November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ziara ya Rais Samia Uturuki kukuza biashara hadi dola bilioni. 1 kwa mwaka

Na Penina Malundo,TimesmajiraOnline,Dar

ZIARA za Rais Samia Suluhu Hassan, zimezidi kuwa na matokeo chanya katika nyanja mbalimbali.

Tangu aingie madarakani tumeshuhudia jinsi alivyoweza kuimarisha ushirikiano na nchi nyingine, hatua ambayo imeweza kuongeza idadi ya wawekezaji.

Tumeshuhidia Tanzania ikizidi kuwa kimbilio la uwekezaji tangu Rais Samia aingie madarakani, achilia mbali kuimarika kwa uhusiano wa kidiplomasia na mataifa mengine.

Katika mwendeleo wa dhamira ya Rais Samia kuhakikisha nchi yetu inakuwa kiuchumi, alikubali mwaliko wa Rais wa Uturuki wa kufanya ziara ya kiserikali, ambapo viongozi hao wawili walikubaliana mambo mbalimbali.

Kupitia ziara hiyo Tanzania na Uturuki zimeweka wazi dhamira za nchi hizo katika kukuza biashara hadi kufikia Dola bilioni 1 kwa mwaka na kuhakikisha zinafungua njia kwa Jumuiya za wafanyabiashara kutoka nchi hizo kutumia fursa zilizopo ili kufikia malengo hayo.

Katika Kongamano kati ya wafanyabiashara wa zaidi ya kampuni 100 za Tanzania na zaidi ya kampuni 200 kutoka Uturuki ,Rais wa Dkt. Samia alipata fursa ya kufungua kongamano hilo na kutoa maelekezo ambayo yatasaidia kufikiwa kwa dhamira hiyo.

Aewataka mawaziri wa biashara kuhakikisha nchi hizo zinafikia lengo la kufikia dola bilioni 1 kwa mwaka katika ufanyaji wa biashara.

Rais Samia Suluhu Hassan akielekea kuweka shada la maua katika kaburi la Rais wa Kwanza wa Uturuki, Hayati Mustafa Kemal Atatürk katika makumbusho ya Anitkabir, Atatürk’s Jijini Ankara nchini Uturuki tarehe 18 Aprili, 2024.

Rais Samia anasema majadiliano na ushirikiano ulioanzishwa kati ya Tanzania na Jukwaa la Biashara la Uturuki mjini Instabul, utafungua njia kwa wafanyabiashara hao katika ufanyaji wa biashara zao.

Anasema kwa sasa kiasi cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki kinafikia karibu dola za Marekani Milioni 300, hivyo imewafanya yeye na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan kujadiliana na kufikia maazimio ya kuongeza kiwango cha ufanyaji wa biashara kati ya nchi hizo mbili.

Hivyo, kupitia kongamano hilo, Rais Samia ametumia fursa ya kuwakaribisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Uturuki kuja kuwekeza nchini na kuitaja Tanzania kuwa nchi yenye fursa nyingi.

Akitaja fursa hizo ni pamoja na ardhi yenye rutuba kwa ajili ya kilimo, utalii na nishati ,madini ikiwemo Tanzanite ambayo hupatikana nchini Tanzania pekee na fursa za biashara na uwekezaji.

Anasema Serikali ya Tanzania imeendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji, ambapo pamoja na mambo mengine imewekeza katika kujenga miundombinu inayoiunganisha Tanzania na nchi nyingine jirani ikiwemo Reli ya Kisasa ya SGR.

Kwa Upande wake Makamu wa Rais wa Uturuki, Cevdet Yilmaz, anasema nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania katika sekta ambazo nchi hiyo imepiga hatua ikiwemo utalii, usafirishaji ,biashara na uwekezaji.

“Naunga mkono wito wa nchi hizi mbili kutumia ushirikiano vizuri na uhusiano uliopo ili kufikia lengo lililowekwa la Biashara,”anasema.

Akizungumzia lengo la kufikia dola Bilioni moja katika ufanyaji biashara baina ya nchi hizo mbili Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji, anasema ni wazi kuwa kiasi cha biashara kati ya Tanzania na Uturuki kinafikia karibu dola za Marekani milioni 352, lakini fursa zilizopo nchini Tanzania ni kubwa.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Mwenyeji wake Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan wakati wakiangalia album ya picha za matukio ya ziara rasmi aliyoifanya katika Ikulu ya Kulliye Ankara nchini Uturuki.

Anasema Mawaziri wa Biashara kutoka Tanzania na Uturuki wamepewa lengo la kufikia Dola Bilioni moja kwa mwaka mmoja na wakuu hao wa nchi hizo mbili, ambapo yeye binafsi amepata fursa ya kuongea na wafanyabiashara wa sekta binafsi kuhakikisha wanatumia fursa zilizopo kati ya Tanzania na Uturuki ili kufikia lengo hilo.

Akitaja miongoni mwa maeneo ambayo yatawafikisha katika lengo hilo,anasema ni pamoja na sekta ya kilimo katika eneo la Pamba,tumbaku na parachichi ambapo zao la parachichi nchini Uturuki hawalimi lakini watu wao wanakula.

Mbali na sekta hizo, Kijaji anasema katika kufikia lengo hilo pia Tanzania inazalisha madini ya aina mbalimbali yakiwemo ya Tanzanite.

“Tumeweza kuitambulisha sekta hii Uturuki ili wadau waweze kuja kuwekeza nasi na kuyachakata pia tuna dhahabu na Daimond na hii itasaidia kuvuka lengo hilo kwa kutengeneza biashara kubwa na ajira kwa watu wote,”anasema.

Anasema Tanzania na Uturuki ni mapacha wawili ambao ushirikiano wao ulianza mwaka 1963 kabla ya Tanganyika kuwa Tanzania,ambapo ushirikiano huo umeendelea katika uchumi, biashara na kisiasa.

Anasema mbali na maeneo hayo pia katika Tamaduni nchi hizo mbili zinafanana na kutopenda migogoro hali inayofanya kutamani kushirikiana kwa pamoja katika ujasiriamali kuwanyanyua watu wa mataifa hayo kutoka katika lindi la umasikini na kuweza kufanikiwa.

*** Kijaji na dhumuni la Kongamano

Anasema kongamano hilo ni la sekta binafsi kutoka nchini Uturuki, Sekta Binafsi ya Tanzania pamoja na Serikali zao wenye lengo la kujadili fursa mbalimbali zilizopo katika mataifa hayo.

Kijaji anasema katika mkutano wa kiserikali kati ya Tanzania na Uturuki, wameona kuna fursa nzuri na kubwa ya kuongeza uwekezaji ndani ya nchi zao na kuongeza ufanyaji biashara.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan wakati wakishuhudia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba na kwa upande wa Uturuki Rais wa Baraza la Elimu Profesa Dkt. Erol Ozvar wakitia saini Makubaliano ya Ushirikiano katika Nyanja ya Elimu ya Juu baina ya Tanzania na Uturuki Aprili 18, 2024.

“Kwa sasa hivi ufanyaji biashara kwetu sisi tunauza kidogo sana Dola Milioni 22 ndio bidhaa tunazoziuza hapa nchini Uturuki na upande wa kununua bidhaa kutoka Uturuki kwenda Tanzania zaidi ya Dola milioni 420,hii inaonesha dhahiri kuwa biashara imelalia sehemu moja,”amesema na kuongeza,

”Namshukuru sana Rais Samia kwa kukubali mwaliko wa Rais Erdogan kuja kufanya ziara ya kitaifa hapa Uturuki, akiwa ameambatana na Sekta binafsi na wafanyabiashara wakubwa wa makampuni 100 kutoka Tanzania.”

Anasema dhamira ya Rais Samia kuambatana na wafanyabiashara hao ni kuwaunganisha na wawekezaji wenzao wa nchini Uturuki kuona namna ngani wataweza kutumia fursa za kibishara.

“Inafahamika kuwa Uturuki na Tanzania zinafanana kiuchumi kwa namna ilivyoanzia,ila kwa sasa imetuacha sana tumekuja na sekta binafsi ya kwetu ili kujifunza kwa pamoja kipi wenzetu wanafanya na sisi tujue wenzetu wanafanya nini ili uchumi wetu uweze kukua,”anasema.

Akielezea fursa zilizopo nchini Uturuki, Kijaji anasema Uturuki wanalima pamba, lakini pamba yao wanaichakata katika viwanda vyao vidogo vya kati na vikubwa ambapo hadi sasa wana uhitaji wa Pamba kwa asilimia 20 zinazohitajika katika viwanda wanavyotengeneza nguo.

“Tumekuja kujifunza wenzetu wanazalisha pamba lakini eneo la viwanda wameweza kuendelea vizuri sana na sisi tunalima pamba ya kiwango cha juu, umeona mfano huo tunaofanana kwa pamoja,”anasema.

Anasema hivyo ujio huo dhamira yake kubwa ni kujifunza ni namna wanavyofanya biashara zao, kwani na Tanzania nayo inalima Pamba katika mikoa mitano ya Tanzania, lakini pamba hiyo inauzwa asilimia 90 nje ya nchi ikiwa malighafi.

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa ziara yake Rasmi katika Ikulu Kulliye Ankara nchini Uturuki Aprili 18, 2024.

“Kuja kwetu huku ni kujifunza wenzetu wamefanyaje ili kuweza kuandaa viwanda vidogo, vyakati na vikubwa ili na sisi tuweze kuchakata pamba yetu ni wazi tutatengeneza ajira kwa vijana wa Kitanzania ,tukiuza kwenye nchi nyingine kama Uturuki tutauza bidhaa ambazo ni za mwisho na bei yake itakuwa kubwa na taifa letu kupata kipato kizuri,”anasema.