October 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lishe bora suluhisho la udumavu ,utapiamlo

Judith Ferdinand,Timesmajira Online

Kwa mujibu wa utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa mwaka 2022, theluthi moja ya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 wamedumaa. Hali hii inatishia maendeleo ya watoto na afya ya jamii kwa ujumla.

Huku tathmini ya tafiti ya The Demographic and Health Surveys (DHS) ya mwaka 2022, imeonesha kuwa hali ya lishe nchini inaendelea kuimarika, kutokana na kupungua kwa viwango vya utapiamlo kwa baadhi ya viashiria.

Kiwango cha udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambacho ndiyo kiashiria kikuu cha utapiamlo kimepungua kutoka asilimia 34 mwaka 2016 hadi asilimia 30 mwaka 2022.

Ambapo Mikoa mitano ya Tanzania Bara, imefanikiwa kupunguza viwango vya udumavu kwa watoto kwa zaidi ya asilimia 10,katika kipindi cha mwaka 2016 na 2022. Mikoa hiyo ni Mtwara (asilimia 15.7), Tanga (14.9), Lindi (13.7), Mwanza (11.1) na Kigoma (10.9).

Hali ya Udumavu Mkoa wa Mwanza
Akizungumza na Timesmajira Online Oktoba 3,2024,Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Jesca Lebba,wakati wa ufungwaji wa mkutano wa 10,wa wadau wa lishe nchini,uliofanyika kwa siku mbili wilayani Ilemela mkoani Mwanza.Wenye kauli mbiu”Kuchangiza mchango wa wadau wa kisekta,ili kudumisha matokeo bora ya hali ya lishe nchini Tanzania”.

Anasema kwamba lishe ni muhimu kwa maendeleo ya binadamu. Bila ya afya njema, mtu hawezi kufanya chochote. Kwa sasa, hali ya udumavu katika Mkoa wa Mwanza ni asilimia 28, ikiwa imepungua kutoka asilimia 39 mwaka 2018. Hali hii inaashiria mwelekeo mzuri, huku lengo la taifa likiwa ni asilimia 30.

Dkt.Lebba,anasema Halmashauri mkoani humo,zinazokabiliwa na changamoto zaidi ni Ukerewe, Buchosa, na Kwimba, lakini jitihada zinafanyika kuboresha hali hiyo. Kwa upande wa uzito pungufu, Mkoa umefanikiwa kuwa na asilimia 2.8, chini ya lengo la taifa la asilimia 5, huku ukondefu ukiwa asilimia 1.8, ukilinganishwa na lengo la kitaifa la asilimia 3.

Mikakati ya Kuboresha Lishe
Dkt. Lebba,anaeleza kuwa kuna mikakati mbalimbali inayoendelea, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa jamii katika mikusanyiko mbalimbali na vituo vya afya, kwa ushirikiano na serikali na wadau. Halmashauri zimeweza kutoa asilimia 92 ya fedha za lishe, na waandishi wa habari wanachangia kwa kutoa taarifa muhimu kuhusu lishe.

“Lishe bora inahitaji vyakula kutoka makundi sita, lakini wavuvi wengi hawatumii samaki wanazovua, badala yake wanauza. Pia, kuna uhaba wa watu kutumia matunda na mboga za majani. Hivyo, jamii inahitajika kuelewa umuhimu wa mlo kamili ili kuweza kufikia maendeleo endelevu,”anasema Dkt.Lebba.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.Jesca Lebba

Mchango wa Shirika la World Vision Tanzania
Meneja Mradi wa Afya na Lishe kutoka World Vision Tanzania, Shukrani Dickson anasema,bado kuna changamoto kuhusu udumavu na utapiamlo nchini.

“Shirika hili linatoa mafunzo kwa wanawake kuhusu jinsi ya kuandaa milo bora kwa watoto, na kuhakikisha watoto wanapata chanjo ya vitamin ‘A’.Tunatoa mbegu za viazi lishe na maharage, ili kuongeza virutubisho katika lishe ya watoto,”.

Ushiriki wa Jamii
Shukrani anasema,lcha ya juhudi hizo, elimu kuhusu masuala ya lishe bado ni muhimu. Wanawake mara nyingi wana majukumu makubwa, huku wanaume wakibaki nyuma. World Vision inasisitiza ushirikishwaji wa wanaume katika masuala ya afya kupitia kauli mbiu ya “man care”. Hii ni muhimu hasa katika kuhamasisha familia kuhusu lishe bora kwa wajawazito na watoto.

Hivyo anasema kuwa mchango wa wanaume katika masuala ya lishe unahitajika ili kuboresha hali ya udumavu. Hii ni kutokana na tamaduni ambazo zinawafanya wanaume kuwa na sauti kubwa katika maamuzi ya familia kuhusu lishe.

“Ni muhimu kwa jamii kuelewa kuwa malezi bora yanahitaji ushirikiano wa wote, ili kuhakikisha watoto wanapata lishe bora na mahitaji mengine muhimu,”anasisitiza Shukrani.

Msisitizo wa serikali juu ya lishe

Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa,anasema lishe ni moja ya vipaumbele muhimu kwa Serikali, kuwezesha kutekeleza mipango ya kuwaletea wananchi maendeleo na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii zikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji, biashara

Hivyo anasisitiza na kuelekeza,mambo kadhaa yatakayochangia kuboresha hali ya lishe nchini na kuondoa changamoto,zinazoikabili sekta hiyo ikiwemo,wadau wa lishe kutumia matokeo ya ripoti ya muda wa kati,kujitathimino na kuchukua hatua stahiki za kuboresha utekelezaji wa afya za lishe kwa kipindi kilichobaki cha mpango wa taifa wa lishe.

Huku akizitaka,Wizara,wakala,taasisi na mashirika ya umma,watumie kikamilifu mwongozo wa mpango jumuishi wa taifa wa lishe na bajeti, kuhakikisha masuala ya lishe yanajumuishwa katika mipango na kutengewa fedha ili yatekelezwe kikamilifu kila mwaka.

“Mikoa na Halmashauri,tumieni vizuri mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimu ya msingi, na kuhakikisha matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa yanajumuishwa na kutengewa fedha katika mipango na bajeti za kila mwaka,”anasisitiza Majaliwa.

Aidha ameitaka,taasisi ya Chakula na Lishe na wadau wengine, kuhakikisha wanabuni mikakati zaidi ya kufikisha elimu sahihi ya lishe kwa umma.Ili kusaidia jamii kuelewa changamoto iliopo na kuchukua hatua sahihi kwa wakati.

“Jitihada za makusudi ziendelee kuchukuliwa ili kuhakikisha wadau wote, hususan sekta binafsi, waweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango wa afua za lishe nchini,”.

Meneja Mradi wa Afya na Lishe kutoka World Vision Tanzania, Shukrani Dickson

Kwa upande wake Katibu Mkuu,Ofisi ya Waziri Mkuu(Sera,Bunge na Uratibu),Dkt.Jim Yonazi,amesema mkutano wa wadau na wataalamu wa lishe uliofanyika Oktoba 2,2024, kupitia majadiliano yalipatikana maazimio matano, ikiwemo masuala ya huduma za lishe yajumuishwe katika dira ya taifa ya mwaka 2050.

Dkt.Jim,anasema pia kuimarisha huduma za lishe kwenye ngazi ya jamii ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hii.

Pia,kuimarisha uratibu na utekelezaji wa vipaumbele vya Mpango wa Pili Jumuishi wa Kitaifa wa Lishe, kwa kuhakikisha kila Wizara za kisekta na wadau wa maendeleo wanawajibika kutekeleza afua za lishe kulingana na Mpango.

“Kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika kutekeleza afua za lishe; na kuimarisha upatikanaji na matumizi ya taarifa za lishe katika ngazi zote,”.

Kwa ujumla ili kupunguza udumavu na kuboresha lishe katika Mkoa wa Mwanza na maeneo mengine nchini,ni muhimu kuendelea na juhudi za elimu, ushirikishwaji wa jamii, na mikakati ya kuongeza upatikanaji wa vyakula vyenye virutubisho. Kila mwanajamii anawajibu wa kushiriki katika kuhakikisha watoto wanapata lishe bora na afya njema.