Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga kimesema wilaya hiyo haitaweza kufikia asilimia 85 ya upatikanaji maji vijijini ifikapo Desemba 31, 2025 iwapo Serikali itashindwa kupeleka fedha sh. bilioni 38,650,373,553 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji.
Kwa sasa wilaya hiyo ndiyo ya mwisho kwenye Mkoa wa Tanga kwa wananchi wake kupata maji. Kutokana na Sensa ya mwaka 2022, Wilaya ya Kilindi inakadiriwa kuwa na jumla ya wakazi 398,391. Idadi ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama vijijini ni 140,294 sawa na asilimia 39.1 ya wakazi waishio vijijini.
Hayo yalisemwa Oktoba 5, 2024 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilindi Mohamed Kumbi wakati anachangia taarifa ya upatikanaji wa maji wa wilaya hiyo kwenye mafunzo ya siku mbili kati ya viongozi wa CCM ngazi ya wilaya za Mkoa wa Tanga, na Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Tanga, yaliyofanyika mjini Korogwe.
“Hawa wenzetu wataalamu ni watumishi, sisi ni viongozi. Sisi kama viongozi kuna sehemu ambazo hatuogopi kufika, na tuna uwezo wa kuyaongelea yanayowakwaza wao. Kwa nini nasema hivyo, katika miradi mingi ya maji Kilindi sisi kama Chama Cha Mapinduzi kupitia Kamati ya Siasa tumeipitia yote, lakini kila tunapokwenda tatizo ni malipo. Kinachotakiwa hapa kinajulikana, ni fedha. Na hapa nataka niende kwa mifano halisi ili mnielewe ni jinsi gani miradi inakwama kule Kilindi.
“Ujenzi wa mradi wa maji Diburuma/Songe ni wa thamani ya sh. 22,956,445,680. Mkandarasi anahitaji angalau sh. bilioni mbili aweze kufanya kazi, lakini hajapata. Tumekwenda wote pale, na mradi tumeungalia kwa macho, wananchi wanataka maji, lakini mradi haujaanza, wananchi hawajapata maji sababu mkandarasi hajapewa fedha. Mradi wa maji Kwamaligwa/Gitu wa sh. 6,988,881,532. Mkandarasi anahitaji apate sh. milioni 687 ili kazi ianze, lakini fedha hajapata. Tunapita tukiwatangazia wananchi mtapata maji, lakini mkandarasi hajaanza kazi, huku mabomba yamejaa pale” alisema Kumbi.
Kumbi alisema miradi mingine ambayo inasubiri fedha ni Ujenzi wa Mradi wa Maji Mabalanga wa sh. 465,511,054, ,Uchimbaji wa visima 23 katika vijiji 23 sh. 1,544,166,600, Ujenzi wa Bwawa la Maji Saunyi (Lombaut), sh. 3,159,681,791, Ukarabati/Upanuzi wa Mradi wa Maji Mgera/Kisangasa sh. 306,400,000, ukarabati wa Mradi wa Maji Chamtui sh. 62,147,812.
“Mradi wa Bwawa la Saunyi ni wa sh. bilioni 3.1. Mkandarasi anahitaji apate sh. milioni 275 ili mradi uendelee, hajapewa hata shilingi. Tunakwenda tunapiga kelele maji yanatakiwa lakini bado fedha hakuna. Tuna mradi wa maji visima 23. Sisi Kilindi tunaomba mtusaidie, zile mashine (mitambo ya kuchimba visima) ziletwe Kilindi, tunahitaji visima vichimbwe, lakini havichimbwi. Ili kuinusuru Kilindi, hali ni mbaya kama mlivyoona. Mradi wa Maji Kilindi Asilia, pale kunahitajika bomba za kilomita tano ili kukamilisha mradi, lakini mkandarasi hajamaliziwa fedha zake, zile bomba haziendi, maeneo tuliyoahidi maji hayaendi” alisema Kumbi.
Kumbi alisema ili kuwapunguzia adha ya maji wananchi wa Kilindi, ameiomba Serikali, Mradi wa Maji wa Miji 28 usiishie Mji wa Handeni, bali watoe nafasi kwa kata tano za Wilaya ya Kilindi ili kupata maji hayo.
“Wataalamu wameshasema maji hayana mpaka. Kuna mradi mkubwa wa maji wa HTM (Miji 28) unakuja mpaka Handeni. Ndugu zangu ukifika Handeni tusaidiwe uingie kilomita 50 za Wilaya ya Kilindi hadi pale Kwediboma, sababu Mradi wa Diburuma kule unachukua kata sita, na huu wa HTM ukichukua kata tano za Jaila, Mkindi, Mabalanga, Msanja hadi Kwediboma, itawasaidia sana wananchi wa Kilindi” alisema Kumb.
Akitoa taarifa kwenye mafunzo hayo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kilindi Mhandisi Alex Odena alisema huduma ya maji kwa Wilaya hiyo inatolewa kutoka kwenye vyanzo vya maji vya chemchemi za asili zilizoboreshwa, mabwawa madogo na visima virefu na vifupi.Huduma hiyo inasimamiwa na RUWASA kwa upande wa vijijini na Mamlaka ya Maji Songe (SOWASA) kwa upande wa mjini. Kuna jumla ya Skimu 42 za maji zinazohudumia vijiji 63 kati ya vijiji 102 vilivyopo katika wilaya hiyo
“RUWASA Wilaya ya Kilindi tumefanikiwa kuunda na kuunganisha vyombo vinane (8) vya utoaji huduma ya Maji ngazi ya Jamii (CBWSOs).Wilaya Kilindi inakadiriwa kuwa na jumla ya wakazi 398,391 (Sensa 2022). Idadi ya wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama vijijini ni 140,294 sawa na 39.1 ya wakazi waishio vijijini. Kuna vyanzo vya maji 42 ambavyo vinahudumia Skimu za maji zilizopo wilayani, matenki ya kuhifadhia maji 46 yenye ujazo kati ya lita 1,000 na 450,000. Vituo vya kuchotea Maji (DPs) 694 zenye sehemu za kuchotea maji 1,011 na mtandao wa mabomba unaokadiriwa kuwa na urefu wa kilomita 238.352
“Ili kuboresha huduma ya maji vijijini katika kipindi cha mwaka 2024/2025 Serikali imepanga kutumia jumla ya Sh.4,107,134,678 kwa ajili ya kuendelea kutekeleza ujenzi wa miradi ya maji . Miradi hii yote itagharimu sh. 38,650,373,553 hadi kukamilika kwake. Miradi hii itakapokamilika itaongeza huduma ya maji kwa asilimia 27.38
Hadi kufikia Septemba, 2024, Wilaya ya Kilindi imepokea jumla ya sh. milioni 200 sawa na asilimia 4.9 ya bajeti” alisema Mhandisi Odena.
Mhandisi Odena amesema katika utafutaji wa vyanzo, Wilaya ya Kilindi imepanga kuchimba visima 23 ambapo tayari mkandarasi anaendelea na uchimbaji wa visima ambapo mpaka sasa amechimba visima sita, ujenzi wa Bwawa la Saunyi (Lombouti) na upimaji wa vyanzo vya maji ya vijito vitano ili kuweza kujua wingi na ubora wa maji. Kilindi kwa kushirikiana na timu ya usanifu ya mkoa pamoja na Makao Makuu wamekamilisha usanifu miradi mitano ambayo ni usanifu wa miradi ya maji Bwawa la Mkonde, Bwawa la Maji Msente, Mradi wa Maji Mkindi, Mradi wa Maji Kwaluguru Negero, Mradi wa Maji Kikunde/Ludewa, na wanaendelea na usanifu wa Mradi wa Maji Kwadundwa/Kilwa na Lumotio /Pagwi, Kwediboma/Makingo, Kigwama/Tilwe/Masagusa.
Mhandisi Odena alisema RUWASA Kilindi imeandaa mkakati wa kuhakikisha ifikapo Desemba, 2025 hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi vijijini ifikie asilimia 85, ambapo Jumla ya miradi tisa inaendelea kutekelezwa na miradi mipya sita ambayo usanifu wake umekamilika. Miradi inayoendelea ikikamilika kutawezesha jumla ya wananchi wapatao 109,074 kupata huduma ya maji sawa na asilimia 27.38 hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 39.1 ya sasa hadi asilimia 66.48.
“Miradi mipya ambayo usanifu wake umekamilika utekelezaji wake ukikamilika utawezesha wananchi wapatao 41,023 kupata huduma ya maji sawa na asilimia 11.43 hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 66.48 ya sasa hadi asilimia 77.91. Vile vile uchimbaji wa visima vitano na ujenzi wa point source katika vijiji vya Mswaki, Makingo, Kitingi, Lusimbi na Tunguli utawezesha wananchi 5,000 kupata huduma ya maji sawa na asilimia 1.4, hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 77.91 ya sasa hadi asilimia 79.31.
“Pia uchimbaji wa visima 23 na ujenzi wa point source katika vijiji vya Sangeni, Msente,Mangidi, Mtonga, Mkindi,Mswaki, Makingo, Kisangasa, Mzinga, Kimembe, Kitingi, Makelele,Lumotio Kwamba, Sambu, Mheza, Ngeze, Mapanga, Vunila, Kwaisapo, Lukole, Vyadigwa na Kitingi kutawezesha wananchi 23,000 kupata huduma ya maji sawa na asilimia 6.4 hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 77.91 ya sasa hadi asilimia 85.7” alisema Mhandisi Odena.
Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga Selemani Sankwa ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, yeye na wajumbe walikubaliana kwa pamoja kuwa, pamoja na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha nyingi kwa miradi ya maji kwenye Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Kilindi inahitaji kuwekewa msukumo wa kipekee ili kupata fedha za kuwezesha kukamilisha miradi ya maji.
More Stories
Amos Lengael Nnko afariki kwa ajali ya gari
Gridi za Tanzania, Kenya kuimarisha upatikanaji wa umeme
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote