October 2, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wazee waomba nafasi ya uwakilishi Bungeni

Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora

WAZEE kutoka Mikoa mbalimbali hapa nchini wameomba serikali kuwaboreshea huduma za kijamii na kuwapa nafasi ya Uwakilishi Bungeni ili Mbunge wao aweze kutetea haki zao ipasavyo ikiwemo kusimamia masuala yote yanayowahusu.

Wametoa ombi hilo kwa nyakati tofauti kwenye Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika Kitaifa leo katika Uwanja wa Chipukizi, katika halmashauri ya manispaa ya Tabora Mkoani hapa.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Older People Platiform (TOP) na Mkurugenzi wa Taasisi ya Endeleza Wazee Kigoma (EWAKI) Bi.Clotilda Isidory Kokupima (80) ameomba serikali iwasaidie kuwa na Mwakilishi Bungeni ili apiganie haki zao.

Amesema kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan iko makini na inajali sana wananchi wake, hivyo anaamini hili watalipokea na kulifanyia kazi ili matatizo yote yanayowakabili wazee yaweze kutatuliwa.

‘Wazee tuna matatizo mengi, serikali imekuwa ikifanya jitihada za hapa na pale kutusaidia lakini bado kuna mambo ya msingi hayajafanyiwa kazi, na hatuna mtu wa karibu anayeweza kutusemea kwa ufasaha bungeni’, ameeleza.

Bi.Kokupima amebainisha kuwa hatua ya serikali kuwapa Uwakilishi Bungeni watu wenye ulemavu, vijana, wanawake na taasisi za elimu ya juu, anaamini kundi la wazee pia linastahili sana kuwa na Mwakilishi ili kuwasemea changamoto zao.

Mzee Muhibha Ndeshi (75) mkazi wa Tabora amesema kuwa licha ya serikali kupitisha sera ya afya kwa wazee bado haijatekelezwa kikamilifu na hakuna sheria yoyote inayosimamia sera hiyo, wazee wenye kadi za matibabu ni wachache sana.

‘Kila mmoja ni mzee mtarajiwa, cha kusikitisha serikali haijaweka utaratibu mzuri wa kutuhudumia, hali hii inapelekea wazee wengi kukosa huduma za msingi hivyo kuishiwa nguvu na kufa mapema kabla ya wakati, hili linatuumiza sana’, ameeleza.

Ameeleza kuwa wazee walio na umri wa miaka 60-75 wana uwezo wa kufanya kazi, hivyo akashauri wawezeshwe mikopo nafuu ya kuendeleza maisha yao kwa kuwa sio wote wanaopata pensheni ya kustaafu, wengine walikuwa wakulima.

Bi. Zuhura Maganga (70) kutoka Katavi ameomba serikali kuweka utaratibu utakaowezesha wazee wote kuanzia miaka 60 kuingizwa kwenye pensheni angalau kila mmoja awe anapata kuanzia sh 100,000 au zaidi kila mwezi.

Ameongeza kuwa wazee walio wengi wakishafikisha umri wa kuanzia miaka 60 wanaanza kuwa na afya duni kutokana na kukosa huduma za msingi, hivyo akamwomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuliangalia hili kwa jicho la pili.

Amefafanua kuwa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 imefafanua wazi juu ya huduma wanazostahili kupewa wazee lakini huduma hizo hazitolewi na hakuna anayewatetea, hivyo akaomba wawe na Mwakilishi Bungeni.

Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora Abakos Kululetera ameeleza kuwa serikali ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina dhamira ya dhati kuinua maisha ya wazee, ndiyo maana imeendelea kuwapatia huduma za afya.