November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Makalla awatahadharisha wanasingida kutokufanya makosa katika kuchagua viongozi

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Singida

KATIBU wa NEC, Itikadi ,Uenezi na Mafunzo Taifa wa Chama Cha Mapinduzi(CCM),Amos Makalla, amewataadharisha wananchi wa Mkoa wa Singida, kutofanya makosa katika uchaguzi mdogo wa Serikali za Mitaa kwa kuchagua viongozi wasiyofaa na badala yake wachague viongozi sahihi kutoka CCM.

Makalla amaesana kuna watu walishafanya makosa wakaonja sumu ikawadhuru na hivi sasa watakuwa wamejifunza hawatarudia tena makosa.

“Niwaombe na nyie kutoka maeneo yote katika Mkoa huu msifanye makosa ya kuonja sumu kwa kuchagua viongozi ambao hawapo kwa ajili ya maslahi ya wananchi isipokuwa kwa manufaa yao wenyewe na badala yake chagueni viongozi wenye nia ya dhati ya kuhudumia wananchi kutoka CCM na maendeleo mtaendelea kuyaona,” amesema Makalla.

Makalla amesema hayo leo Mei 30, akiwa katika ziara na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, mkoani Singida, ambapo ameeleza kuwa ni vyema wananchi wa Singida wakajifunza kutokana na makosa, hususani katika kipindi hiki cha kuelekekea katika uchaguzi mdogo unaotarajiwa kuanza Novemba mwaka huu na uchaguzi mkubwa wa mwaka 2025.

“Mafanikio haya tuyaseme wakati wote hata Balozi anapaswa kuyasema, kuna wale wanaosema sasa hivi Watanzania wamekuwa machawa yani kila kitu wanamtaja Samia..sasa wanataka tumtaje nani?.Hata wao familia zao zinawapongeza na kuwashukuru pale zinapiwafanyia mambo mazuri ndiyo maana na sisi tunamshukuru Rais pale anapotufanyia mazuri na ndiyo utamaduni wetu kushukuru,”amesema Makalla.

Katika ziara hiyo wameridhishwa na taarifa ya CCM Mkoa kuwa hali ya kisiasa mkoani humo ipo shwari na hakuna wasiwasi kuhusu ushindani kutoka vyama pinzani na kusema kuwa wananchi wa Singida wameonesha kuridhishwa na chama hicho.

“Viongozi wa chama tuendelee kuimarisha chama na kuwatumikia wananchi kwani ndiyo waliotuweka hapa tulipo hivyo viongozi wote kutoka ngazi ya Shina, Tawi na Kata tuendelee kuongeza wanachama wapya,”amesisitiza Makalla.

Sanjari na hayo, amewataka viongozi wa CCM Mkoani humo kutenga siku na muda wa kusikiliza kero za wananchi na si kuwaachia viongozi wa Serikali pekee.

“Niwaombe ndugu zangu viongozi, suala la kusikiliza kero za wananchi ni letu sote na si suala la Serikali pekee, wekeni muda katika ofisi zenu msikilize changamoto zao na zinazoweza kutatuliwa zitatueni zinazohitaji kutatuliwa na viongozi Serikalini muwaelekeze huko,”.

Ziara hiyo iliyoanza Mei 29 na kutarajiwa kumalizika Juni 9 inalenga kutembelea mikoa mitano, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.