September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

HYDO kutoa elimu kukabiliana na ukatili,matumizi ya dawa za kulevya

Judith Ferdinand,Timesmajira Online,Mwanza


Shirika la Hope for Youth Development(HYDO), limesema litaendelea kutoa elimu kwenye jamii,shuleni,vyuoni na hata kwa vijana ambao wapo nje ya shule ili kuweza kukabiliana na changamoto ya vitendo vya ukatili pamoja na matumizi ya dawa za kulevya ambavyo vinachangia kupoteza nguvu kazi ya taifa.


Ukatili una athiri ndoto za vijana wengi kwani walitamani kufika mahali fulani lakini wakikutana na vitendo hivyo inachangia kukatisha ndoto zao mfano wasichana wanaacha shule wanapata mimba.


Mkurugenzi wa shirika la Hope for Youth Development,Anitha Samson akizungumza na Timesmajira Online ofisni kwake jijini Mwanza hivi karibuni ameeleza kuwa tangua kuanza kwa shirika hilo Januari mwaka 2023 mpaka sasa wameisha fikia vijana 59 wanaofanya nao kazi moja kwa moja na nje ya shule kupitia midahalo ni vijana takribani 500.


“Tunaamini kupitia hao watakuwa mabalozi wazuri wa kupeleka taarifa kwenye jamii na sehemu nyingine ambazo hatuwezi kufika,pia tunatumia vyombo vya habari kuhakikisha tunafikisha taarifa mbali zaidi na kuweza kutoa elimu ya namna gani ukatili unaathiri maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,pia matumizi ya dawa za kulevya yanaweza kusababisha vijana wanajiingiza katika vitendo vya kikatili ikiwemo kuwa wabakaji,”ameeleza Anitha.


Sanjari na hayo Anitha ameeleza kuwa elimu ya afya ya uzazi ina msaada kwa vijana kwa sababu dunia ya sasa imegubikwa na janga la kundi hilo kujihusisha na ngono katika umri mdogo,kupitia elimu hiyo watapata huduma sahihi na uelewa wa kujikinga na ngono na mimba za utotoni.


Kwani wengi wao wanafanya ngono isiyo salama na kusababisha magonjwa,mimba katika umri mdogo,kuacha shule pia ata kufikia hatua ya kujiua kwa sababu ya mahusiano yasiyokuwa salama.

“Elimu hii inasaidia kuhakikisha kijana anapata taarifa sahihi na lini aanze kufanya au kujihusisha na masuala ya ngono,namna gani anaweza kujikinga na magonjwa na namna gani ataweza kufikia ndoto zake, pia elimu hiyo inaenda sambamba na elimu ya stadi za maisha ,”.