October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Tulia ampa tabasamu mwanafunzi aliyeshindwa kuripoti shule kwa kukosa mahitaji

Na Esther Macha, Timesmajira Online,Rungwe

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dkt.Tulia Ackson amemsaidia kiasi cha shilingi 550,000 Richard Mwaisela (18), mwanafunzi aliyeshindwa kuripoti kidato cha tano shule ya sekondari Kisondela wilayani Rungwe kutokana na kukosa mahitaji ya shule.

Msaada huo wa fedha umekabidhiwa na Taasisi ya Tulia Trust ambayo Mkurugenzi wake ni Dkt. Tulia Ackson ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani.

Richard ambaye ni yatima anaishi na bibi yake katika Kijiji cha Mpuga Kata ya Kisondela Wilaya ya Rungwe ambaye hana uwezo wa kumsomesha kutokana na kutokuwa na shughuli yeyote ya kumuingizia kipato .

Mwanafunzi huyo alifaulu kujiunga na kidato cha tano shule ya sekondari Isongole wilayani Rungwe ambapo alishindwa kuanza masomo kutokana na kukosa mahitaji ya shule.

“Nitaithamini fedha hii niliopatiwa na Mbunge kwa kujituma kusoma kwa bidii bila kumuangusha kwani amenijali na kunithamini,hivyo nami lazima nioneshe juhudi kubwa za kusoma na kuja kuwa mkombozi wa bibi yangu,”amesema .

Kwa upande wake Kaimu Ofisa Habari na Mawasiliano wa Taasisi ya Tulia Trust,Addy Kalinjira amesema Dkt. Tulia ametoa msaada huo ili aweze kutimiza ndoto za Richard na baadae awe msaada kwa jamii na taifa kwa ujumla.

“Nakusihi ukasome kwa bidii kwani elimu ni mtaji mkubwa sana kwenye maisha yetu hivyo elimu ikawe nguzo yako,”amesema.