September 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbunge Ulenge akerwa na wazazi kuwataka watoto kujifelisha

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Mkinga

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhandisi Mwanaisha Ulenge amesikitishwa na kauli za baadhi ya wazazi kuwaeleza watoto wao kuwa wasifaulu, kwani wakifanya hivyo wazazi hao watavunja chungu ili wafe.

Madai hayo yametolewa na mwalimu mmoja wa Shule ya Sekondari Bosha iliyopo Kata ya Bosha wilayani Mkinga, kuwa kama mwanafunzi atafaulu, mzazi atavunja chungu (kimila) na watu wote wa ukoo huo watakufa.

Mhandisi Ulenge ameelezwa hayo Julai 28, 2024 akiwa kwenye ziara ya mkoa mzima wa Tanga kufika kwenye shule za sekondari kuhimiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuweza kufaulu ili baadae waweze kuwa na maisha mazuri wao na wazazi hao.

Ni baada ya kutoridhishwa na matokeo ya shule hiyo kuanzia mwaka 2021 hadi 2023, ambao matokeo yake ni mabaya na yanawafanya watoto wasiweze kufaulu na kusonga mbele kwa elimu ya kidato cha tano ama kwenda vyuo vya kati.

Mhandisi Ulenge amesema Rais Dkt. Samia Sulihu Hassan anapeleka fedha nyingi kwenye elimu kwa ajili ya kujenga miundombinu na kuboresha hali ya elimu nchini, lakini inapotokea wazazi wanawakatisha tamaa watoto wao wasifaulu, inakatisha tamaa juhudi za Rais Dkt. Samia.

“Watoto wangu, ni kweli wazazi wenu hawataki mfaulu na wanawatisha kwamba mkifaulu watakufa?” aliwauliza wanafunzi hao wa Shule ya Sekondari Bosha, na kukiri kuwa ni kweli, wanatishiwa hivyo na wazazi wao.

“Inasikitisha sana kuona baadhi ya wazazi wanawatisha na kuwazuia watoto wao wasisome na kufaulu wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan  anatoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga miundombinu ya madarasa na nyumba za walimu, na kuboresha kiwango cha elimu nchini.

“Nataka kuwaeleza watoto wangu, marafiki zangu, hatima ya maisha yenu ipo mikononi mwenu. Ili kuwa na maisha mazuri ni lazima usome. Elimu haina optional (kuchagua), usiposoma lazima maisha yatakupiga tu. Someni kwa nguvu zote ili elimu hiyo ije kukusaidia wewe na huyo mzazi wako anaekuzuia usifaulu” alisema Mhandisi Ulenge.

Akizungumza na wananchi Kata ya Mhinduro  mara baada ya kutembelea Shule ya Sekondari Lanzoni, aliwataka wazazi kulima mazao ya chakula ili waweze kupeleka chakula hicho shuleni, kwani gharama ya kuwalipia watoto wao wanaoishi hosteli sh. 400,000 kwa mwaka kama pesa ya chakula, ingeweza kupungua kama chakula hicho wangelima wenyewe.

“Wazazi wenzangu, nimekwenda Shule ya Sekondari Lanzoni nimekuta mtoto mmoja analipa sh. 400,000 kama pesa ya chakula kwa yule anaeishi hosteli. Lakini nimeona ardhi yenu ni nzuri, hivyo mngeweza kulima na kupunguza gharama ya fedha ya chakula ili watoto wote wanaostahili kukaa shuleni wakae huko huko” amesema Mhandisi Ulenge.

Mhandisi Ulenge katika kutoa motisha na ari ya watoto kujisomea, alitoa sh. 200,000 kwa kila shule ikiwemo Bosha, Lanzoni na Kwale ili kinunua mchele kwa wanafunzi wa kidato cha nne wanaojiandaa na mtihani wa kitaifa.