November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dulla Mbabe amtwanga TKO Alen

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

BONDIA wa kimataifa wa Tanzania Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ amemtwanga bondia Alen Mlati kwa ‘Technical knock Out (TKO)’ ya raundi ya nne katika pambano lisilo la ubingwa la raundi nane lililofanyika usiku wa kuamikia jana kwenye ukumbi wa Dar Live, Mbagala.

Toka raundi ya kwanza Mbabe alionesha dalili ya kushinda pambano hilo kutokana kumtupia makonde makali mpinzani wake ambaye naye alionesha kurudisha mashambulizi.

Lakini kuanzia raundi ya tatu, Mbabe alionekana kutawaza zaidi pambano hilo na raundi ya nne alimtupia makonde makali mpinzani wake yalimfanya kushindwa kuendelea na pambano hilo.

Katika pamabano lingine lililofanyika usiku huo, bondia mkongwe, Mada Maugo ameshindwa kutamba mbele ya Imani Mapambano katika pambano la taundi nane la uzito wa Light Heavy lililomalizika kwa sare ya pointi.

Bondia Selemani Kidunda amemshinda kwa ‘Technical knock Out (TKO)’
ya raundi ya pili bondia Ambukile Chusa katika pambano la raundi sita la uzito wa Super Middle.

Kwa upande wake Fredy Sayuni ameangukia pua baada ya kupingwa kwa pointi na mpinzani wake Haidal Mchanjo.

Akizungumzia mapamabano hayo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Kulipwa (PST), Anthony Rutta amesema kuwa, mapambano hayo hayakuwa ya ubingwa na lengo kuu lilikuwa ni kupima uwezo wa mabondia hao mara baada ya janga la Corona kupita.

Amesema kuwa, pia rekodi za pambano hilo zitatumwa kwa shirikisho la ngumi ulimwenguni ambano limekuwa likikusanya rekodi za kila pambano ambazo zimekuwa zikitumika kuwapandisha au kuwashusha viwango mabondia.

“Licha ya kuwa pambano hili halikuwa la ubingwa lakini rekodi zitatumwa kwa wahusika ambazo pia zimekuwa zikisaidia kujua ni bondia gani bado yupo kwenye ngumi lakini pia zitatumika watakapokuwa wanapanga orodha ya viwango vya mabondia kwa kila uzito, ” amesema Rutta.