December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania, Uturuki zatia sainiya hati sita za Makubaliano

Na Penina Malundo, TimesmajiraOnline, Uturuki

 TANZANIA  na Uturuki zimetiliana hati sita za Makubaliano (MoUs) zenye lengo la kurahisisha ushirikiano katika maeneo mbalimbali ikiwemo masuala ya elimu ya juu, ushirikiano wa kiuchumi ,Masuala ya Kiitifaki na kubadilishana utamaduni.

Akizungumza baada ya kushuhudia kusainiwa kwa makubaliano hayo, Rais wa  Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania haijawahi kurudi nyuma kuthamini mahusiano baina ya nchi hizo mbili.

Amesema ujio wake nchini Uturuki ni kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo mbili na kujikita kwenye majadiliano  hayo waliyokubaliana kushirikiana ya kidiplomasia

“Kwa upekee kabisa nipende kukushukuru,Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan  na Serikali ya watu wa Uturuki kwa mapokezi  makubwa mliotupatia pamoja na ushirikiano tulio nao baina ya Serikali zetu,”amesema na kuongeza;

“Uturuki imekuwa mshirika wa thamani kwa Tanzania na ziara hii inasisitiza dhamira ya kuenzi ushirikiano huo uliopo.”

Aidha amesema uhusiano huu umeongeza kufungua njia kwa wataalamu wa Uturuki kuchangia katika kuleta mabadiliko ya Tanzania kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ya mradi wa  reli ya kisasa (SGR) inayounganisha Tanzania na nchi nyingine jirani.

Akizungumzia Mikataba hiyo, Rais Samia amesema  ili kutekeleza mikataba hiyo iliyoafikiwa, wamewaelekeza mawaziri wenye dhamana na timu zao za wataalamu kwa pamoja kukutana na kuja na mkakati wa kuweka mikakati ya utekelezaji wa maeneo ya ushirikiano.

“Ninashukuru sana na kuheshimiwa kuwa katika nchi hii nzuri. Natanguliza shukrani zetu za dhati kwako kwa mkutano wenye tija sana na kwa kujitolea kwako kutekeleza uhusiano thabiti wa ushirikiano kati ya serikali zetu,” amesema.

Akizungumzia uhusiano wa kidiplomasia, alisema, “Nitakuwa na mambo machache ya kuongeza kwa kuwa kaka yangu Rais Erdogan ameangazia mengi tuliyojadili. Kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba Tanzania ilirejesha dhamira yake ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu na rasmi.

Serikali ya Uturuki kwa ushirikiano wake wa Kimaendeleo na usaidizi wa kutushika mkono katika elimu katika sekta nyinginezo nchini Tanzania, hasa kwa Uwekezaji muhimu katika miundombinu na maendeleo ya rasilimali watu.”

Kuhusu kukuza biashara na uwekezaji, Rais Samia, amesema Tanzania inalenga kushirikiana na sekta binafsi ya Uturuki kuhakikisha uwekezaji unazidi kukua baina ya nchi hizo mbili.