November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

SIDO waja na Teknolojia mpya ya ubanguaji korosho

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), wamekuja na Teknolojia mpya ya ubanguaji korosho inayoendeshwa na umeme ambayo itasaidia kuondoa changamoto ya ubanguaji korosho Moja moja kama ilivyokuwa hapo awali.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Sylvester Mpanduji katika maonesho ya 48 ya biashara ya kimataifa sabasaba ambapo amesema kupitia huduma wanazozitoa wapo pamoja na wajasiriamali ambao wamefaidika na huduma zao.

“Hii ni mashine ambayo wanavikundi au mwananchi mmojammoja wakiitumia inaweza kuwaingiza katika uanzishwaji wa viwanda vya ubanguaji korosho”

Aidha Mpanduji amesema wamekuja na Teknolojia nyingine mbalimbali mahususi ya Nishati safi ya kupikia ambapo katika Banda lao majiko yanayotumia Nishati safi yanapatikana.

“Utakapotembelea itakua ni fursa kwako pale utakaponunua au kuona teknolojia hizo” Alisema

Kuhusu mwitikio wa wajasiriamali Katika maonesho hayo, Mpanduji amesema mwaka huu wajasiriamali wadogo 135 wameshiriki ukilinganisha na wajasiriamali 110 mwaka Jana.

” Watanzania wanaendelea kupata mwitikio wa kupata huduma za SIDO na kuweza kuanzisha viwanda vyao”