October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

282,wafanikiwa kujiunga na mfumo rasmi wa elimu

Na Israel Mwaisaka, Timesmajira Online,Rukwa

Wanafunzi 282 kati ya 302 waliofanya mitihani ya kitaifa ya upimaji wa darasa la nne kwa mwaka 2023, wamefanikiwa kujiunga na mfumo rasmi wa elimumkoani Rukwa.

Huku wanafunzi 1,785 kati yao wavulana 899 na wasichana 886, wamejiunga na madarasa ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Waliokosa (MEMKWA) kutoka Halmashauri nne za Mkoa huo.

Hivyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere,akiwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo,Dkt. Lazaro Komba,amepongeza mafanikio waliopata wanafunzi hao,ya kujiunga na mfumo rasmi wa elimu, wakati wa maadhimisho ya kilele cha siku ya Elimu ya Watu Wazima, yaliyofanyika wilayani Kalambo.

Dkt. Komba,amesisitiza umuhimu wa jamii kujiendeleza kielimu kwa kushiriki katika programu za elimu ya watu wazima.

Pia ameeleza kuwa, shule zote mkoani Rukwa,zina vyumba maalum kwa ajili ya watu wazima kujiendeleza kielimu.Ambapo matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022,yanaonesha kuwa asilimia 25.9 ya watu wazima hawajui kusoma, kuandika, na kuhesabu (KKK),changamoto hiyo inahitaji hatua za dharura.

Sanjari na hayo,amewataka wazazi na walezi, kutimiza majukumu yao ya malezi kwa kuhakikisha watoto wao wanahudhuria masomo katika mfumo rasmi wa elimu, ili kuepuka changamoto zinazoweza kukwamisha maendeleo yao.

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Rukwa, Matinda Mwinuka, amesema ukosefu wa vitendea kazi maalum,kwa ajili ya elimu ya watu wazima na muamko mdogo wa vijana kujiunga na vyuo vya elimu ya watu wazima ni changamoto kwa walimu wakati wa kutoa elimu hiyo.

Hata hivyo baadhi ya wazazi wenye watoto wanaosoma katika shule hizo, wameomba Serikali kuongeza walimu wenye weledi na maadili ili kusaidia kuboresha viwango vya ufaulu wa wanafunzi.

Vilevile, wadau wa elimu mkoani humo, akiwemo Edwin Moses, wamesisitiza umuhimu wa Serikali kuwekeza zaidi katika elimu ya watu wazima kwa kuboresha miundombinu na kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kufanikisha malengo yao.