November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi na Uvuvi, Luhaga Mpina (kushoto) akipokea fomu ya kuomba kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea Ubunge Jimbo la Kisesa wilayani Meatu Mkoa wa Simiyu. kulia ni Katibu wa CCM Wilaya ya Meatu, Charles Dotto Mazuri. Amechukua fomu leo, Julai 15, 2020

Waziri Mpina aanika sababu za kuwania ubunge tena Kisesa

Na Mwandishi Wetu, Simiyu

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ametaja sababu zilizomsukuma kuwania tena ubunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu Mkoa Simiyu baada ya kuwatumikia wananchi wa jimbo hilo kwa kipindi cha miaka 15 kwa mafanikio makubwa huku akibainisha kuwa kazi ya kusaka maendeleo katika jimbo hilo bado haijakamilika.

Akizungumza nje ya Ofisi Kuu ya CCM Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kuteuliwa kugombea Jimbo la Kisesa, Waziri Mpina amekishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kumruhusu kuchukua fomu hiyo na kuwashukuru wanachama wa CCM kwa kuendelea kumuunga mkono katika safari hiyo.

“Naamua kuchukua fomu ya kugombea Jimbo la Kisesa kwa sababu kazi ya kusaka maendeleo ya jimbo bado haijakamilika,”alisema Waziri Mpina.

Kwa mujibu wa Katibu wa CCM Wilaya ya Meatu, Charles Mazuri hadi kufikia Julai 15 saa saba mchana jumla wa watia nia nafasi ya ubunge kwa Jimbo la Kisesa walikuwa wamefikia tisa, akiwemo Waziri Mpina na Mbunge anayemaliza muda wake.

Mazuri amesema kwa upande wa jimbo la Meatu jumla ya wagombea 11 wamejitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho na kufanya idadi ya wagombea 20 wanaowania nafasi hiyo kwa majimbo yote mawili.

Nao baadhi ya wananchi waliojitokeza kumlipia fomu ya kugombea ubunge jimbo la Kisesa Waziri Mpina walisema wamesukumwa na hali hiyo kutokana na uchapakazi wa mbunge huyo na maandeleo makubwa aliyowapatia katika kipindi cha uongozi wake.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wa CCM kutoka Kata ya Mwakisandu, Monica Mirega amesema wanamshukuru kwa maendeleo aliyowaletea huku wakiamua kumtuma tena.

“Ni kijana mchapakazi, mwadilifu na hachoki katika kazi za maendeleo kwa hiyo nawaomba wanachama wote tumpe tena kura zetu arudi kuchapa kazi” Monica