November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaombwa kuangalia gharama za masomo ya Afya

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online,Tanga

Imebainika kuwa wataalamu wengi wanaotaka kujiunga na masomo ya huduma za afya ngazi ya kati nchini wanashindwa kuendelea kutimiza ndoto zao kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa mafunzo hayo jambo ambalo serikali imeombwa kulitazama kwa jicho la tatu.

Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya, Kolandoto, mkoani Shinyanga Paschal Shiluka amebainisha hayo kwenye maadhimisho ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika jijini Tanga.

“Kama walivyofanya kwenye mafunzo ya radiolojia, basi wasaidie na mafunzo haya ili wataalamu wengi wanaoshindwa kumudu garama hizi waweze kujiendeleza,hii itasaidia sana hata kupata wataalamu wengi zaidi ambao wanahitajika sana kwenye jamii, lakini pia tutakuwa tumewapunguzia gharama kwa wale ambao hawana uwezo na hatimaye familia zao zitakaa kwa amani” amesema.

Shiluka amefafanua kuwa msaada wanaotamani serikali ifanye ni kutoa mikopo kwa wataalamu hao wa ngazi ya kati na kwakuwa ndiyo wengi hata Bodi ya Mikopo itanufaika zaidi kuliko hata kwa walioko katika vyuo vikuu.

“Hawa ndiyo wanaojiriwa kwa wingi, kwahiyo hata wakipatiwa mikopo kurudisha kwao itakuwa rahisi, takwimu zinatuonesha kwamba wanafunzi wengi wanapenda na wanajiunga lakini wanapofika njiani wanakwana na hii inatuumiza sana kwa kuona nguvu kazi kubwa inapotea bure,”amesema.

Kwa upande wake Ofisa Masoko Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Josephine Charles amesema chuo hicho kimekuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi wanaomaliza masomo yao chuoni hapo na kuwapatia fursa za ajira zinazohusu masuala yote ya afya..

“Tunawafundisha wanafunzi kwa weledi na taaluma lakini pia mwisho wa siku tunawapatia ajira na wanakwenda kwa jamii ambapo zinawajenga na wamekuwa wakifanya vizuri,” amesema.