Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limeongezewa nguvu na taasisi ya African Wildlife Foundation (AWF), kwa ajili ya kutokomeza ujangili katika hifadhi zake.
Taasisi hiyo imelikabidhi Shirika hilo vifaa vya doria ambavyo ni pikipiki, Boots na riders suit, kutokana na jitihada mbalimbali za kutokomeza ujangili zinazofanywa na TANAPA.
Pikipiki hizo 4 na vifaa vingine vimetolewa leo Mei 11, 2024, katika Makao Makuu ya TANAPA yaliyopo mtaa wa Majengo jijini Arusha, ambazo zitatumika katika maeneo korofi ambayo magari ya doria hayawezi kufika.
Mara baada ya kutoa vitendea kazi hivyo, Mwanasheria wa Taasisi ya AWF, Crisent Michael Nyelo amesema vitendea kazi hivyo kwa ajili ya kuunga mkono jitihada zinazofanya na TANAPA kuhakikisha ujangili unatoweka katika hi.
“Tunatoa vitendea kazi hivi kwa kutambua na kuunga mkono jitihada maridhawa za Uhifadhi zinazofanywa na TANAPA. Shirika hili limeendelea kuhifadhi maliasili hizi kwa weledi mkubwa bila kuchoka wala kukatishwa tamaa.
“Mapambano dhidi ya ujangili ni suala mtambuka linalohitaji nyenzo mbalimbali kukabiliana nalo ikiwemo doria za ndege, helkopta, magari, boti, pikipiki na doria za miguu. Hivyo msaada huu utaongeza kazi ya kupambana na wimbi hili la ujangili ambao kila kukicha unakuwa na sura mpya,” amesema Nyelo.
Akipokea vifaa hivyo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Richard Kafwita amewashukuru AWF, kutokana kuwapa vitendea kazi ili kukabiliana na ujangili.
“Nawashukuru sana AWF, kwetu huu si msaada tu ni vitendea kazi na mmetuongezea nguvu zaidi ya kupamba na hawa waharifu, tunawaahidi tutavitumia kama mlivyokusudia kwa maslahi ya TANAPA na Taifa kwa ujumla,” amesema Kafwita
More Stories
Wagombea CHADEMA wakipewa ridhaa,watakuwa wawazi
TTCL yafanya maboresho katika huduma zake
HGWT yawataka wazazi na walezi kulinda watoto dhidi vitendo vya ukatili