*Aagiza kiwanda cha Mkulanzi kuzalisha sukari kwa ajili ya wananchi, atumia falsafa ya aliyekuwa Rais wa Ethiopia, aitaka NFRA kuhifadhi sukari kama inavyofanya kwa chakula
Na Penina Malundo,Timesmajiraonline,Kilosa
RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo ya kuhakikisha tatizo la sukari nchini kubaki historia kwa kukitaka kiwanda kipya cha Sukari Mkulazini, kuzalisha kwa ajili ya wananchi hata kama kukiwepo kwa mabadiliko ya kisera, kikodi au mabadiliko yoyote.
Pia aliitaka Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuingiza sukari kama moja ya chakula cha kuhifadhi, ili kukiwa na upungufu wa sukari nchini iweze kudhibiti upungufu, kwa kutumia akiba hiyo.
Rais Samia alitoa maelekezo hayo jana wakati akizungumza wilayani Kilosa mkoani Morogoro wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho cha Sukari Mkulazi kinachomilikiwa na taasisi za Serikali.
Rais Samia alisema hata kukiwepo kwa mabadiliko hayo kiwanda hicho hakitaweza kusitisha kuzalisha, hivyo kufanya uzalishaji ajili ya nchi.
Alisema uwepo wa kiwanda hicho kuna umuhimu wake katika uwekezaji kwa Serikali na sekta binafsi (PPP) katika kutoa uhakika wa kutoa sukari nchini.
Rais Samia alisema kiwanda hicho kimejengwa na taasisi za Serikali, hivyo kukiwa na mabadiliko mbalimbali uenda kwa sekta binafsi wasiridhike nayo na kuvuta nyuma kidogo, na uzalishaji ukapungua, lakini kiwanda hiki kitazalisha kwa ajili ya nchi.
”Niwaambie wana miradi, wanahisa tutaangalia iwezekanavyo kufanya utanuzi wa kiwanda hiki…nilipata tetemeko kidogo wa sukari kwa mwezi Februali au Machi hadi Aprili, ziliponyesha mvua nyingi viwanda havikuweza kuzalisha, lakini sukari kwenye baadhi ya maeneo ilikuwepo na baadhi ya maghala ilikuwepo, lakini watu wakabana na sukari ikapanda bei kupindukia, kiasi ambacho Mtanzania wa kawaida hasingeweza kununua.
”Sukari si chakula chetu wakubwa, ni chakula cha watoto, sisi wakubwa ikifika umri unakataa sukari na hata kama unatumia ni kidogo sana ila watoto hawawezi kuacha kutumia sukari ,lakini pia wafanyabishara wadogo wadogo kama mama lishe matumizi ya sukari ni makubwa unapomwambia akanunue sukari kwa sh. 7000 au 8,000 hawezi kupata chochote,”alisema.
Alisema uwepo wa kiwanda hicho kitaepukana na changamoto aidha za kumenyesha mvua, kwani akiba itakuwa ndani katika ghala ambapo itachukuliwa na kuwafikishia wananchi bila migogoro yoyote na heshima kuwepo.’
‘Kwa mtu binafsi huwezi kumwambia hatoe sukari ghalani labda uende na mtutu wa binduki na hapo kutakuwa hakuna utawala bora,”alisema.
***Akizungumzia NFRA
Alisema aliwaambia watu wa NFRA waingize sukari kama moja ya chakula cha kuhifadhi, ambapo huko mbele watafanya NFRA kununua sukari na kuweka vile inavyotakiwa kuhifadhika ili inapotokea ukosefu wa sukari NFRA watakuwa nayo na kiwandani pia watakuwa nayo, hii tunaenda kuwahudumia wananchi bila kuwa na changamoto yoyote,” alisema.
”Nawapongeza kwa ajira mlizotengeneza kiwandani na mashambani hizi ni ajira nyingi, niombe muende nao vizuri hatutaki kuona vyama vya wafanyakazi wanakuja na kuleta matatizo kwa sababu kiwanda cha Serikali mambo yote yaende murua,”alisema .
Aidha, Rais Samia alisema kiwanda hicho kinatakiwa kuwa endelevu na kuondokana na dhana ya kitu kikiwa cha Serikali au kikiwa na mkono wa Serikali umakini wake unakuwa sio mkubwa.
Alisema hali hiyo imesababisha viwanda vingi vya Serikali kushindwa kuendelea. ”Nadhani kuna mambo ambayo Serikali inadhibiti viwanda hivi au kuna mambo tu kitu kikiitwa cha serikiali kinakuwa hivi,Meneja mradi nataka usimamie kwelikweli mradi huu.
Nataka uwe endelevu mradi huu, kama kutakuwa kuna mkono wowote unatoka juu kuingiza, zipo sera ya kiwanda nenda moja kwa moja sikwambii usiwe flexible, ila kiwanda hiki kisimame,” alisema na kuongeza;
”Sasa hapa natumia njia ya Rais wa Ethiopia, alikuwa akiwaambia huu mradi ukifa na wewe ufe, na mimi nasema mradi huu ukifa ufe nao, usife mradi wewe ukawa hai , mradi ukifa na wewe ufe , vinginevyo ukiishi na wewe uishi kwa manufaa ya taifa.”
Aidha, Rais Samia alihimiza suala zima usalama mahali pa kazi akisema hiyo ni sehemu yao ya kazi, hivyo wanapaswa kufuata kanuni zote ikiwemo vifaa vya kulinda wafanyakazi na bima ya wafanyakazi.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa