November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daktari Bingwa wa Moyo JKCI aishauri Serikali kuhusu matibabu ya kibingwa

Na Cresensia Kapinga, Timesmajiraonline,Namtumbo

DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Baraka Ndelwa, ameishauri Serikali kufikisha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo ngazi ya wilaya na kata.

Hatua hiyo inalenga kuokoa maisha ya watu wanaoishi maeneo hayo ambao wengi wao wana kipato cha chini.

Dkt. Ndelwa, alitoa ushauri huo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Kituo cha Afya Lusewa wilayani Namtumbo kilichopo umbali wa kilometa 200 kutoka makao makuu ya wilaya.

Alisema hiyo ni mara ya kwanza tangu walipoanza kutoa huduma za upimaji na uchunguzi wa magonjwa ya moyo kupitia taasisi hiyo kufika kwenye vituo vya afya ngazi ya kata.

Alisema kuwa kwenye vituo hivyo wamebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa baadhi ya vifaa muhimu vya upimaji wa magonjwa hayo.

“Mara nyingi tunafanya kazi hizi kwa ngazi ya mkoa katika kumbukumbu zangu hatujawahi kwenda kufanya kazi ngazi ya wilaya na kata na mara nyingi tunaishia katika Hospitali za rufaa, hii ni bahati kubwa sana kwangu na mimi nimejifunza huku chini kupoje,” alisema Ndelwa.

Baadhi ya wagonjwa waliokuja kuchunguza afya zao jana katika kituo cha Afya cha lusewa.

Aidha, alisema tangu zoezi hilo lilipoanza wamefanikiwa kuwafikia zaidi ya wagonjwa 258 waliofanyiwa vipimo vya magonjwa ya moyo, ambapo waliofanyiwa uchunguzi kwa kipimo cha ECHO ni 185, kipimo cha umeme wa moyo 89 ambapo wagonjwa wanne wamepewa rufaa ya kwenda Taasisi ya Moyo Dar slaam kwa ajili ya vipimo zaidi na ikiwezekana watapatiwa matibabu zaidi.

Alishauri umuhimu wa wananchi kujenga tabia ya kwenda kuchunguza afya zao mara kwa mara kutokana na idadi kubwa ya watu wenye shinikizo la damu kutofahamu hali zao.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa,aliwataka wananchi wa kata ya Sasawala na maeneo mengine kujitokeza kwa wingi kupima afya zao kwani zoezi hilo ni bure na limefanyika kwa mara ya kwanza ngazi ya kata.

“Kiongozi anajivunia kuongoza wananchi wenye afya bora ili kuwasaidia kujiletea maendeleo zaidi kwenye maeneo wanayoishi ukizingatia asilimia kubwa ya wananchi tunategemea kilimo,”alisema Kawawa.

Alisema wananchi watumie fursa ya uwepo wa madaktari bingwa kwenda kupata huduma ya upimaji moyo, shinikizo la damu ,kisukari pamoja na kupewa elimu sahihi ya lishe bora.

Mkazi wa Kijiji cha Ligunga, Athumani Haule, alisema kituo cha Afya Lusewa kipo mbali sana na Hospitali ya Wilaya Namtumbo, hivyo ujio wa madaktari bingwa umesaidia wananchi kupatiwa huduma na kujua matatizo yanayowasumbua kiafya.

Naye Pilly Said ,mkazi wa Lusewa, alishafika kituo kwa ajili ya matibabu na madaktari.

Dkt. Baraka Ndelwa akibadilishana mawazo na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa katika Kituo cha Afya Lusewa.

Alisema awali aliambiwa ana changamoto ya moyo, lakini baada ya kufika madaktari bingwa amepatiwa matibabu na kubainika kuwa ana changamoto ya Acid kwenye mfumo wa chakula.

Kwa upande wake Diwani Kata ya Lusewa, Said Zidadu alisema huduma inayotolewa kwenye kituo cha afya cha Lusewa ni ya muhimu na itawasaidia watu wengi kupima afya zao ili kujua magonjwa yanayowasumbua ambapo yeye ni mmoja wa watu waliopimwa na amegundulika hana shida.