Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Mbozi
MFAMASIA wa Kituo cha Afya cha Isansa, wilayani Mbozi,mkoani Songwe, Daudi Kwibuja (30), amekufa katika kifo cha kutatanisha na mwili wake kukutwa kando ya barabara kuu itokayo Mbeya kwenda Tunduma (Tanzam) katika eneo la Mlowo, wilayani hapa.
Mwili wa mtumishi huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi katika Idara ya Afya umekutwa ukiwa na majereha mwilini mwake na tayari Jeshi la Polisi limeanzisha uchunguzi.
Akitoa taarifa ya kifo hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga, amesema kuwa uchunguzi unaonesha mtumishi huyo aliuawa usiku wa Julai 3, 2024 na mwili wake kukutwa ukiwa umetupwa kando ya barabara hiyo leo Julai 4, 2024, majira ya asubuhi.
Kamanda Senga amesema licha ya kuwa awali kudhaniwa kuwa marehemu alifariki kwa ajali ya kugongwa na gari, lakini baada ya mwili huo kuchunguzwa umekutwa na majeraha ambayo hayafanani na ya ajali ya kugongwa na gari.
“Uchunguzi unaendelea ili kuweza kubaini ni ajali kweli au mauaji kwa hiyo tunaendelea kuchunguza na tutakapopata ukweli kupitia matabibu tutauhabarisha umma chanzo cha kifo cha ndugu yetu huyu (marehemu) kimetokana na nini,”amefafanua Kamanda Senga.
Aidha amesema kuwa pindi majibu ya uchunguzi yatakapobainisha kuwa marehemu ameuawa Jeshi hilo litahakikisha linawasaka na kuwakamata wahusika wote, huku akiwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa katika jeshi hilo.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi