Na Jackline Martin, TimesMajira Online
SHIRIKA la Masoko ya Kariakoo (KMC) limesema mradi wa ujenzi wa ukarabati wa Soko la Kariakoo upo katika hatua za mwisho za kukamilishwa tayari kuwarejesha wafanyabiashara kwenye soko hilo, ambapo litafanyakazi kwa saa 24.
Kwa mujibu wa uongozi wa soko hilo mradi wa ujenzi wa soko hilo umefikia asilimia 93.
Pia hadi sasa hatua kadhaa zimeendelea kuchukuliwa ikiwemo utambuzi na uhakiki wa waliokuwa wafanyabiashara kabla ya janga la moto.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la masoko ya Kariakoo (KMC), Sigsibert Valentine, amesema kazi nyingine inayoendelea ni kupanga biashara kulingana na eneo husika pamoja na kufuatilia madeni ya waliokuwa wafanyabiashara wa soko la kariakoo.
Valentine amezitaja faida mbalimbali ambazo zitapatikana pale mradi huo utakapokamilika kuwa ni kuongezeka kwa nafasi za biashara kufikia 3,500, ajira zisizo za moja kwa moja zisizopungua 4,000, kuboresha mandhari ya jiji la Dar es Salaam ambalo ni kitovu cha biashara nchini.
Fursa ni nyingine ni wafanyabiashara kuwa na uwezo wa kufanya biashara kwa masaa 24, mapato ya Serikali kuongezeka maradufu kupitia tozo, ada na ushuru, lakini pia kuendeleza historia ya soko la Kariakoo kama kivutio cha utalii”
Kuhusu muda rasmi wa kurejea wafanyabiashara sokoni Kariakoo, Valentine amesema taarifa rasmi itatolewa na Serikali mara baada ya kukamilika kwa hatua za mwisho za mradi wa ujenzi.
Kuhusu madeni ya wafanyabiashara, Valentine amesema takwimu za shirika la masoko ya kariakoo zinaonesha kuwa sh. 497,773,019.00 madeni ambayo walilimbikiza kwa muda mrefu ambapo madeni hayo yanapaswa kuwa yamelipwa na wafanyabiashara kabla ya kurejea sokoni ili wapate nafasi ya kusajiliwa na mfumo.
Amesema hadi sasa kiasi cha sh. 15,830,977.71 sawa na asilimia 3 ya deni linalodaiwa kimekusanywa hadi Aprili 2024
Amewataka wafanyabiashara kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kulipa deni alilokuwa amelimbikiza kabla ya kusitisha shughuli za biashara Julai 10, 2021 kwenye soko hilo.
“Kwa taarifa hii, Shirika la Masoko ya Kariakoo linapenda kuwakumbusha wafanyabiashara kutumia kipindi hiki kifupi kilichobaki kabla ya ufunguzi rasmi wa soko kukamilisha ulipaji madeni yao hatua itakayoondosha malalamiko na usumbufu wakati wa kuomba nafasi,”amesema.
Mbali na hayo, Valentine amesema kutokana na maboresho yanayofanyika katika uendeshaji wa biashara katika soko jipya la Kariakoo na maagizo ya Serikali kutumia mifumo ya kielektoniki ili kuleta tija, Shirika litatumia mfumo wa kielektoniki wa TAUSI kutangaza maeneo ya biashara na kukusanya mapato.
“Shirika halitaruhusu mfanyabiashara mwenye deni la awali kupata umiliki wa eneo la kufanya biashara katika Soko la Kariakoo.”
Valentine amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wote wa soko la Kariakoo wakiwemo wafanyabiashara, Mamlaka za usimamizi na udhibiti wa majanga pamoja na kodi kuhakikisha soko litakapoanza kazi linakuwa na viwango vya kimataifa vya usalama ili kuleta ufanisi na tija katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto