji ambavyo katika bajeti ya mwaka 2024/2025 vitajengewa miundombinu. Pia tumeweza kuunganisha (Crustering) Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSO’s) kutoka 11 hadi vinane (8),”amesema Mhandisi Mohamed.
Mhandisi Mohamed amesema pia wamefanikiwa kuwawezesha watumishi wa CBWSO’s kupata mafunzo mbalimbali juu ya uendeshsji na utoaji huduma ya maji vijijini ikiwa ni pamoja na mafunzo ya Mfumo wa Kielektroniki wa ukusanyaji wa fedha za umma serikalini (GePG) na kuanza kukusanya mapato yao kwa kutumia mfumo huo.
Mhandisi Mohamed amesema RUWASA Korogwe imefanikiwa kuwezesha CBWSO’s kupata vitendea kazi ambavyo ni pikipiki tatu, kompyuta mpakato (laptop) 11, na simu za mkononi 11.
“Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 RUWASA Korogwe inatarajia kupokea fedha za maendeleo sh. 6,325,934,901 kutoka kwenye Mfuko wa Taifa wa Maji (NWF) na PforR. Kiasi hiki cha fedha ni ongezeko la sh. 2,853,520,016 ya bajeti iliyopita ya mwaka 2023/2024,”amesema Mohamed.
More Stories
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya