December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Muhongo awakaribisha wadau kuchangia ujenzi maabara masomo ya Sayansi

Fresha Kinasa,TimesMajiraOnline,Musoma.

WADAU mbalimbali wa maendeleo hasa wazaliwa wa Halmashauri ya Musoma Vijijini Mkoani Mara,wameombwa wajitokeze kuchangia kwa hiari ujenzi wa maabara za masomo ya Sayansi kwenye Sekondari za kata.

Idadi ya Shule za Sekondari za kata ambazo ni za Serikali  katika Halmashauri hiyo ni 26, Sekondari
za Binafsi 2, na Sekondari mpya zinazojengwa ni  12. Ambapo maabara zinazohitajika kwenye Sekondari za Kata  za masomo ya Sayansi  Phisics, Biology na Chemistry  ni 78, huku zilizopo ni 41.

Hayo yameelezwa na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Prof.Sospter Muhongo kupitia taarifa yake aliyoitoa Octoba 6, 2024 huku akisema kuwa ili kumaliza tatizo hilo ni  jukumu la wadau wote wa Maendeleo kuungana pamoja kuchangia  na kushirikiana na Serikali kufanikisha ujenzi wa maabara hizo.

Kupitia taarifa yake Prof. Muhongo amesema kuwa, ameendelea kuweka nguvu katika kuhakikisha ujenzi wa maabara unaendelea kwa   kuendesha  harambee  katika shule mbalimbali  za ujenzi huo akishirikiana na Wananchi,  viongozi wao na Serikali ndani ya Jimbo hilo lenye kata 21, zenye Vijiji 68 na vitongoji 374.
 
Lengo ni kuhakikisha kwamba,wanafunzi wayasome masomo hayo kwa vitendo na uhalisia  ambayo yanafaida katika Jamii yao, Taifa pia na Kwa  maisha yao kwa siku za usoni. 

Prof.Muhongo amesema kuwa, shule ambazo hazina maabara ni Bukwaya Sekondari, Busambara Sekondari, Mtiro Sekondari, Murangi Sekondari, Nyanja Sekondari, Seka Sekondari na Tegeruka Sekondari huku Sekondari zenye maabara moja ni Bukima Sekondari, Dan Mapigano Sekondari, Kasoma Sekondari na  Mabuimerafuru  Sekondari.

“Sekondari 7, zina maabara tatu, Sekondari 8, zina maabara mbili, Sekondari 4, zina maabara moja na Sekondari 7, hazina maabara.  Ni jukumu la wadau wote wakiwemo Waziliwa wa Musoma Vijijini kujitokeza kuchangia maabara za masomo ya Sayansi kwenye Sekondari zetu ili Watoto wetu wasome kwa vitendo. “amesema Prof. Muhongo.

Neema Mafuru ni Mkazi wa Kata ya Nyakatende Katika Halmashauri hiyo, akizungumza na Times Majira,  amewahimiza pia  Wadau mbalimbali wa elimu  kuunga mkono juhudi za Mbunge wao Prof. Muhongo kuendelea kushirikiana katika ujenzi wa maabara kwa faida ya watoto wao ambao ndio wanufaika.

Naye Hamidu Masegesa Mkazi wa Kata ya Nyegina amesema, dunia ya sasa inahitaji Wasomi na Wabobezi wa fani mbalimbali   za  Sayansi. Hivyo wazazi na walezi wanalojukumu la kuhamasisha Watoto wao  wapenda kusoma masomo hayo na njia pekee ya kufanikisha jambo hilo  ni kuwekeza nguvu zao na pesa zao wakishirikiana na serikali  kujenga  maabara katika shule ambazo bado hazijajenga.