November 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU Tabora yabaini miradi isiyo na ubora

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora imefuatilia utekelezwaji miradi 15 ya maendeleo yenye thamani ya sh bil 5.6 ili kujiridhisha kama kazi iliyofanyika inaendana na thamani ya fedha iliyotumika.

Akitoa taarifa kwa waandishi na habari jana Mkuu wa Taasisi hiyo Mkoani hapa Mhandisi Abenry Mganga alisema katika kipindi cha Januari-Machi 2024 Ofisi yake imetekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo kufuatilia utekelezaji miradi hiyo.

Amebainisha kuwa miradi iliyofuatiliwa ni ya sekta ya elimu, afya, maji na barabara na kati ya hiyo miradi 3 ilibainika kuwa na kasoro mbalimbali ambapo walitoa maelekezo ya kurekebishwa kasoro zilizopo haraka iwezekanavyo.

Mhandisi Mganga ametaja miradi iliyobainika kuwa na kasoro kuwa ni ujenzi wa shule ya msingi Matinje iliyopo katika kata ya Mwanshiku Wilayani Igunga uliogharimu sh mil 463 ambao ulibainika kuwekewa milango isiyo na ubora.

‘Baada ya kubaini kasoro hii tulielekeza Msimamizi wa mradi kutomlipa mzabuni hadi atakapobadilisha milango yote isiyo na ubora kwa kuwa haiendani na thamani ya fedha iliyotolewa kwa kazi hiyo, hili lilitekelezwa kwa asilimia 100’, amesema.

Mradi mwingine uliokuwa na kasoro ni ujenzi wa shule mpya ya Msingi Chief Kabikabo iliyopo katika kata ya Puge Wilayani Nzega wenye thamani ya sh mil 361.5 ambapo manunuzi ya vifaa yalikuwa makubwa kuliko fedha iliyotengwa.

Amefafanua kuwa uchunguzi ulibaini kuwa Msimamizi alinunua baadhi ya vifaa kwa idadi kubwa kuliko idadi halisi iliyotakiwa na baadhi ya vif aa vilinunuliwa kwa bei ya juu kuliko iliyokubaliwa hivyo kuongeza gharama kwa sh mil 30.

Mhandisi Mganga ametaja mradi mwingine uliokutwa na kasoro kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Afya Misha katika kata ya Misha, Manispaa Tabora ambao ulibainika kutokamilika kwa wakati kutokana na fedha zilizotengwa kuisha mapema.

Amefafanua kuwa mradi huo ulitekelezwa kwa awamu 2 na kugharimu sh mil 250 kwa kila awamu lakini haukukamilika kwa wakati kutokana na kilichoelezwa kuwa fedha ziliisha kutokana na gharama za vifaa kupanda wakati ukitekelezwa.

Aidha ameongeza kuwa sababu nyingine iliyoelezwa ni kuongezeka kwa jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji na la kufulia ambayo hayakuwepo kwenye bajeti ya awali, katika miradi hii 2 TAKUKURU imeanzisha uchunguzi wa kina.

Mganga amewashukuru wananchi, vyombo vya habari na taasisi mbalimbali za umma na binafsi zilizopo Mkoani hapa kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo ili kufanikisha majukumu yake, aliomba ushirikiano huo uendelee.

Pichani ni Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Tabora Mhandisi Abnery Mganga na picha ya Ofisi ya TAKUKURU Mkoa.