October 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia apongezwa kwa kuboresha huduma kwa wazee

Na Allan Kitwe, Timesmajiraonline,Tabora

WAZEE wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma zao ikiwemo kurahisisha upatikanaji huduma za afya katika Vituo vya Kutolea huduma hizo.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Taifa Lameck Sendo alipokuwa akitoa salamu katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kitaifa jana katika uwanja wa Chipukizi Mjini Tabora.

Alisema kuwa upatikanaji huduma za afya ilikuwa changamoto kubwa kwa wazee katika Mikoa mingi hapa nchini lakini serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia imeendelea kufanya kila linalowezekana ili kuhakikisha wazee wanapata matibabu.

Aidha aliongeza kuwa uongozi wa Rais Samia umeendelea kuelekeza halmashauri zote kutambua wazee waliopo katika maeneo yao na kuhakikisha wanawapatia kadi za Bima ya Afya iliyoboreshwa kwa ajili ya kupata matibabu.

‘Tunampongeza Rais kwa kujali wazee na kuendelea kuboresha huduma zao, sasa hivi wazee hawafi mapema kwa sababu ya kuboreshewa huduma za afya, naomba Mungu amjalie kufanikisha mipango yote aliyonayo kwa ajili ya wazee’, alisema.

‘Wazee ni hazina ya Taifa, ni kinu cha hekima, vijana tumieni fursa hii kuchota hekima kwa wazee, wazee wanajua mengi na wanaona mbali, hawako tayari kuona vijana wakijiingiza katika vitendo visivyofaa ikiwemo ndoa za jinsia 1’, alisema.

Naye Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Wazee, Masanja Matimbwa alibainisha kuwa kupitia maadhimisho hayo wazee wamelaani vitendo vya utekwaji, ndoa za jinsia moja na kuitaka serikali kutoruhusu ndoa za namna hiyo hapa nchini.

Aidha wameomba itoe tamko la kuanzishwa klabu za wazee kwa ajili ya kujenga afya zao, idara zote za ustawi wa jamii ziwe na kitengo cha wazee na zitenge bajeti, Taasisi ya Kusaidia Wazee (Helpage International) ifike katika Mikoa yote.

Mzee Matimbwa aliongeza kuwa pia wameazimia masuala ya wazee kuingizwa katika dira ya taifa na mmomonyoko wa maadili iwe agenda ya kudumu katika vikao vyote vya kisekta.

Mkuu wa Mkoa huo Paul Chacha akifunga maadhimisho hayo kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Doroth Gwajima, alisema kuwa serikali inawathamini wazee na itaendelea kufanya kila linalowezekana ili kuboresha huduma zao.

Aliwataka kupitia mabaraza yao kuendelea kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili, kupinga ndoa za jinsia moja na vitendo vyovyote vya uhalifu miongoni mwa jamii.