Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
KUTOKANA na ubovu wa miundombinu ya barabara za mitaa Jijini Mbeya serikali imeombwa kukamilisha ujenzi wa barabara za mitaa ili kuweza kurahisisha adha wanayoipata akina mama wajawazito katika kufikia huduma za afya .
Hayo yamesemwa October 2,mwaka huu na wananchi wa kata ya Isanga wakati Spika wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini na Rais umoja wa mabunge duniani (IPU)Dkt.Tulia Ackson alipokuwa akikabidhi mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa Zahanati ya kata ya Isanga .
Mmoja wa wananchi wa Kata ya Isanga Jijini Mbeya,Zainabu Mwaseba amesema kuwa kukamilika kwa Zahanati hiyo kutakuwa msaada hususani kwa akina mama wajawazito,wazee pamoja na watu wenye ulemavu ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Akielezea zaidi Mwaseba amesema kwamba uwepo wa Zahanati hiyo umeleta nafuu kwa kwa wananchi kwani awali ilikuwa changamoto hususani akina mama wajawazito ambapo kipindi cha mvua madaraja yalikuwa yakijaa maji hivyo kupata ya kuvuka wakati wakielekea hospitali nyingine kutafuta huduma .
“Suala hili lilichangia akina mama wajawazito kujifungulia njiani au kupoteza maisha kutokana na changamoto ya ubovu wa barabara za mitaa, tunamshukuru Mbunge wetu Dkt.Tulia kwa msaada huu wa mifuko 100 ya saruji tunaamini inaenda kukamilisha jengo letu la kata “amesema Mwaseba.
Kwa upande wake Mbunge wa Mbeya mjini na Spika wa Bunge na Rais umoja wa mabunge duniani (IPU)Dkt.Tulia Ackson amesema Mbeya mjini kuna changamoto ya miundombinu ya barabara ya kilometa 400, ambazo ni vumbi na kuwa katika kilometa hizo tayari zimepungua kutokana na juhudi za serikali na kueleza kuwa barabara ya Mbwiga yenye mita 500 iliyopo kata ya Isanga na juhudi tayari zimewekwa lami.
“Barabara nyingi zinafanyiwa kazi na tungetamani kasi iwe kubwa lakini tunafahamu kwamba changamoto zipo nyingi kwasasa ila tunaenda kwa hatua na hapa tumesogeza huduma ya Zahanati lakini bado barabara ya kufikia ni changamoto ya mashimo hivyo ndo maana mama mjamzito anapokuwa kwenye ile hali anapata shida kutokana na mtikisiko wa mashimo “amesema Dkt.Tulia.
Dkt.Tulia amesema zipo barabara ambazo zinawekwa lami na zingine kuwekewa changarawe na zingine kukwanguliwa ili ziweze kupitika kihalahisi na kisha kuja kuwekewa lami.
Akielezea zaidi amesema Zahanati ya Isanga itakuwa maalum kwa kuongezewa jengo la mama na mtoto ili kupunguza mwendo mrefu .
Meya wa Jiji la Mbeya na Diwani wa Kata Isanga Dourmohamed Issa amesema kukamilika kwa Zahanati hiyo kutapunguza adha kwa wananchi wa kata hiyo kutembea umbali mrefu huku alisema changamoto za barabara za mitaa tayari zimeanza kutatuliwa kwa kuanza na Miata 500 za barabara ya mtaa wa Mbwiga ambako tayari kumewekwa lami.
More Stories
TAKUKURU,rafiki yanufaisha wananchi Mwanza
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa