September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hospitali ya Aga Khan, Taasisi ya Moyo Tanzania washerehekea siku ya Moyo Duniani


Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Imeelezwa kuwa Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kwamba takribani wagonjwa zaidi ya milioni 20 huwa wanakufa kila mwaka duniani kote kwasababu ya magonjwa ya moyo ambayo kwa asilimia 80 yanatokea kwenye nchi za uchumi wa kati na chini.

Hayo yalisemwa  na Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo Tanzania na Rais wa Chama cha madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo Dkt. Robert Mvungi wakati wakisherehekea siku ya moyo Duniani inayosherehekewa kila tarahe 29 Septemba iliyoandaliwa na Hospitali ya Aga Khan kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo Tanzania ambapo washiriki walipata punguzo la asilimia 50 kwenye chunguzi za ziada.

Dkt. Mvungi alisema takribani makundi yote yanaathirika na matatizo ya moyo kutokana na uzito uliozidi kiwango cha kawaida,presha, gandamizo la damu, kisukari, damu kuwa juu, kuvuta sigara na kutofanya mazoezi hivyo aliyataka makundi hayo kuchukua hatua za haraka ili kuepukana na magonjwa hayao.

“Chukua hatua kabla haujapata matatizo ya moyo kwasababu haya matatizo yanachukua rasilimali kubwa sana katika kuyatibu kwahiyo watu wanasema kinga ni bora kuliko tiba”



Aidha Dkt. Mvungi alisema chama chao cha madakatari bingwa wa magonjw ya moyo Tanzania watafungua kampeni ambayo haitaishia mjini pekee bi itafika na vijijini pamoja na sehemu zote za nchi ili kuweza kutoa elimu kuhusu magonjwa hayo na kuweza kuchukua hatua.

“Tunajua serikali yetu inajitahidi kuweka mikakati mbalimbali kuhusu magonjwa ya moyo, lakini bado haijawafikia walengwa wote hapa Tanzania, tunataka tuwafikie walengwa hata vijijini hivyo kupitia siku hii mkakati ni kwamba tuweze kutoa elimu kuwafikia watu waweze kujua matatizo ya moyo, wajikinge na wachukue hatua” Alisema

Akizungumza kwa niaba ya Daktari Bingwa wa Moyo kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dkt. Javed  Jalbani , Dkatari mbobezi na bingwa wa magonjwa ya hayo kutoka Hospitali ya Aga Khan, Julius Msukuya alisema kati ya asilimia 25-30 ya wagonjwa ambao wanawapokea katika hospitali ya Aga Khan wanamagonjwa ya moyo yakiwa ni magonjwa mtambuko lakini pia wagonjwa ambao wanawaona ni zaidi ya asilimia 30 -50 wana shida ya moyo na matibabu yake yameimarika yakiwa ni mkusanyiko wa chakula na mzoezi lakini pia usaidizi wa dawa kutoka kwa madktari.



Aliwataka watu wote kufanya maamuzi ya haraka dhidi ya ugonjwa wa shambulizi la moyo kwani hatua za haraza zinaweza kuleta tofauti kubwa katika matokeo ya matibabu.

“Usipuuzie dalili za magonjwa ya moyo , fanya uamuzi wa haraka dhidi ya ugonjwa wa shambulizi la moyo, katika siku hii ya moyo Duniani ni muhimu kwamba tuweke Afya ya moyo kuwa kipaumbele kwa kujifunza kutambua daliliza awali za shambulio la moyo , hatua za haraka zinaweza kufanya tofauti kubwa katika matokeo ya matibabu, pamoja tunaweza kuongeza uelewa na kukuza jamii yenye afya bora ya moyo”

Naye Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Biashara wa Hospitali ya Aga Khan , Stiven Olayce alisema  Rais samia amekua akisisitiza suala la utalii wa mataibabu huku akiitaka Tanzania kuwa ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Subsaharan Afrika kufanya matibabu ya aina mbalimbali iliwemo ya moyo hivyo hospitali hiyo wameendelea kuwekeza katika teknolojia kwani kwa sasa tayari wamekamilisha uwekaji wa vifaa husika katika vyumba vya upasuaji ambapo ifikapo mwakani kutakua na mapinduzi makubwa ya huduma ya moyo.



Daktari bingwa wa magonjwa ya dharura katika Taasisi ya Aga Khan,Hussein Manji  alisema tayari wanamiundombinu ya kupambana na magonjwa hayo huku akiwasihi wananchi kulinda afya zao ili dharura za moyo zisitokee.