November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makalla:Naheshimu maamuzi ya Jeshi la Polisi

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, amesema anaheshimu maamuzi ya Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngorongoro ya kumzuia kufanya mkutano Ngorongoro Mkoani Arusha.

CPA Makalla, ambaye pia ni Mlezi wa Dar es Salaam kichama, amesema hayo Agosti 28, 2025 Jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Sokoine Azimio Wilayani Temeke, kwenye muendelezo wa ziara yake ya siku tatu katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Amesema, kutokana na katazo hilo la kutofanya mkutano Ngorongoro lililotolewa na Jeshi la Polisi, CPA Makalla amesema ataendelea na maeneo mengine yaliyokuwa yamepangwa, ambayo ni Longido Monduli na Karatu.

“Nikiwa kama Mwenezi wa Chama nilitakiwa kufanya ziara Ngorongoro mkoani Arusha, lakini baada ya kupata barua ya zuio la kufanya mkutano wa kichama kutoka Jeshi la Polisi nchini, hivyo sitafanya tena mkutano eneo hilo kwani naheshimu maamuzi ya Jeshi la Polisi na badala yake nitaendelea katika maeneo mengine” amesema CPA Makalla.

Aidha CPA Makalla amesema ni vyema wananchi wote wakaendelea kuunga mkono juhudi za CCM kwani ndicho chama chenye mkataba na wananchi katika kuwaletea maendeleo.

Pamoja na hayo CPA Makalla amewataka watendaji katika taasisi za umma, kuwa na Lugha nzuri wanapotoa huduma ili kuendelea kuleta Imani kwa wananchi huku akisisitiza kuwa,CCM ipo kwa ajili ya kutatua kero na changamoto za wananchi na si kuzikimbia.

Akizungumzia kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, CPA Makalla amewahimiza wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura  ifikapo Oktoba 11 hadi 20, 3024, ili waweze kushiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao utafanyika Novemba 27 mwaka huu.

Hata hivyo amewahakikishia  wananchi, kuwa CCM itawaletea wagombea wazuri ambao hawana makando kando ili waweze kuwapelekea maendeleo kwenye maeneo yao.

Sambamba na hayo, CPA Makalla wakati akiendelea kuhutubia wananchi katika mkutano huo, alionesha kuguswa na Mama ambaye hakufahamika jina lake kwa haraka, aliyekuwa akiuza barafu ‘Ice cream’ huku akiwa amebeba mtoto mgongoni katika mkutano huo, ambapo alimuita na kumsaidia Sh. 200,000 nao viongozi wengine walionesha kuguswa na kuanza kuchangia hadi kufika Sh. 620,000 ambazo alikabidhiwa ili zimsaidie kujikimu kimaisha.

“Kuna mama anauza ice cream tangu naingia hapa kwenye mkutano nilimuona anapita pita anauza ice cream kama yupo naomba aje hapa mbele, imenigusa sana ndugu zangu kwani maisha haya tumepitia wengi nikiwemo mimi, kwani hata Mama yangu amewahi kuwa Mama Ntilie wakati Baba akiwa Askari hivyo nilipomuona Mama huyu tena akiuza huku akiwa na mtoto mdogo mgongoni imenigusa naomba nisaidie kiasi kidogo ili kimsaidie na mtoto huyu mgongoni akiwa anaona”, amesema CPA Makalla