November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa

Mwanadiplomasia nguli, mwanasiasa maridhawa aliyeacha alama ya milele

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

NIANZIE wapi kumuelezea Mzee wa Uwazi na Ukweli? Hebu nianzie kwenye kitabu chake cha Maisha Binafsi ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa chenye jina la “Maisha Yangu, Dhamira Yangu:

Rais wa Tanzania Akumbuka” alichokizindua hapo Novemba 12, 2019 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alikuwa Mgeni Rasmi, Mzee Mkapa anasimulia kuwa maono yake: Ni maisha ya hali ya juu, amani, utulivu na umoja, utawala bora, jamii iliyoelimika na uchumi shindani wenye uwezo wa kukua kiendelevu na mgawanyo shirikishi wa kipato.

Ni dhahiri kuwa kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa kilichotokea hapo jana Julai 24, 2020 ni pigo kwa taifa, Afrika pamoja na dunia kufuatia mchango wake ulioakisi mabadiliko ya uchumi, mahusiano ya kimataifa na mapinduzi katika sekta za umma na binafsi.

Kama mjuavyo ni katika uongozi wa Mzee Mkapa ambapo mikakati mbalimbali ya kimaendeleo ilianzishwa, baadhi ni Dira ya Taifa 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA), Mpango wa Kurasimisha Biashara na Mali za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na Mini Tiger Plan 2020.

Mmoja wa wanufaika wa Mfuko wa TASAF akipokea fedha kwa ajili ya kupambana na umasikini.

Aidha, Rais Mkapa alianzisha Bima ya Taifa, Mageuzi katika Elimu, na Mradi wa Maji ziwa Victoria, halikadhalika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), mageuzi haya yalihitaji kiongozi makini mwenye mapenzi kwa taifa lake lakini aliyeishi na kuamini ndoto zake za kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

Shughuli za maendeleo na ukuaji wa uchumi

Wakati wa uongozi wake Mzee Mkapa aliyekuwa Rais, mwandishi wa habari na mwanadiplomasia nguli aliweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii, ikiwa ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kupitiliza malengo na kukusanya kiasi cha sh. bilioni 133 kwa mwezi kati ya Julai na Novemba 2004, kulingana na takwimu za Serikali, kudhibiti mfumuko wa bei kutoka asilimia 30 hadi chini ya 5.5 na kukua kwa uchumi kwa asilimia sita.

Duru za siasa za ndani na kimataifa

Itakumbukwa kuwa Mkapa ni Rais wa kwanza nchini Tanzania kuingia madarakani kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika zama za siasa za vyama vingi mnamo mwaka 1995.

Akiwa amebakiza takriban miezi kumi tu kumaliza kipindi chake cha kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Benjamin William Mkapa aliwahi kukemea tabia ya watu wanaotishia kuvunja amani katika nchi aliyoipokea kutoka kwa wenzake waliomtangulia ikiwa na amani na utulivu.

Alionesha wazi kuwa mfumo wa siasa wa vyama vingi haukuanzishwa nchini ili kudhoofisha utaifa, umoja na mshikamano kwa taifa.
“Hatukuanzisha mfumo wa siasa wa vyama vingi ili watu wetu wachukiane, watishane kwa kunoa mapanga waumizane, wauane au waharibiane mali zao,” alisema Mzee Mkapa.

Hakuna shaka kwamba utawala wa Rais Mkapa ulijaa mambo mengi mazuri ambayo hayataweza kufutika katika kizazi hiki na mara kadhaa alihubiri juu ya amani, na kuheshimu haki za binadamu ikiwemo haki ya kuishi.
Katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu, ni vyema tukakumbuka aliyowahi kusema Rais Mkapa mwaka 2005 wakati ambapo nchi ilifanya Uchaguzi Mkuu.

“Tuje tuwaogope sana wanaohubiri chuki kwa kisingizio cha ushindani wa kisiasa. Ushindani tunaotaka sisi ni wa hoja, wa fikŕa, wa mikakati na mipango ya maendeleo. Tunashindanisha ilani za uchaguzi wa vyama.

Ningependa vyama vyetu vyote vya kisiasa viwe na malengo makuu yanayofanana yaani umoja, amani, upendo, maendeleo na ustawi wa taifa na wananchi. Tunachotofautisha na tunachoshindania kiwe mipango na mikakati ya kufikia malengo hayo makuu,” alisema Mzee Mkapa.

Aidha, Mzee Mkapa alikuwa mpatanishi wa mgogoro wa Burundi ambapo alizitaka pande husika katika nchi hiyo kushikamana na kuheshimu mchakato wa amani na hatua zilizopigwa za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Pia, alihusika katika upatanisho wa migogoro ya nchi za Sudani ya Kusini, Congo Mashariki, na Kenya.

Katika hali isiyotarajiwa na wengi ni kwa kiongozi aliyewahi kuwa Rais kukiri wazi juu ya udhaifu wake, ambapo aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Rwekaza Mukandala amechambua wasifu wa Mzee Mkapa katika kitabu chake cha Maisha Yangu, Dhamira Yangu: Rais wa Tanzania Akumbuka, anaandika, “Mheshimiwa Mkapa anakiri kuwa, kabla hajawa Rais, hakujua kuwa kazi moja wapo ya Rais ni kutoa pole. Mojawapo ya mapungufu yangu ni kwamba si mwepesi wa kuonyesha hisia zangu. Mrithi wangu Rais Kikwete ni mzuri sana katika hili.

“Anasema Mheshimiwa Mkapa, ameandika Profesa Mkandala.
Mwisho kabisa Mzee Mkapa, anamalizia kwa kusema; Nitamuachia Mungu wangu na nyinyi kuamua ni tofauti gani nimeifanya humu duniani.

Kama taifa yapo mengi ya kujifunza kutoka kwa Mzee Mkapa na kumuenzi ni pamoja na kuthamini mchango uliosaidia kuleta maendeleo ya kijamii, kiasiasa na kiuchumi.