September 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kamera 6500, kufungwa kwenye majiji manne nchini

Na Ashura Jumapili, TimesMajira Online Kagera

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Daniel Sillo,amesema katika mradi wa Majiji salama jumla ya kamera 6,500 za kisasa zinatarajiwa kufungwa katika Majiji manne hapa nchini.

Sillo,amesema hayo wakati akiongea na Kamati ya Usalama ya Mkoa wa Kagera pamoja na Askari na kudai kuwa hayo ni maboresho yanayofanywa katika vyombo vya ulinzi nchini.

Amesema kamera hizo zitaanza kufungwa kwenye Jiji la Arusha,Mwanza,Dar -es Salaam na Dodoma maeneo ya viwandani,sokoni na yenye mikusanyiko ya watu pamoja na barabara kuu.

Ameeleza kuwa lengo la kufunga kamera hizo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na mali zao sambamba na kupunguza matukio ya uhalifu.

Pia amesema Wizara imeagiza magari mengi kwa ajili ya makamanda wa mikoa wa Jeshi la Polisi ( RPC )na Wakuu wa vituo wa Wilaya ( OCD ) nchi nzima.

Vilevile Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wameagiziwa magari ya zima moto 150 ambayo watayagawa mikoa yote na wilaya zake kwa thamani ya dola milioni 100.

Aidha boti 23 ambazo ztatumika baharini na kwenye mito hasa Mkoa wa Kagera,helkopta moja,mitambo mbalimbali ya uokoaji na gari za wagonjwa (ambulace )40 .

Hata hivyo amesema wameboresha mfuko wa tozo na tuzo kwa sababu hapo awali hapakuwa na sheria wala kanuni ili asilimia 60 ya mapato ijenge vituo vya polisi na nyumba za askari.

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 maboma 77 ya vituo vya polisi Wilaya na Kata yatakamilishwa sambamba na kujenga vituo vipya 12 vya polisi kwenye Kata.

“Hivi karibuni kuliibuka wimbi la utekaji watoto,kuuawa na kunyofolewa baadhi ya viungo lakini habari nyingine zilikuwa ni huzushi ,sijasema ukatili haupo upo,”amesema Sillo.

Amewataka viongozi wa usalama linapotokea jambo watoe ufafanuzi mapema ili kuondoa taharuki kwa umma isiyokuwa ya lazima.

Hata hivyo alilipongeza jeshi la Magereza kwa kazi nzuri wanayoifanya ya uzalishaji Mali na kutoa elimu kwa wafungwa ili waweze kujitegemea baada ya kumaliza vifungo vyao na kuwa raia wema.

Pia ,amesema yapo madai mengi ya vitambulisho vya Taifa ( NIDA )hasa maeneo ya Wilaya za Kyerwa na Ngara hivyo amezitaka mamlaka husika kuendelea kutoa vitambulisho hivyo kwa watu wanaokidhi vigezo kwa mujibu wa sheria.

“Kuweni makini katika suala hili lisiingiliwe na wanasiasa kwa presha za uchaguzi na kujikuta mnatoa vitambulisho kwa watu wasiokuwa na sifa,”amesema Sillo.

Ameeleza kuwa vitambulisho vya Taifa ni ulinzi wa nchi hivyo wapewe wanaohusika tu kwa ajili ya maslahi ya kulinda nchi.

Pia ,amesema usambazaji wa vitambulisho viliyotoka uanzie ngazi ya Kata na vijiji ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kupata kadi zao kwa wakati.

Pia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana katika kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia,ubakaji wa watoto,ulawiti na unyanyasaji wa wanaume na wanawake huku akisisitiza kuwa suala la amani ni jukumu la kila mtanzania sio jeshi pekee.

Kwa upande wake kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera ( RPC ) Blasius Chatanda ,amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa Mkoa huo umejiandaa kikamilifu katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Askari namba H.4147 wa kikosi cha Wanamaji Kagera ,alimuomba Naibu Waziri huyo kuboresha makazi ya Askari kuishi chumba kimoja na watoto ni changamoto kwani hali hiyo inaweza kuchangia wao kutokutimiza majukumu yao kwa ufanisi.

Naye namba P.3233 Mkaguzi kutoka Jeshi la Magereza Bukoba,amesema wanakabiliwa na uhaba wa usafiri ,makazi ya Askari na uhaba wa vifaa vya mawasiliano.