November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wabunge viti maalumu Katavi watoa simu janja

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

WABUNGE wa viti Maalumu wa Mkoa wa Katavi,Tasker Mbongo na Martha Maliki wameiomba jamii kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ambapo litawawezesha kutumia haki ya kikatiba ya kuchagua viongozi katika uchanguzi wa serikali za mitaa 2024 na uchanguzi mkuu 2025.

Hamasa hiyo imetolewa na wabunge hao ikiwa tayari zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la mpiga limeanza kufanyika leo Julai 20, 2024 katika Mkoa wa Katavi ambapo wananchi waliofikisha miaka 18 ya kupiga kura na wengi kuhuwisha taarifa zao ambazo zilikosewa au kuhama kwenye maeneo yao ya awali.

Wabunge hao wakizungumza leo katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi wakati wakikabidhi simu janja nane zenye thamani zaidi ya Milioni 1.9 kwa katibu wa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho UWT wamesema wajibu wao ni kuhakikisha jamii yote hususani wanawake wanajiandikisha.

“Tumetoa simu janja kwa chama chetu kwa sababu tunahitaji wanawake wengi zaidi wasajiliwe kwenye mfumo wa UWT sambamba tukitoa hamasa kwa nguvu kila mahala alipo mwanamke wajitokeze kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura” Amesema Taster akiugwa mkono Martha.

Mbunge wa Viti Maalumu, Tasker Mbongo amesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa za maendeleo na kama sehemu ya kumuuga mkono jamii inapaswa kujitokeza kwa wingi zaidi kujiandikisha kwenye daftari  la kudumu la mpiga kura.

Amesema kuwa kuimarishwa kwa sekta ya usafiri wa ndege,barabara, bandari Karema na reli miradi yote hiyo inakisi moyo wake wa upendo na uzalendo kwa Watanzania ambapo jambo hilo linapaswa kulipwa fadhira kwa wananchi kujiandikisha kwenye daftari hilo.

Wakati akiwakumbusha wazazi na jamii kushiriki kwenye malezi bora ya watoto wa kike na wakiume ili kuepuka na kutokomeza mimba za utotoni ambazo kwa mkoa wa Katavi zina asimilia 32.2 amesema wanachama wa CCM wanawajibu wa kujenga nyumba moja kwa kuwa wamoja ili chama hicho kiendelee kushika dola.

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Katavi  maarufu “DADA YA MKOA”, Martha Maliki amesema kuwa simu janja walizotoa ni kwa ajili ya Ofisi ya UWT Mkoa, Wilaya ya Tanganyika, Mlele na Mpanda ikiwa kitendo hicho ni sehemu ya kiu ya kuhakikisha UWT inakuwa na wanachama wengi.

Martha amesema katika kuhakikisha uhai wa UWT Mkoa wa Katavi pia ameshatoa kadi jumla ya 5000 ikiwa awamu ya kwanza ni kadi 2000 na ya pili kadi 3000,Kadi zote ni kwa ajili ya wanawake ambao ni jeshi kubwa lenye mchango katika kila changuzi nchini kwa sababu hushiriki kikamilifu.

Ameeleza kuwa wananchi wanahaki ya kuchagua kiongozi bora atakaye watumikia na kiongozi huyo ni Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani ameonesha uwezo mkubwa wa kiongozi hususani kwenye ujenzi wa miradi ya maendeleo kama vile Hosptali na sekta ya maji kupitia mradi wa miji 28 hivyo wananchi ili waweze kuwa na sifa ya kumchagua wanapaswa kujiandikisha kwenye daftari hilo.

Katibu wa Jumuiya ya Wanawake ya Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Katavi,Edina buzima ameigana na wabunge hao wa viti maalumu huku akiwapongeza kwa kazi nzuri ya kuwatumikia wananchi wa mkoa.

Edina amesema kuwa hamasa inayotolewa na wabunge hao itafanikisha lengo la mkoa la kuandikisha wapiga kura 123,000 ikiwa kwa sasa imeshaanza kufanywa kwenye jumla ya vituo 444 hivyo anahakika kwa umoja huo zoezi hilo litafanikiwa.