September 21, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baba atuhumiwa kumuua mtoto wake,kisha ajinyonga

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online, Mwanza

Watu wawili wilayani Magu mkoani Mwanza akiwemo mtoto wa miaka mitatu wameuwawa huku watuhumiwa wa mauaji hayo wakidaiwa kukutwa wamejinyonga katika matukio mawili yalitendeka kwa nyakati tofauti.

Akizungumza mkoani hapa Agosti Mosi,2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza DCP.Wilbrod Mutafungwa, ameeleza kuwa katika tukio la kwanza lililotokea Julai 28,2024 majira ya saa 11 na dakika 30, alfajili wilayani humo ambapo Lukonya Kisumo(3), mkazi wa kijiji cha Sayaka aliuawa kwa kunyongwa shingo na baba yake mzazi aitwaye Kisumo Emmanuel(38) mkulima na mkazi wa kijiji hicho.

Mutafungwa amedai kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kufanya tukio hilo aliutupa mwili wa mtoto huyo kwenye kisima cha maji kilichochimbwa kwenye shamba la mpunga.

Baada ya kutekeleza unyama huo inadaiwa baba huyo alijinyonga kwa kutumia kipande cha shuka alichokifunga kwenye mti umbali wa kilomita moja kutoka nyumbani kwake.

Ameeleza kuwa Julai 26,2024 alimpokea mtoto huyo kutoka kwa mama ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama na Julai 28,2024 ndipo alipopata nafasi ya kuongozana na mtoto huyo umbali wa mita mia tano kutoka nyumbani kwake na kutekeleza mauaji hayo.

Uchunguzi wa tukio hilo ulifanyika kwa kukagua eneo la tukio ambapo mwili wa marehemu ulichukuliwa na kupelekwa hospitalini kwa uchunguzi zaidi.

“Wakati Askari wa Jeshi la Polisi wakiendelea kumsaka mtuhumiwa huyo katika maeneo mbalimbali ya Kijiji cha Sayaka ndipo waliweza kumpata akiwa ameshafariki dunia huku mwili wake ukiwa unaning’inia kwenye mti ndani ya shamba la jirani yake umbali mfupi kutoka kwenye nyumba alipokuwa akiishi,mwili wa marehamu huyo umefanyiwa uchunguzi pia na tayari umekabidhiwa kwa ndugu kwa mazishi,”ameeleza DCP.Mutafungwa.

Katika tukio jingine DCP.Mutafungwa ameeleza kuwa Julai 30,2024 majira ya saa 10 na dakika 30 kitongoji cha Nela, kijiji cha Kisamba, Kata ya Lubugu wilayani Magu ambapo Christina Kisinza,(40) aliuawa kwa kukatwa shingo na kitu chenye ncha kali na mume wake aitwaye Fednand Mabula(41) mkazi wa kijiji hicho wakati wakiwa wamelala chumbani kwao.

DCP Mutafungwa ameeleza kuwa chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa muda mrefu uliotokana na wivu wa kimapenzi baada ya mwanaume kumtuhumu mke wake kuwa na uhusiano na mwanaume mwingine.

Baada ya kutenda unyama huo mtuhumiwa alitoweka na kwenda kusiko julikana na wakati askari wa Jeshi la Polisi wakiendelea kumsaka katika maeneo mbalimbali ya kijiji hicho ndipo Julai 31,2024 walipata taarifa kutoka kwa wananchi kuwa kuna mwili wa mwanaume mmoja unaninginia kwenye mti.

“Walipofika walikuta mwili wa mtuhumiwa huyo ukining’inia kwenye mti katika eneo la uwanja wa Mwanankanda,kjiji cha Kisamba,”.

Wakati huo huo Mutafungwa ameeleza kuwa Jeshi hilo linamsaka Benjamin Masanye(29), Mkazi wa Usegeng’e kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mke wake aitwaye Veronica Ndabile(23).

Ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea Julai 31,2024 majira ya saa mbili na dakika 30 ,usiku kijiji cha Isegeng’e , Kata ya Mwakiliambiti wilayani Kwimba baada ya marehamu kukatwa na kitu chenye ncha kali sehemu za mabegani, shingoni na miguu yote miwili na kusababisha kifo chake na mume wake huyo wakati alipokuwa nyumbani kwa mama yake mzazi.

“Mtuhumiwa alifika nyumbani kwa mama mkwe wake aitwae Limi Nyanda na kuingia kwenye chumba ambacho marehamu alikua amelala na kuanza kumshambulia kwa kumkata na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wake,”.

Hata hivyo ameeleza kuwa baada ya mtuhumiwa huyo kutekeleza unyama huo alipiga simu kwa baba mlezi wa marehamu aitwae John Lyeni na kumueleza kwamba yeye ndiye aliyemuua mtoto wao kwa sababu walimkatalia asimchukue na kwenda kuishi nae,ambapo ametaja chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia.

Sambamba na hayo, Jeshi la Polisi mkoa wa Mwanza limeanza ufuatiliaji wa haraka wa kumtafuta mtuhumiwa popote alipo ili aweze kukabiliana na mkono wa sheria.

“Tunaomba wanachi watoe ushirikiano kwa kutoa taarifa za mhalifu huyo na wahalifu wengine ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka iwezekanavyo,pia waache

kujichukulia sheria mkononi badala yake mtumie njia sahihi ya kutatua matatizo kwa kuwashirikisha viongozi wa dini, wazazi na taasisi za ushauri nasaha,”.