October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Katibu we Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma Mjini, Ramadhani Dallo akimkabidhi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania ubunge Jimbo la Musoma Mjini, Dkt. Theophili Kayombo mapema leo. (Picha na Fresha Kinasa).

Dkt.Kayombo asema yupo tayari kuwatumikia wananchi

Na Fresha Kinasa,TimesMajira Online, Mara

Daktari Theophili Kayombo amekuwa mtia nia wa 42 kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania ubunge katika Jimbo la Musoma Mjini huku akisema kuwa iwapo chama chake kitampa ridhaa ya kumpitisha kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kufanikiwa kushinda, atahakikisha anatatua tatizo la ajira kwa vijana katika Jimbo la Musoma Mjini.

Kayombo amesema, anaipongeza Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kwa kutekeleza miradi ikiwemo miundombinu ya barabara, maji na vituo vya afya na hivyo amesema kuwa akifanikiwa kuwa Mbunge atahakikisha anasukuma mbele jitihada za maendeleo katika Jimbo la Musoma Mjini kwa kutafuta fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi.

“Nitashirikiana kutekeleza ilani hasa kusaidia vijana kupata mitaji ya kuwawezesha kujiajiri na kuwa na uchumi bora, pia kinamama kuwasaidia kupata mitaji kwa kushirikiana na Serikali kuwakwamua kiuchumi kwa kutumia taaluma yangu ya maendeleo ya jamii kusaidia wananchi wa Musoma,”amesema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kayombo amepongeza Serikali ya Rais Magufuli kurejesha nidhamu kazini, kujenga miradi mikubwa ya maendeleo, amesema iwapo atapewa ridhaa atashiriki kutoa mchango wake kulipaisha Taifa kiuchumi.