September 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi kupata elimu ya mbolea maonesho 88 Mwanza

Na Mwandishi wetu,Mwanza

MAMLAKA ya Udhibiti wa mbolea Tanzania (TFRA),Kanda ya Ziwa imejipanga kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wanaotembelea banda la Mamlaka katika maonesho yanayoendelea viwanja vya Nyamhongolo Jijini Mwanza ili kujifunza.

Akizungumza bandani kwake, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Kanda ya Ziwa, Michael Sanga amesema kufuatia uwepo wa mbolea za ruzuku kumekuwa na muitikio mkubwa wa wakulima kutumia mbolea, hivyo wao kama wadhibiti wa mbolea wanahakikisha elimu ya matumizi sahihi ya mbolea inamfikia kila mkulima.

Amesema kutokana na mwitikio huo Mamlaka imekuwa ikishirikiana na Kutokana na vyama vya ushirika kusaidia katika kusambaza mbolea ya ruzuku lakini pia maafisa Ugani wamekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea.

Ameongeza kuwa, Kanda yake imejipanga kuhakisha msimu wa kilimo unapowadia wakulima wanajua maeneo ya kupata mbolea ya ruzuku, lakini pia kuwa na uelewa wa namna sahihi ya kutumia mbolea.

Ametoa wito kwa wakulima kujitokeza kwa wingi ili wawe na uelewa wa namna ya kunufaika na mbolea za ruzuku ikiwa ni pamoja kufahamishwa maeneo ya kujisajili ili kuingia kwenye mfumo wa mbolea za ruzuku.

Naye Afisa Udhibiti mbolea wa TFRA Kanda ya Ziwa Khanafi Mohamed amesema moja ya changamoto wanayokutana nayo ni wakulima kutokuwa na uelewa wa majukumu ya Mamlaka na hivyo kuhisi ndio wanauzaji wa mbolea.

Amesema jambo hilo wamekuwa wakitoa elimu na kiwaonyesha sehemu sahihi ya kupata mbolea kwa ajili ya matumizi yao ya kilimo.

“TFRA inajitahidi kuwafikia wakulima kwa elimu ili kuwajenegea uwezo katika nyanja mbalimbali zinazohusiana na tasnia ya mbolea nchini,”amesema.