Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline
KLABU ya Azam FC yenye maskani yake jijini Dar es Salaam, imekuwa timu ya pili kwa mwaka huu kuonja Ladha ya zawadi ya Goli la Mama, baada ya kukabibidhiwa Sh Milioni 5 kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni matokeo ya ushindi wake wa bao 1-0 dhidi ya wageni wao APR kutoka nchini Rwanda waliomenyana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wengine walionyakua zawadi hiyo ya Goli la Mama ni Yanga SC, walioibuka na ushindi wa magoli 4-0 dhidi ya wageni wao Vitalo ya nchini Burundi, ambapo kwa matokeo hayo timu hiyo ya Tanzania ilikabidhiwa Sh Milioni 20 kutoka kwa Rais Samia.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Damas Dumbaro, alisema ni jambo la kumshukuru Mungu kuona Azam FC wameshinda bao 1-0 dhidi ya timu ngumu ya APR.
Alisema ni jambo la kutia moyo kuona ushindi wa Azam katika mechi ya kwanza utawatia moyo kuelekea mechi yao ya marudiano ili aweze kusonga mbele, ikiwamo hatua ngumu ya kupenya kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Wakati huu ambao Rais Samia anatoa zawadi ya Goli la Mama, ni matumaini yetu kuona timu zetu zinafanya vizuri katika mashindano haya ili iwe ni shangwe kwa Watanzania wote, haswa wakati huu tunaona Rais wa nchi akiweka nguvu zaidi,”
Alisema Ndumbaro.
Naye Mtendaji Mkuu wa Azam FC Abdulkareem Popa alisema wanajivunia kuona nao wamekuwa miongoni mwa timu za Tanzania zinazonufaika na hamasa ya goli la mama, haswa baada ya wao kuanza kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya APR.
“Kwakweli Rais Samia amefanya jambo kubwa kwa mpira wa Tanzania, sio kwetu tu Azam, bali kwa timu zote zinazoshiriki michuano ya Kimataifa kama vile Yanga, Simba na Coastal Union,” Alisema Popa.
Azam FC inajiandaa kusafiri hadi jijini Kigali, nchini Rwanda kwa ajili ya kumenyana na APR katika mechi yao ya marudiano itakayotoa jibu la timu gani inaenda hatua ya pili ya michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025