Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha
UBALOZI wa China kwa kushirikiana na Kampuni ya Oryx Gas Tanzania wametoa mitungi 800 ya gesi yakiwa na majiko yake kwa walimu, madereva na wahudumu wa Serikali
pamoja na Waandishi wa habari wa Mkoa wa Arusha lengo ni kutekeleza sera ya Serikali ya Tanzania pamoja na China katika kutunza mazingira.
Hafla hiyo imefanyika leo Oktoba 7,2024 jijini Arusha na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian ,Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Oryx Gas Tanzania Benoit Arama ,Mbunge wa Arusha Mjini pamoja na viongozi wa dini
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kugawa mitungi kwa makundi hayo Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian amesema Serikali ya China inaunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira na uoto wa asili.
Amesema Tanzania ni nchi rafiki wa mazingira na inazingatia uhifadhi wa Mlima Kilimanjaro na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kwamba kwa muda wa miaka mitatu amefanya kazi hapa nchini na ameshuhudia juhudi za ajabu ambazo zimefanywa na Tanzania katika nyanja ya utunzaji wa mazingira.
Amesema licha ya mitungi hiyo ya gesi sio tu itaboresha maisha ya walimu bali pia itapanda mbegu za ulinzi wa mazingira katika mioyo ya wanafunzi na kufafanua Rais Xi Jinping wa China mara nyingi husema maji ya bahari na milima mirefu ni mali ya thamani sana.
“Kama nchi zinazoendelea zinazowajibika, China na Tanzania zote zimekataa kukubali na kukataa kufuata njia ya zamani ya uchafuzi wa mazingira.Badala yake, tumechagua njia mpya ya kipaumbele cha kiikolojia na maendeleo ya kijani…
“Huku tukiendeleza kwa nguvu mazingira, kwa njia ya uchumi na kuboresha maisha ya watu, pia tumechukua jukumu muhimu la kulinda mazingira. Mei mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alipendekeza mkakati wa nishati safi ya kupikia ambao unadhihirisha kikamilifu falsafa ya Serikali ya Tanzania ya kujali wananchi wake kwanza na kuishi kwa usawa kati ya mwanadamu na maliasili.
“China na Tanzania ni kaka na dada wazuri sana, na pia ni washirika wazuri sana. Daima tunasaidiana. Mwezi uliopita, Jukwaa la Ushirikiano wa China na Afrika lilifanya mkutano huko mjini Beijing. Wakuu wa nchi, serikali na wajumbe kutoka nchi 53 akiwemo Dkt. Samia Suluhu Hassan walikusanyika Beijing kushiriki, nami nilifuatana na ujumbe wa Rais katika tukio hilo muhimu.”
Ameongeza Rais Xi Jinping alitoa hotuba muhimu, na Rais Samia Suluhu Hassan, naye aliiwakilisha Afrika Mashariki, alitoa hotuba kwenye hafla ya ufunguzi.Wakati huo huo, alitangaza hatua za ushirikiano kati ya China na Afrika, katika Ushirikiano wa Maendeleo ya Kijani, zilipendekeza kuwa China inapenda kutekeleza miradi 30 ya nishati safi katika bara la Afrika ili kuzisaidia nchi za Afrika kufikia maendeleo ya kijani kibichi.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Ltd Benoit Araman kuanzia Julai 2021, upatikanaji wa suluhisho la kupika imekuwa mada ya umuhimu mkubwa, chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan na leo wako pamoja kuunga mkono utekelezaji wa Programu ya Kupika kwa Nishati Safi nchini Tanzania.
Amesema programu ya nishati safi ya kupikia itachukua miaka 10 kuwezesha upatikanaji wa Nishati Safi kwa ajili ya kupikia kwa angalau asilimia 80 ya Watanzania ifikapo mwaka 2034. Hivyo kuna haja ya kuungana kufanikisha juhudi hizo.
“Ukizungumza kuhusu nishati safi ya kupikia kwa wanafunzi wenu na katika mikutano na wazazi itachangia kwa kiasi kikubwa kueneza kwa nishati safi ya kupikia nchini Tanzania. Ninyi kuwa watumiaji wa Oryx Gas itasaidia idadi ya watu kuona manufaa ya kupika kwa kutumia LPG na kuipitisha zaidi.
“Naushukuru Ubalozi wa China nchini Tanzania, kwa ushirikiano wao, ambao umeruhusu makabidhiano ya mitungi ya gesi na majiko yake 800. Kwa kushirikiana na Gambo Foundation “Alama Africa” na Oryx Gas Tanzania, nchi ya China inaonyesha nia na dhamira yake ya kuunga mkono utekelezaji wa programu ya Kupika kwa Nishati Safi nchini Tanzania.
Ametumia nafasi hiyo kueleza kwa kina faida za kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo ya Uboreshaji wa Afya kwani nchini Tanzania, wananchi 33,000 wanakufa kila mwaka kutokana na kuvuta pumzi ya moshi na chembechembe zinazotokana na mkaa na kuni. Kupika na Oryx LPG kutaondoa changamoto ya Vifo hivyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema Oryx Gas imekuwa Kampuni ya kwanza kwa Arusha kuonesha wamedhamiria kuunga mkono kampeni ya Rais Samia na wamekuwa mstari wa mbele katika kampeni hiyo.
Amesema hata katika utoaji wa mitungi ya gesi 5000 kwa walimu , Oryx Gas walikubali kutoa mitungi na majiko na leo wameendelea kutoa mitungi ya gesi na majiko yake 800 kwa kushirikiana na Ubalozi wa China pamoja na Alama Africa.
More Stories
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja