November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Samia kuandika historia, kuzindua safari za SGR

*Anazindua safari zake kesho na kuifanya Tanzania nchi ya kwanza Afrika na ya tano Duniani kwa mtandao mrefu zaidi wa Reli ya SGR, kubeba tani 10,000 za mzigo kwa mkupuo

Jackline Martin na Joyce Kasiki, Timesmajiraonline,Dar na Dodoma

RAIS Samia Suluhu Hassan, anatarajia kuandika historia kwa kuwa Rais wa kwanza nchini tangu Uhuru kwa kuzindua utoaji huduma wa usafiri wa treni katika Reli ya Viwango vya Kimataifa (SGR) kuanzia Dodoma kwenda Dar es Salaam, kupitia Morogoro.

Uzinduzi huo unafanyika ukiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa kwa uongozi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuwa ifikapo Julai safari za treni hiyo ziwe zimeanza kati ya Dar es Salaam na Dodoma.

Aidha, hatua hiyo ni kielelezo cha utekelezaji wa ahadi zake za kuendeleza miradi yote iliyoachwa na mtangulizi wake, Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli, aliyefariki Machi, 2011.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema uzinduzi huo utafanyika kesho, Agosti 1, 2024 Mkoani Dodoma, ambapo kupitia mradi huo Tanzania imekua nchi ya kwanza Afrika na ya Tano Duniani kuwa na mtandao mrefu zaidi wa Reli ya SGR.

Alisema treni za kisasa zenye kutumia nishati ya umeme zitakuwa na uwezo wa kubeba mzigo mkubwa hadi tani 10,000 kwa mkupuo ambazo ni sawa na malori 500 ya mizigo, ambapo itasaidia kupunguza mrundikano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza uharibifu wa barabara.

Prof. Mbarawa alisema SGR itaongeza soko la ndani na kuimarisha shilingi ya Tanzania kwa sababu treni inatumia umeme utakaozalishwa nchini. “Endapo tungetumia mafuta ya dizeli ambayo huagizwa kutoka nje ya nchi ingeongeza gharama kubwa za uendeshaji na matumizi ya akina ya fedha za nje, matumizi ya umeme kwa uendeshaji wa treni ya kisasa ni rafiki wa mazingira pia inapunguza gharama mara tatu ukilingaliswa na utumiaji wa mafuta, kupungua kwa gharama za uendeshaji inaleta nafuu ya gharama kwa wananchi,”alisema.

Pia alisema kuanza kwa huduma za usafiri katika reli ya kiwango cha kimataifa kutachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la pato la Taifa pamoja na maendeleo ya shughuli nyingi za kiuchumi, kijamii ja kiutawala kwa kutoa usafiri wa uhakika na wa haraka.

Sekta ambazo zinatarajiwa kuguswa moja kwa moja na usafiri wa reli ya SGR ni pamoja na biashara, utalii, viwanda, kilimo, uvuvi na ufugaji,” alisema Prof. Mbarawa alisema zipo njia mbili ambazo mwananchi anaweza kutumia kukata tiketi za treni za SGR ambazo ni njia ya kawaida kwenye madirisha ya tiketi ndani ya majengo ya Stesheni za SGR na kupitia mfumo wa tiketi unaopatikana kwa anuani https.

“Abiria anashauriwa kukata tiketi mapema ili kuepuka usumbufu na endapo kuna changamoto yoyote abiria anaweza kuwasiliana na TRC kupitia simu ya bure 0800110042 kwa ajili ya kupata msaada.”

Wakati huo huo, Mkuu wa mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewataka wananchi wa mkoa huo na wale wa mikoa ya jirani kuhudhuria uzinduzi huo ili kujionea na kumuunga mkono Rais Samia kwa juhudi zake za kukamilisha kipande hicho cha Dar es Salaam -Morogoro-Dodoma.

Alisema kufuatia uzinduzi huo Tanzania inaenda kuandika historia mpya ya kuwa na treni ya mwendokasi miongoni mwa nchi chache Afrika.

“Tunaenda kuandika historia ambayo haitajirudia maana treni ya mwendokasi ndiyo inaanza ,kwa hiyo tuna kila sababu ya kumpongeza Rais .Samia kwa juhudi.,” alisemana kuongeza; “Leo Rais Samia amekamilisha reli ya SGR kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.