January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nyamagana yaanika mafanikio utekelezaji Ilani ya CCM

Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza

SERIKALI wilayani Nyamagana kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025,imeeleza mafanikio ya miradi ya maendeleo yaliyopatikana katika sekta mbalimbali kwa katika kipindi cha Julai,2023 hadi Machi,mwaka huu.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika mkutano maalumu wa Halmashauri Kuu CCM wilayani humo Aprili 22,2024 Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi,amesema serikali imeonesha dhamira ya kuleta maendeleo kwa wananchi na taifa kwa kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na kijamii.

Amesema mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta mbalimbali ambayo kasi yake inaonesha CCM inavyosimamia kwa karibu utekelezaji wa ilani kuhakikisha huduma za jamii zinapatikana kwa wananchi tangu serikali ya awamu ya sita ilipoingia madarakani.

“Serikali ikishirikiana na sekta binafsi na wadau wa maendeleo imekuwa ikitekeleza sera za kimkakati za kitaifa kwa kuzingatia muda,weledi,kuweka mazingira wezeshi,kufutilia changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa sera hizo na kutafutia ufumbuzi,”amesema Makilagi.

Hali ya Uchumi

Makilagi amesema sekta ya fedha ni kipimo cha kuonesha viwango vya uchumi wa nchi vilivyofikiwa na uimara wa uwezeshaji wa sekta hiyo huleta maendeleo ya haraka,hivyo kutoka Julai,2023 hadi Machi, 2024,Jiji la Mwanza,lilikusanya bilioni 16.271 kati ya sh.bilioni 26.546 za makisio.

Amesema ili kuongeza uwezo wa serikali kugharamia huduma za jamii na kiuchumi,katika kipindi hicho Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya bilioni 66.2 kati ya lengo la bilioni 75.5 ambapo makusanyo ya kodi za ndani bilioni 39.658 na ushuru wa forodha bilioni 26.565.

Aidha Wilaya ya Nyamagana,imeendelea kutekeleza mradi wa kimkakati wa Soko Kuu ambao umefikia asilimia 94.5 na mkandarasi amelipwa sh.bilioni 20.2.

Ambapo kuwepo kwa miradi ya kimkakati ya Soko Kuu na Stendi ya Nyegezi,watu 1,275 wamenufaika kwa ajira za muda huku stendi ikiingiza mapato ya sh.milioni 749.8.

Sekta ya Elimu

Makilagi amesema katika kipindi hicho cha Julai, 2023 hadi Machi, 2024, ili kufanikisha msingi wa uchumi wa kisasa Wilaya ya Nyamagana imeboresha,imeimarisha na kupanua miundombinu ya kutolea elimu kuhakikisha ngazi zote zinakuwa na ubora unaostahili.

Amesema milioni 904.2 za elimu bila malipo zilipokelewa kwa shule za msingi 86 na 31 za sekondari,milioni 238 zilipokelewa na Idara ya Elimu za ujenzi wa madarasa 40,matundu 13 ya vyoo, ukarabati wa madarasa 45,utengenezaji madawati 100,ukamilishaji mabweni ya wenye mahitaji maalum.

Aidha kiasi cha milioni 797.8 za mapato ya ndani zilitolewa kukamilisha madarasa 76,maabara tano katika sekondari tatu, kukamilisha jengo la utawala Igogo sekondari na utengenezaji wa madawati 112 na samani.

Sekta ya Maji

Pia, Wilaya ya Nyamagana imekuwa ikitekeleza programu ya maji ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wote.

Hivyo, kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA),imetekeleza miradi ya maji ya Butimba (sh.bilioni 71.7),matokeo ya haraka (sh.milioni 783.1) wa kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo Luchelele na mfumo wa kuondoa na kutibu majitataka Butimba (sh.bilioni 1.97).

Huduma za Jamii

Makilagi amesema sekta ya afya kwa kuzingatia dhamira ya wananchi kuwa na afya bora na kushiriki shughuli za kiuchumi,serikali ikishirikiana na wadau,imewezesha kupatikana kwa huduma bora za matibabu,dawa,vifaa tiba,vifaa saidizi na vitendanishi kwa asilimia ya 100.

Amesema miongoni mwa mafanikio ni kuongezeka kwa vituo vya huduma za upasuaji wa dharura hasa kwa wajawazito (CEmONC),kutoka 7 hadi 14,wataalamu wenye ujuzi wapo kila kituo na ununuzi wa vifaa umefanyika kwa asilimia 98.

Makilagi amesema Jiji lilipokea bilioni 1.55 za ujenzi wa miundombinu ya Hospitali ya Nyamagana,milioni 800 jengo la wagonjwa wa nje la zahanati ya Shadi,milioni 50 na ruzuku ya ununuzi wa makasha ya dawa,vifaa na vifaa tiba zimepokelewa sh.milioni 700.

Amesema Idara ya Afya ilipokea milioni 440.9 za uboreshaji wa afya katika vituo vya kutolea huduma za afya, ununuzi wa dawa na vifaa tiba kutoka kwa wahisani UNICEF na Sector Basket Fund.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Wilaya fedha za mapato ya ndani sh.milioni 180 kati ya hizo sh. milioni 100 zilitolewa kwa ujenzi wa kituo cha afya Mhandu huku sh.milioni 80 zikipelekwa kukamilisha wodi ya wazazi,upanuzi wa miundombinu ya TEHAMA na ununuzi wa vifaa tiba katika zahanati ya Shadi.

Amesema utekelezaji huo wa ilani umegusa pia mradi wa ujenzi wa barabara ya Buhongwa-Igoma ya urefu wa km 14 kwa kiwango cha lami unaogharimu zaidi ya bilioni 22.

Makilagi amesema Wilaya ya Nyamagana itaendelea kuwasistiza wananchi kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuleta tija katika uzalishaji,kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi,kupiga vita ubadhirifu,kuhimiza uwekezaji wa viwanda vinavyotumia malighafi za ndani ili kuongeza kipato cha wananachi na ajira kwa vijana.