September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TANAPA yazindua Twenzetu Kilele msimu wa nne

Na Penina Malundo,Timesmajira

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa kushirikiana na wadau makampuni ya waongoza watalii nchini imezindua rasmi kampeni ya msimu wa nne wa Twenzetu Kileleni 2024, huku ikitarajiwa zaidi ya Watanzania 500 kusheherekea siku ya Uhuru katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro.

Kampeni hiyo imezin jana jijini Dar es Salaam katika ofisi za TANAPA, huku ikiwa na kauli mbiu isemayo “Stawisha Uoto wa Asili Tanzania, Okoa Barafu ya Mlima Kilimanjaro”, kampeni ambayo imezunduliwa leo mpaka Disemba 4, 2024. 

 Akizungumza tukio hilo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara wa TANAPA, Jully Lyimo amesema kuwa lengo la kampeni hii ni kusherehekea miaka 63 ya Uhuru, tukio ambalo ni la kihistoria hufanyika kila mwaka ifikapo Disemba 9.

 “Katika sura ya Utalii, TANAPA imekuwa ikitumia fursa hii ya maadhimisho ya siku ya uhuru kuhamasisha watanzania kupanda mlima Kilimanjaro na kutangaza vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hii kupitia kampeni ya “Twenzetu kileleni” lengo la kampeni hii ni kuhamasisha Watanzania kupanda mlima ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa Tanganyika”.

 “Nichukue nafasi hii kuwahamasisha Watanzania wenzangu kushiriki upandaji huu ikiwa ni kuonyesha uzalendo na kupenda vivutio vyetu,”amesema

Amesema kwa mwaka huu ni msimu wa nne wa kampeni hiyo, tunatoa hamasa kwa watu binafsi, watanzania ndani na nje ya nchi, mabalozi, taasisi za Serikali na binafsi kujitoa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi hizi.

 “Kama tulivyofanya mwaka jana jumla ya kampuni tatu ndio zimejitokeza kushiriki kampeni hii katika msimu huu wa nne Kampuni hizo ni ZARA Tours, African Zoom na African Scenic,”amesema Kamishna Lyimo. 

Aidha, siku saba kwa njia ya Machame na kwa Lemosho itakuwa siku 8 huku Gharama za kupanda mlima zitakuwa ni shillingi 1,55,000/- kwa njia ya Marangu, shillingi 1,830,000/- kwa njia ya Machame na 2,000,000/- kwa njia ya Lemosho ameongeza Kamishna Lyimo.

Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu Mapinduzi Mdesa kutoka Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro amewataka watanzania wote kujitokeza katika kuadhimisha sherehe hizo za uhuru katika kilele kirefu zaidi barani Afrika pamoja na kushiriki katika juhudi za kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro.

 “Kama mwenyeji wa mlima niwakaribishe watanzania kuja kushiriki nasi katika sherehe hizi za Uhuru katika Paa la Afrika lakini tunajukumu la kuokoa barafu ya Mlima Kilimanjaro kwa kustawisha uoto wa asili kwenye maeneo yetu”,amesema.

 Aidha, Mdesa aliongeza kuwa tafiti zinaonyesaha kuwa chanzo cha barafu kuyeyuka Mlima Kilimanjaro ni uwepo wa pepo kavu zinazotokea baharini na maeneo mengine ya nchi zikifika kwenye ile barafu ya Mlima Kilimanjaro zinapelekea Barafu ile kupungua ukubwa wake na kutoa rai ya kukijanisha Tanzania kwa kupanda miti ya asili ili pepo zinazotoka kwenye fukwe ziende na unyevu na kusaidia barafu iendelee kuwepo. 

Historia inaonyesha kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa na utaratibu wa kuadhimisha sherehe za Uhuru wa Tanganyika tangu ulivyopatikana mwaka 1961. Maadhimisho haya yamekuwa yakifanyika kwa kupandisha bendera ya nchi yetu katika kille cha Mlima Kilimanjaro. 

Tukio hili limekuwa likihusisha kikundi cha wanajeshi wachache wakishirikiana na askari wa Hifadhi za Taifa Tanzania kwa utaratibu wa kampuni ya utalii ya ZARA ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita maadhimisho haya yalipata sura mpya ya ushiriki wa wananchi na kutambulika kwa jina la”Twenzetu Kileleni” ambapo kwa sasa ni msimu wa nne.