September 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Kilakala alivalia njuga vitendo vya ubakaji,ulawiti,aagiza kukamatwa kwa mtuhumiwa

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online Pangani

Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mussa Kilakala ameanza kuvalia njuga vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto huku akiliagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kumfuatilia na kumkamata mtu mmoja kwenye kijiji cha Bushiri ambaye ameripotiwa kwa tuhuma za kuwashawishi watoto wa kiume ili afanye nao vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Wilaya amepiga marufuku uuzwaji wa pombe nyumbani ambao umebainika kuwa chanzo cha ukatili wa kijinsia kwa familia hususani wakati ambao watu wanaanza kulewa.

Kilakala ametoa maagizo hayo Juni 24,2024 wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)Wilaya ya Pangani huku akiitaka jamii kuungana kuhakikisha wanafanikiwa kwenye vita dhidi ya ukatili huo kwa watoto.

Mkuu huyo wa Wilaya alitolea mfano mwanafunzi mmoja wa kidato cha tatu kwenye kijiji hicho ambaye mara kadhaa mtu huyo amekuwa akimrubuni kwa kutaka kumlawiti na kwamba ameripoti maeneo kadhaa lakini mtu huyo bado hajachukuliwa hatua.

Ameeleza kuwa alienda kwenye shule moja ( jina lake limehifadhiwa) hapa Bushiri mtoto mmoja jasiri, alizungumza kwa uchungu ambaye alikuwa kidato cha 3 au 4 hivyo kungekuwa na watoto majasiri kama yule hili tatizo lingekwisha kabisa kwa muda mfupi.

“Ameonesha maigizo akaimba baadae akachukua maiki na kuzungumza kuniambia Mkuu wa Wilaya mimi binafsi nimefanyiwa ukatili wa kijinsia kuna mzee ananitaka mimi kimapenzi hali yakuwa anajua mimi ni mtoto wa kiume,nimekwenda kushitaki kijijini,kwenye kata sijapata msaada nimempongeza yule kijana kwa kuwa jasiri,” ameeleza Kilakala na kuongeza kuwa

“Watoto wetu mpaka wanaharibika ndio tuchukue hatua,nimeliagiza Jeshi la Polisi yule mzee anayetuhumiwa wamuhoji atuambie kazi zile anazifanya na nani na ameshawaharibu watoto wangapi Bushiri, mambo haya si kwamba hayapo yapo tukikaa na watoto wetu tutayajua taratibu,”.

Pia amesema baadhi ya kaya zinazouza pombe watu wanapoanza kulewa wanawabaka watoto wa familia bila mama au baba mzazi kujua kutokana na kuwa ‘bize’ na biashara hiyo.

Kufuatia hali hiyo Kilakala amepiga marufuku pombe kuuzwa nyumbani na tayari wameshaanza kuyafungia baadhi ya maeneo ambayo walevi hufanya vitendo vya ovyo eneo ambalo wanafunzi wanapita wakitoka shuleni na wengine kwenda kuiga na kupelekea mmomonyoko wa maadili.

Ambapo amemuelekeza Ofisa Biashara kupitia Mkurugenzi maeneo yote yanayoendesha biashara kiholela yafungiwe mpaka hapo yatakapopata leseni pia wamemuelekeza Mkurugenzi kuhakikisha hakuna watoto kurudi nyumbani wakitokea shule usiku.

“Masomo gani yanapatikana usiku watoto wanarudi nyumbani saa mbili mpaka saa nne usiku wanatoka wapi, muda wa masomo uzingatiwe, mzazi ukiona mtoto hajarudi mpaka saa kumi uanze kuwa na wasiwasi sio mtoto anarudi saa nne usiku unasema hiyo kawaida yake, “amesisitiza Kilakala.

Awali akizungumzia mafanikio waliyoyapata katika Wilaya hiyo Kilakala amesema serikali imewafanyia maendeleo ikiwemo katika sekta ya elimu, afya, maji na barabara.