September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwenge wataka mazingira bora ya uwekezaji

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline,Tanganyika.

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024, Godfrey Mnzava ametoa wito kwa taasisi zote za umma zinazofanya uwezeshaji kwa wananchi kibiashara kutengeneza mazingira rafiki na rahisi ya kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Mnzava amesema hayo leo Septemba 13, 2024 katika kijiji cha Ikaka Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi wakati akifungua kiwanda kidogo cha Flamingo food Co Ltd ambapo amefafanua kuwa mazingira bora ya uwekezaji yatawahakikishia wawekezaji kuona sehemu salama ya kuweka mitaji yao.

Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa mikoa mitano nchini inayotajwa kuwa na uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula ambapo kiongozi huyo, amesema kuibuliwa kwa viwanda vingi zaidi utasaidia kutoa ajira kwa wananchi na kuinua uchumi wao huku akiwaomba wananchi kutumia fursa ya viwanda hivyo kuongeza thamani ya mazao yao.

Vilevile wakulima kupata eneo sahihi la kuhifadhia mazao yao ili kupunguza upotevu wa mazao kutoka shambani hadi kwa mlaji na wawekezaji watachangia pato la taifa kupitia kulipa kodi kwa serikali.

“Nakipongeza kiwanda cha Flamingo Co.Ltd kwa kuwa kinaongeza thamani ya zao la mpunga” Amesema kiongozi huyo, Ambapo pia Septemba 9, 2024 aliweza kufungua kiwanda kingine cha Mtemi Rice kilichopo kijiji cha Majimoto Manispaa ya Mpimbwe kimejengwa kwa gharama ya Mil 201 kikiwa na uwezo wa kuchataka tani 96 kwa siku moja.

Kiwanda cha Mtemi Rice na Flamigo Co Ltd ni kati ya viwanda viwili vya kisasa mkoani Katavi ambavyo vinatoa mchango makubwa kwenye sekta ya kilimo kutokana na kuongeza thamani zao la mpunga na kuuzwa katika nchi za Zambia, Burundi, Uganda, Rwanda na Congo DRC.

“Kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru, Godfrey Mnzava akizungumza Jambo na mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesimo Buswelu.”

Meneja wa kiwanda cha Flamingo Co.Ltd, Enea Elia akisoma taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru Godfrey Mnzava amesema kuwa ujenzi wa kiwanda hicho umegharimu Mil 700 na kuwepo kwa kiwanda hicho umetoa fursa wakulima na wafanyabiashara.

Fursa hizo ni pamoja na wakulima kuuza mpunga kwa karibu zaidi na kuepuka gharama za usafirishaji kupeleka sokoni, kutoa ajira za kudumu na muda, kuchangia mapato ya ndani ya halmashauri na kuongeza thamani ya zao la mpunga kwa kuchakatwa na kuwekwa katika madaraja na kusafirishwa ndani na nje ya nchi.

Mkulima wa Kijiji cha Mnyagala wilaya ya Tanganyika, Shindika Mashala ameshukuru kuwepo kwa kiwanda hicho kwa kuwa na uhakika wa kuuza mazao yake kwa urahisi zaidi tofauti na hali iyokuwepo hapo awali ambapo alisafirisha kwa umbali wa km 75 kutafuta masoko.

Aidha ameomba serikali kuendelea kutoa elimu ya kilimo kwa wakulima kwani bado wengi hao wanafanya kilimo cha mazoea na kukosa tija ya uzalishaji.

“Moja ya mtambo wa kupongeza thamani zao la mpunga uliopo katika kijiji cha Majimoto halmashauri ya Mpimbwe.”

Aidha Mwenge wa uhuru kitaifa 2024 katika mkoa wa Katavi umemalizika leo kwenye wilaya ya Tanganyika ukikimbizwa zaidi ya km 150 na kuzindua mradi wa maji Mnyagala wenye thamani ya Bil 1.3 fedha kutoka serikali kuu na kutembelea shamba la miti zahanati ya Kagunga.

Mwenge wa uhuru umezindua zahanati ya Kagunga wenye gharama ya Mil 408.2, kuzindua jengo la wagonjwa wa nje OPD katika kituo cha afya Sibwesa wenye gharama ya Mil 216.2 na kuweka jiwe la msingi bweni la wasochana shule ya sekondari Majalila wenye gharama ya Mil 170.

Pamoja na uzinduzi na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi hiyo, Mwenge wa uhuru umetembelea kikundi cha vijana Gift Kasekese wenye thamani ya Mil 25, kuzindua klabu ya kupambana ba kuzuia rushwa shule ya sekondari Sibwesa wenye thamani ya Mil 1.3 na kuzindua klabu ya lishe shule ya sekondari Sibwesa wa Mil 1.3.

“Meneja wa kiwanda Cha Flamingo food co.Ltd, Enea Elia akitoa taarifa ya uwekezaji wa kiwanda kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru Godfrey Mnzava.”