September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wakala wa vipimo Zanzibar wajifunza kutoka WMA Bara

Na Nwandishi Wetu, Timesmajira Online

MKURUGENZI Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai amefanya ziara ya siku mbili mkoani Mtwara kwa lengo la kujifunza majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) ambapo amekiri kunufaika zaidi ya alivyotarajia.

Akizungumza baada ya kuhitimisha ziara yake, Agosti 17, mwaka huu, Simai amesema lengo hasa la ziara hiyo lilikuwa kutembelea eneo linalotumiwa na Wakala wa Vipimo Mtwara kwa ajili ya ukaguzi na uhakiki wa magari ya kusafirishia mafuta ili ZAWEMA ikatumie teknolojia hiyo na kuboresha zaidi huko Zanzibar.

“Hata hivyo, ziara hii imekuwa ya mafanikio makubwa kwetu kwa sababu tumepata zaidi ya kile tulichokusudia,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai (katikati), akisikiliza maelezo kutoka kwa Mussa Kongola, Msimamizi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Kampuni ya Maurel & Prom, Madimba Mtwara (kushoto). Kulia ni Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mtwara (WMA), Saad Haruna. Simai alitembelea Mtwara Agosti 16 na 17, 2024 kujifunza namna WMA mkoani humo inavyotekeleza majukumu yake.

Akifafanua, Simai ameeleza kwamba mbali na kujionea na kujifunza kuhusu uanzishaji wa mtambo wa ukaguzi na uhakiki wa magari ya kusafirishia mafuta, amepata fursa ya kutembelea maeneo mengine ambako WMA hutekeleza majukumu yake ikiwemo Bandari ya Mtwara na katika eneo ambalo gesi asilia huvunwa na kuchakatwa huko Madimba.

Amesema, matarajio yake ni kwenda kuibua miradi mbalimbali ukiwemo wa ujenzi wa eneo la ukaguzi wa magari ya mafuta ambao utaenda sanjari na ujenzi wa mtambo wa kisasa wa ukaguzi wa dira za maji kwa njia ya kielektroniki. “Hata hivyo kwa nilichokiona huku WMA Mtwara, iko haja kutumia mtambo wa kawaida pia pamoja na uwepo wa huo wa kielektroniki,” ameeleza.

Simai amemshukuru Mtendaji Mkuu wa WMA Tanzania Bara, Alban Kihulla kwa ushirikiano ambao amekuwa akiutoa kwa ZAWEMA katika kuhakikisha wanatimiza matarajio yao ya kutekeleza majukumu ya uhakiki vipimo kwa ufanisi na tija kwa manufaa ya wananchi wa Zanzibar.

Awali, akieleza kuhusu majukumu yanayotekelezwa na WMA mkoani Mtwara, Meneja wa Mkoa wa Wakala hiyo, Saad Haruna amesema ni pamoja na uhakiki wa vipimo ambavyo hutumika katika sekta za kilimo, biashara, mazingira pamoja na usalama.

Katika sekta ya kilimo, Haruna amesema WMA huhakiki mizani zinazotumika wakati wa kununua mazao pamoja na wakati wa kuyasafirisha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai (mwenye fulana nyeusi-kushoto), akiwa katika ziara ya mafunzo Bandari ya Mtwara. Agosti 17, 2024 kujionea na kujifunza namna majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) katika sekta mbalimbali.

Aidha, kwa upande wa biashara amesema WMA inawajibika kuhakiki vipimo vinavyohusiana na sekta hiyo ambapo ametoa mfano wa mafuta yanayosafirishwa kutoka nchi za nje kuletwa nchini kupitia Bandari ya Mtwara.

“WMA hufanya uhakiki kuanzia Bandarini mafuta yanaposhushwa na kupita kwenye kipimo maalum kijulikanacho kama ‘flow meter’ kwa lugha ya kigeni, zoezi ambalo huendelea kufanyika katika matenki ya kuhifadhi mafuta, vituo vya mafuta na katika pampu zinazotumika kujaza mafuta katika magari.”

Vilevile, Haruna amesema jukumu lingine ambalo hutekelezwa na WMA mkoani humo ni kuhakiki dira mpya za maji ambazo hutumika kuwafungia wateja maji pamoja na zile ambazo zilikwishaanza kutumika.

Pia, katika sekta ndogo ya gesi asilia, amesema WMA huwajibika kuhakiki vipimo vyote vinavyotumika kupima kiwango cha nishati hiyo kuanzia inapovunwa hadi kiwango kinachopelekwa kwa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa ajili ya kuzalisha umeme, kiwango kinachopelekwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na hata kile kinachopelekwa kwa Kampuni kubwa ya kuzalisha saruji ya Dangote.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai (katikati), akisisitiza jambo kwa Mussa Kongola, Msimamizi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Kampuni ya Maurel & Prom, Madimba Mtwara (kushoto) na Meneja wa Wakala wa Vipimo Mkoa wa Mtwara (WMA), Saad Haruna. Simai alitembelea kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia Agosti 17, 2024 kujifunza namna WMA mkoani humo inavyotekeleza majukumu yake katika sekta mbalimbali.

Akizungumzia malengo ya kuhakiki vipimo, Haruna amesema ni jukumu la Serikali kupitia Wakala wa Vipimo, kuhakikisha pande zote zinalindwa yaani mlaji apate bidhaa kadri alivyolipia bila kupunjwa ilhali muuzaji apate malipo stahiki kulingana na kiwango alichouza.

Kwa upande wake, mmoja wa Wasimamizi wa Mtambo wa kuchakata gesi asilia katika Kiwanda kilichoko Madimba, Mussa Kongola ameipongeza Serikali kwa kuanzisha Wakala wa Vipimo akisema inatekeleza majukumu muhimu sana yanayozinufaisha pande zote.

“Uwepo wa jicho la tatu ni muhimu sana ili kuhakikisha pande zote zinanufaika kwa kupata kilicho stahiki na kwakweli nimewafahamu WMA kwa muda mrefu, kazi yao ni njema sana,” amesisitiza.

Ikumbukwe kwamba, kwa mujibu wa takwimu kutoka TPDC, asilimia 60 ya umeme unaozalishwa nchini kupitia TANESCO hutokana na gesi asilia. Aidha, korosho ambazo huzalishwa kwa wingi mkoani Mtwara ni moja ya mazao ya kimkakati yanayolimwa nchini. Vilevile, uwepo wa Bandari ya Mtwara pamoja na maeneo mengine mbalimbali ambayo yanatumia vipimo, vyote vinadhihirisha umuhimu wa uwepo wa Wakala wa Vipimo kwa manufaa ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA) Mohammed Simai (kushoto), akiwa katika ziara ya mafunzo katika kiwanda cha kuchakata gesi asilia kilichoko Madimba, Mtwara, Agosti 17, 2024 kujionea na kujifunza majukumu yanayotekelezwa na Wakala wa Vipimo Tanzania Bara (WMA) katika sekta mbalimbali.

Utendaji mzuri wa wataalamu wa Wakala wa Vipimo Tanzania Bara umekuwa ukivutia nchi mbalimbali kuja kujifunza namna bora ya kuendesha sekta hiyo.

Ziara ya mafunzo ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Vipimo Zanzibar imefanyika mkoani Mtwara badala ya Dar es Salaam au Mkoa mwingine kulingana na ukubwa wa kazi zinazotekelezwa na ZAWEMA ambao unaelezwa kuwiana na majukumu yanayotekelezwa na WMA Mtwara.