September 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Rais Samia Songea yaendelea kuwa ya kishindo

Na Cresensia Kapinga, Timesmajirainline, Songea.

ZIARA ya Rais Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuwa ya kishindo, ambapo mbali ya kuzidi kupata mapokezi makubwa, ameendelea kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani.

Katika mwendeleo huo wa ziara yake, Rais Samia ametoa miezi mitatu kwa RUWASA kukamilisha mradi wa maji wa Mchangombole uliopo Halmashauri ya Madaba wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma

Aidha, amewataka wananchi kutoharibu vyanzo vya maji, kwani vyanzo hivyo ndio uhai wa binadamu na wanyama.

Alisema miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali ili iweze kuwa endelevu ni pamoja na kuhakikisha miundombinu inalindwa kwa kuwa maji ni rasilimali muhimu inayogusa maisha ya kila kiumbe.

Rais Samia, aliyasema hayo jana wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa maji wa vijiji vitatu uliopo katika Kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya Madaba ambao hadi kukamilika utakuwa umegharimu sh. Bilioni 5.5.

Alisema ni jukumu la kila mwananchi kulinda chanzo cha maji cha mto Mtichi ambao upo katika hifadhi ya Milima ya Matogoro B na sio jukumu la watu wa maji ambao kazi yao ni kuangalia maji yapo wapi ,watafanya nini ili maji yasambae yawafikie wananchi na si vinginevyo.

“Niwaombe kutoharibu kile chanzo cha maji ule ndio uhai wenu,maji haya yatatumika kwa matumizi ya binadamu ,wanyama lakini pia kwenye baadhi ya maeneo kwa hiyo niwaombe msiende kuharibu kile chanzo kinachotupa maji kule mtoni tuende tutumie, lakini kuwe na ulinzi wa kutosha,” alisema Rais Samia.

Alisema katika Mkoa wa Ruvuma ameweka jiwe la msingi kwenye miradi 30 inayoendelea mkoani humo, mradi huo utakwenda kuhudumia vijiji vitatu na ndio kusudio lakini kwa kuwa maji yatakuwa mengi yatakwenda kwenye kijiji kingine cha nne .

“Ndugu zangu mnakumbuka wakati wa kampeni tuliahidi kumtua ndoo mama kichwani sasa tumeenda kuifanyia kazi habari ile tumeifanyia kazi kwa kusambaza maji nchi nzima kama mnavyoona tulivyofanya hapa Ruvuma na hivyo hivyo kwa nchi nzima kwa hiyo tunatarajia ikifika mwaka 2025 tuwe tumetimiza lengo la vijiji vyote vya Tanzania vipate maji,” alisema Dkt. Samia.

Kwa upande wake katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri akisoma taarifa ya mradi wa maji Mchangombole alisema umekamilika kwa asilimia 50 na tayari wamejenga nteki ambalo lina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 1.9 na baada ya hapo watajenga mabomba yenye urefu wa mita 20.9 ambalo litafika kwenye matenki mawili yaliyojengwa Mtyangimbole ambapo tenki moja lina uwezo wa lita 150..

Alisema,Tenki la pili linaujazo wa lita laki mbili litahudumia vijiji viwili kijiji cha Luhimba na Likarangiro na watajenga mtandao wa maji wenye urefu wa kilometa 19.97 na vituo 24 vya kuchotea maji, hivyo kuwa na mtandao wa maji wenye urefu wa kilometa 52.7 pamoja na vituo vya maji vipatavyo 40 ambapo mahitaji ya maji katika vijiji hivyo ni lita 634 ambapo chanzo hicho kina uwezo wa kuzalisha lita milioni 1.9.

“Rais uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi huu unawakilisha miradi yote 30 ya maji inayoendelea kutekelezwa mkoani Ruvuma, ambapo itakapokamilika itasaidia wananchi 14,000 kupata huduma ya maji safi na salama, kwani hivi vijiji havijawai
pata maji ya bomba bali vinatumia maji ya visima vya zamani,” alisema alisema Waziri.

Naye Waziri wa Maji Juma Aweso amemshukuru Rais Samia, akisema; “Ulitupa maelekezo maji yapatikane miji na vijijini, kwa sasa nakuhakikishia asilimia kubwa wanaoteseka na adha ya maji ni akina mama.

Sitaki kusikia, kuona wamama wa nchi hii wanateseka kwa kukosa maji ,kazi umeifanya kwa muda mfupi inaonekana kwa macho, umetoa asilimia 50 ya upatikanaji wa maji vijijini hadi asilimia 79 na tuna miradi zaidi ya 200 inayoendelea haijawahi kutokea sawa na asilimia 89.”

Wakati huo huo, Samia , ameongoza hafla ya uwekaji jiwe la msingi kwa ujenzi wa maghala 28 mapya ya kuhifadhi nafaka katika eneo la Luhimba, Ruvuma.

Hafla hii imefanyika jana ambayo ni hatua muhimu kwa wakulima katika kuhakikisha uhifadhi bora wa mazao yao.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, aliyehudhuria hafla hiyo, alieleza kuwa maghala hayo 28 ni sehemu ya awamu ya kwanza ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia ya kujenga maghala 70 vijijini, ambayo yana uwezo wa kuhifadhi tani 28,000.

Kila ghala lina uwezo wa kuhifadhi tani 1,000, jambo linalotarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wakulima wa maeneo husika.

Maghala hayo yatajengwa katika halmashauri nne za wilaya, ambazo ni Songea Manispaa (ghala 1), Songea DC (maghala 11), Madaba (maghala 9), na Namtumbo (maghala 7). Waziri Bashe alibainisha kuwa tayari maghala matano kati ya 28 yameanza kutumika kuhudumia wakulima, huku mengine matano yakitarajiwa kukamilika katika wiki chache zijazo.

Ujenzi wa maghala haya unagharimu sh. bilioni 14.7, ambapo kila ghala limejengwa kwa gharama ya sh. milioni 527.

Pia, Waziri Bashe alimueleza Rais Samia kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ina mpango wa kujenga maghala makubwa ya kisasa yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000 kila moja katika mikoa mitano yenye uzalishaji mkubwa wa mazao, ikiwa ni pamoja na Katavi, Rukwa, Ruvuma, Songwe, na Tabora.

Uwekezaji huu unalenga kuimarisha usalama wa chakula nchini na kutoa fursa zaidi kwa wakulima, huku ukionesha juhudi za Serikali katika kuhakikisha mazingira bora ya kuhifadhi mazao kwa maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo.