November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yashauriwa kudhibiti mihemko ya kisiasa

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

VIONGOZI wa madhehebu mbalimbali ya dini Mkoani Tabora wameiomba serikali kukemea kauli zozote zenye viashiria vya uvunjifu wa amani ikiwemo vitendo vya rushwa kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Wametoa ushauri huo jana kwenye semina ya siku 1 iliyoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani hapa ambayo ilihusisha pia waandishi wa habari.

Askofu wa Kanisa la Free Pentecoste Church of Tanzania (FPCT) Dkt Peter Shan amesema kuwa Tanzania ni miongoni nchi ambazo zimeendelea kudumisha amani na utulivu kwa wananchi wake na kufanya siasa kwa misingi ya kidemokrasia.

Amebainisha kuwa katika siku za karibuni baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitoa kauli zenye mihemko ya kisiasa ambazo zinaweza kupelekea uvunjifu wa amani, hili linapaswa kudhibitiwa, demokrasia isiyo na mipaka ni fujo.

‘Naomba serikali au mamlaka husika zikemee au kuchukua hatua dhidi ya wale wote wanaotoa kauli zinazoashiria uvunjifu wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi wa Viongozi wa serikali za mitaa’, amesisitiza.

Askofu Elias Mbagata wa Kanisa la Injili Afrika ameshauri serikali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kujipanga vizuri ili kuhakikisha uchaguzi ujao unafanyika kwa amani na utulivu na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Ili kuhakikisha uchaguzi ujao unakuwa huru na wa haki ameshauri wale wote wenye tabia ya kugawa fedha za rushwa ikiwemo wanaonunua vipalata vya wapiga kura waonywe mapema na hatua stahiki zichukuliwe ili kuepusha malalamiko.

Padre Constantine Kabudi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora ameomba serikali kutopuuza kauli zenye viashiria vyo vyote vya uvunjifu wa amani kuelekea kwenye uchaguzi, aidha alishauri sheria na taratibu za uchaguzi zizingatiwe.

Shekhe wa Mkoa wa Tabora Ibrahimu Mavumbi ameomba TAKUKURU kuhakikisha elimu ya rushwa inafikishwa kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili wanasiasa watakaopita na kutoa rushwa wakataliwe.

Akitoa mada katika semina hiyo Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma wa Taasisi hiyo Happiness Madeghe amesema kuwa Viongozi wa dini ni kioo cha jamii hivyo akawaomba kuhamasisha waumini wao kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao.

Ameahakikishia kuwa Taasisi hiyo imejipanga vizuri kudhibiti vitendo vya rushwa katika uchaguzi huo unaoatarajiwa kufanyika Novemba 27mwaka huu.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari Mkoani hapa Juma Kapipi ameshauri Viongozi wa dini kutoa matamko ya kukemea vitendo vya rushwa katika ibada zao na mihemko ya aina yoyote inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani.